|Leonard Mang’oha, Dar es Salaam
Waziri wa Ulinzi Dk. Husein Mwinyi, amewahimiza Waislamu nchini kudumisha amani na kuacha vitendo viovu vitakavyosababisha kutoweka kwa tunu hiyo.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo Jumatano Agosti 22, katika swala ya Eid iliyofanyika kitaifa katika Uwanja wa Msife Moyo Vingunguti jijini Dar es Salaam.
Amesema amani ndiyo tunu kubwa zaidi ambayo taifa limejaaliwa na kwamba ikitoweka hakutakuwa na nafasi ya kufanya ibada.
“Kama mlivyosema tunu hii ndiyo kubwa zaidi, bila tunu hii hakuna nafasi ya kufanya ibada, kwa hiyo tuache vitendo vya uvunjifu wa amanio ambavyo matokeo yake huwaathiri zaidi wanawake na watoto,” amesema.
Aidha, Dk. Mwinyi amelitaka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kuhakikisha linaleta tija kwa Waislamu wote na taifa kwa ujumla.
“Niwapongeze kwa juhudi mbalimbali ambazo mmezifanya hasa utoaji wa huduma katika jamii ikiwamo elimu, niwasisitize kuliombea taifa letu ambalo linapitia changamoto nyingi pamoja na Rais wetu John Magufuli,” amesema Dk. Mwinyi.