27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mwigulu acharuka polisi kutolipwa mishahara

nchemba1Na HERIETH FAUSTINE – DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, amemtaka Ofisa Utawala Mkuu wa Uhamiaji kufika ofisini kwake leo asubuhi kueleza sababu zilizofanya askari polisi wapya 297 kushindwa kulipwa mishahara yao katika kipindi cha miezi minne.

Hayo aliyasema jana Dar es Salaam, alipokutana na makamishna, maofisa na watumishi wa Idara ya Uhamiaji wakati alipokwenda kukagua kazi mbalimbali katika idara hiyo.

Alisema wakati akiwa bungeni aliulizwa swali la kwanini askari hao walishindwa kulipwa mishahara yao katika kipindi cha miezi minne.

“Juzi bungeni niliulizwa swali wakati wa kipindi cha maswali na majibu, sababu za askari wapya kutopata malipo yao kwa wakati, nilipofuatilia nikagudua tatizo lipo kwetu.

“Niliongea na Waziri wa Utumishi, akanielezea kuwa sisi hatukupeleka majina na hatukuyaweka kwenye mfumo wa malipo, nataka kujua tatizo liko wapi na ni nani anayehusika kuyaweka majina yale. Je, ni ofisa wa Uhamiaji au wizarani?” alihoji Nchemba.

Alisema kutokana na askari kutokuwa na tabia ya kulalamika mara kwa mara, wamekuwa wakiwacheleweshea mishahara yao na hata kutoongezewa pindi wanapopandishwa vyeo na kufanya kuwa kigezo cha wao kuwa na sababu mbalimbali za kusingizia.

Nchemba alisema amegundua maofisa utawala kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani wamekuwa tatizo kubwa baada ya kutembelea idara mbalimbali zilizopo chini ya wizara hiyo.

“Kwa sababu askari hawawezi kuandamana, kulalamika, mnachukulia sawa tu, ukiongea na watu wa utumishi wanasema majina hayajapita kwao na sasa tunaenda kuandaa bajeti ya miaka ijayo.

“Mmeshindwa kupeleka hata orodha ya  watu waliokaa miaka minne, miezi sita, saba na vyeo vipya ili kupata mishahara mipya na mpo mnashughulikia watumishi, hamjafanya hayo mpaka mimi naanza kukaa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha kumwambia kuna watu hawajalipwa wakati nyinyi mpo.

“Nahitaji kuonana nanyi kesho (leo) saa mbili asubuhi ofisini kwangu, mnafanya mambo kimzahamzaha huku watu wanapata shida, ninyi mmelipwa wakati askari wako porini hawajalipwa mnaona kawaida, kumtoa mtu Nachingwea na kumpeleka Mara hana ndugu yeyote na kutomlipa miezi minne mnaona kawaida tu,” alisema Nchemba.

Naye Ofisa Utawala Mkuu wa Uhamiaji, Mulegi Majogoro, alisema mishahara ya askari wapya ilishindwa kutolewa kwa sababu ya kuwapo kwa makosa mbalimbali katika vyeti vyao.

Alisema baadhi ya vyeti vya askari hao vilikuwa na tofauti ya majina pamoja na miaka jambo lililosababisha kushindwa kulipwa mishahara yao kwa miezi minne kutokana na kuvichunguza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles