27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 12, 2024

Contact us: [email protected]

WALIOVUNJIWA KIVULE WAMWANGUKIA JPM

Rais Dk. John Magufuli
Rais Dk. John Magufuli

Na MWANDIHI WETU, DAR ES SALAAM

WAKAZI wa Kata za Kivule na Msongola wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam waliovunjiwa nyumba zao wamemwomba Rais Dk. John Magufuli kuwatembelea kwenye makazi yao ili wamweleze unyama waliofanyiwa na kikundi kinachojiita Umoja wa Kikristo Tanzania (UVIKIUTA).

Wakazi hao zaidi ya 2000 ni miongoni mwa wamiliki wa nyumba 500 zinazodaiwa kuvunjwa kimakosa kwa amri ya Baraza la Ardhi la Wilaya ya Temeke.

Wakizungumza na MTANZANIA mwishoni mwa wiki, baadhi ya wakazi hao walisema mtu pekee ambaye wanaona anaweza kuwasaidia ni Rais Dk. Magufuli kwani wanao uhakika kwamba waliowafanyia unyama huo wana mkono wa mtu mzito aliyeko serikalini.

“Kama rais wetu (Dk John Magufuli ) anatusikia tunamwomba aje hapa katika ziara zake za kushtukiza ili tumweleze ukweli wa jambo hili, kuna wateule wake wachache wameamua kututesa na kutufanyia hila, hawa wana mkono wao humu. Hii si mara ya kwanza, kila wakijisikia wanakuja kutubomolea nyumba bila haki yoyote” alisema mmoja wa wananchi hao Aneth Athuman.

Naye Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) aliiomba Serikali kukifanyia uchunguzi kikundi cha Uvikiuta kwani huenda kimetumika kubeba ajenda za watu wengine.

Mwita ambaye alikwenda kutoa misaada ya kibinadamu kwa wananchi waliobomolewa nyumba zao alisema kuna baadhi ya wateule wa rais wapo nyuma ya kikundi hicho ambacho kimejificha kwenye mgongo wa dini kuhodhi eneo kubwa la ardhi kinyume cha taratibu.

“Ukitaka kujua kwamba huu unyama una mkono wa baadhi ya wateule wa Rais, angalia namna viongozi hao walivyokaa kimya hadi sasa bila kuchukua hatua, leo hii hatumwoni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akija hapa kusikiliza kero za wananchi kama alivyofanya maeneo mengine.

“Kama RC Makonda alifanya ziara maeneo mbalimbali ya Dar es salaam na baadhi ya mikutano yake ikaripotiwa ‘live’ na vyombo vya habari kwa nini asije hapa akawasikiliza wananchi ambao wamebomolewa nyumba zao bila hatia, kama hakuna ajenda ndani yake ni nini?,” alihoji Waitara.

Wiki iliyopita Polisi wilayani Temeke kwa kushirikiana na dalali wa mahakama walibomoa nyumba 500 za wakazi wa Kivule na Msongola kwa madai kuwa Uvikiuta wameshinda kesi ya ardhi namba 73 ya mwaka 2014 ambapo iliamriwa nyumba hizo zibomolewe.

Hata hivyo wananchi wanadai kuwa hati iliyotolewa na mahakama hiyo inahusu nyumba tano tu na si vinginevyo.

Washtakiwa katika kesi hiyo walitajwa kuwa ni Elia Mharage, Astria Charles, Daud Zebedayo na Chacha Marwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles