22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mwigulu awataka polisi kusaidia wanyonge

NA RAMADHAN HASSAN, DODOMA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, jana alianza ziara yake ya kwanza mkoani Dodoma tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo kwa kutoa wito kwa Jeshi la Polisi kuwasaidia wananchi wanaoonewa na wenye nguvu.

Akizungumza na makamanda wa polisi wa wilaya saba za Mkoa wa Dodoma, maofisa, wakaguzi na askari wa kawaida, Waziri Mwigulu alisema wananchi wanyonge wanaonewa na watu wenye nguvu hivyo ni kazi ya jeshi hilo kuwasaidia ili waweze kupata haki.

“Wapo watu wanaoonewa na wenye nguvu, tuwasaidie ili yeyote anayeonewa aone uonevu umekoma, tuwe ngao kwa wanaolia kwa kuonewa,” alisema Waziri Mwigulu.

Aidha, waziri huyo alisema Jeshi la Polisi licha ya kupambana na mtandao haramu wa wauzaji wa dawa za kulevya linatakiwa kuongeza nguvu katika mapambano hayo ili liweze kuufyeka

“Tukibaini mnyororo huo na kuukata kila Mtanzania atajua uwepo wetu. Hakuna siku tumewahi kuwa na mashaka na ninyi, kinachotakiwa ni kuzingatia miiko ya kazi, fedha za dili zinapopungua hata ukwapuaji wa hapa na pale unaongezeka.

“Miongoni mwa matatizo nitakayoshughulika nayo ni makazi ya askari, nitatafuta njia ya kushughulikia tatizo hilo ikiwemo kutumia nguvu mbadala,” alisema Waziri Mwigulu.

Waziri huyo pia alifanya ziara katika makazi ya askari yaliyopo eneo la Barabara ya Iringa na Nzuguni na kuahidi kuyaboresha pamoja na kujenga mapya.

“Ingawa bajeti ni ndogo lakini nitahakikisha askari wanakuwa na makazi mazuri na nitaanza na maeneo ambayo hayahitaji fidia,” alisema Waziri Mwigulu.

Aidha, waziri huyo alisema Serikali inakusudia kujenga nyumba za mkoani Dodoma na aliwaasa viongozi wa Serikali kutoa kipaumbele kwa upatikanaji wa magari ya polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, aliyekuwa ameambatana na Waziri Mwigulu katika ziara hiyo, alisema jeshi hilo mkoani Dodoma litaendelea kufanya kazi kwa weledi na kujituma ili kutimiza  malengo ya uwepo wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles