25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mwenyekiti SIMCU asimamishwa Uongozi kwa wizi wa Simu

Na Derick Milton, Simiyu

Chama Kikuu cha Ushirika Mkoani Simiyu (SIMCU Ltd 2018) kimemsimamisha Mwenyekiti wa Chama hicho, Charles Madata kwa tuhuma za wizi wa simu pamoja na fedha za wakulima wa pamba.

Hatua hiyo imefikiwa leo Januari 25, kwenye mkutano mkuu wa chama hicho baada ya wajumbe wa mkutano huo kuridhia hatua za zilizochukuliwa na bodi ya chama hicho kumsimamisha kwa muda.

Awali akisoma tuhuma dhidi ya Mwenyekiti huyo, Kaimu Meneja wa Chama hicho, Ednard Magenda alisema Bodi hiyo ilimsimamisha Mwenyekiti wa chama hicho tangu Machi mosi, 2020.

Taarifa hiyo imesema kuwa Mwenyekiti huyo anadaiwa kuiba simu ya aliyekuwa Meneja wa SHIRECU 1984 Ltd Mzee Muhangwa wakati wakiwa kwenye kikao jijini Dodoma.

“Mwenyekiti alikamatwa akiwa hapa mjini Bariadi na polisi mkoa wa Simiyu kuthibitisha tukio hilo la wizi wa simu ambayo walimkutana nayo…baadaye aliombewa msamaha kwa mwenye simu kisha akairejesha pamoja na gharama nyingine,” imesema taarifa hiyo.

Aidha, Mwenyekiti huyo anadaiwa kuhusika na wizi wa pesa za wakulima bora ambao walipewa zawadi na Chama Kikuu, mshindi wa kwanza Sendama Nzumbi Sh 500,000 ambapo mwenyekiti huyo alimpatia mshindi huyo bahasha yenye Sh 100,000 badala ya 500,000 na kuficha Sh 400,000.

“Mshindi wa pili, Gwishida Hunge Sh 300,000 alimpatia bahasha yenye Sh 100,000 na kuficha Sh 200,000 na mshindi wa tatu, Makoye Ngaga akimnyima pesa yake bila sababu za msingi,” imesema taarifa hiyo.

Aidha, Mwenyekiti huyo pia anakabiliwa na tuhuma za kughushi saini ya mtumishi ambaye ni Meneja wa Nasa Amcos, Deogratius Faini pamoja na kuchukua mshahara wake wa mwezi Desemba 2019 kiasi cha Sh 295,911.

Akijibu tuhuma hizo wakati wa kikao hicho, Mwenyekiti huyo amesema kuwa tuhuma hizo siyo za kweli na hakuna kikao chochote cha Bodi ya Chama hicho ambacho kimekaa na kumuita kwa ajili ya kujibu tuhuma hizo.

“Nimesikitishwa na tuhuma hizi, ni kitu kinachoonekana cha kutengeneza wala sijui haya mambo wamekaa kwenye kikao gani na mimi sikuwepo…kuhusu fedha za malipo ya wakulima, ni uongo na kuhusu simu siyo kweli,’’ amesema Madata.

Kwa upande wake, Kaimu Mrajisi wa Ushirika Mkoa, Ibrahimu Kadudu ameipongeza Bodi ya Chama hicho kwa kuchukua hatua za kumsimamisha kiongozi huyo ambapo amesema ofisi yake inaendelea na uchunguzi na itatoa adhabu zaidi.

Naye, Mchunguzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa, Aquilinus Shiduki amesema taasisi hiyo ilipokea tuhuma dhidi ya kiongozi huyo toka Bodi ya Simcu ambapo amesema uchunguzi unaendelea na uko katika hatua za mwisho.

Kutokana na hali hiyo wajumbe wa mkutano mkuu huo wameridhia kiongozi huyo kuendelea kusimamishwa uongozi ndani ya chama hicho hadi pale uchunguzi dhidi ya tuhuma zake utakapokamilika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles