25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

MWANGA MPYA TANGA FRESH

Na WAANDISHI WETU -TANGA

WAKATI kwenye baadhi ya maeneo madini yanaonekana kuwa mkombozi, kwa wengine maziwa ni kila kitu kwenye maisha yao, ndiyo maana wanayaita dhababu nyeupe.

Hii ndiyo maana licha ya kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye ng’ombe wengi, kila siku lita za maziwa  64,628.5 zinaingia nchini kutoka mataifa mengine. Hali hiyo ndiyo inayotoa changamoto kwa kampuni za uzalishaji maziwa nchini, ikiwamo Tanga Fresh ya Tanga kufikiria namna ya kuongeza uzalishaji kila uchwao.

Kwa sasa Tanga Fresh ambayo imepata fursa nyingine ya soko kutokana na wafanyakazi zaidi ya 30,000 watakaokuwa wanajenga bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga, inafikiria kuongeza uzalishaji wake kwa zaidi ya asilimia 100.

Meneja wa ufundi wa kiwanda cha Tanga Fresh, Adam Gamba, anasema: “Kwa kuwa sisi ni wazalishaji wa maziwa na bidhaa zake, tunatarajia kuwa watu wengi watakaoshiriki mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta watatumia bidhaa za maziwa kwa matumizi yao ya kila siku.

“Kazi watakazokuwa wanazifanya, kwa namna moja au nyingine watahitaji virutubisho na lishe kujenga afya zao.

“Kazi hiyo ya ujenzi inahusisha matumizi ya nguvu nyingi na wakati mwingine katika mazingira ya vumbi, hivyo maziwa yatakuwa ni muhimi sana kulinda afya za wafanyakazi,” anasema Gamba.

Aidha meneja huyo anautazama mradi huo wa ujenzi wa bomba la mafuta kama fursa si tu kwa Tanga Fresh pekee bali hadi kwa wafugaji wadogo wadogo.

“Sisi tunafanya kazi na chama kikuu cha msingi kinachojulikana kama Tanga Dairies Coo-perative Union ambao wanamiliki hisa asiliamia 42.5, huku mwekezaji kutoka Uholanzi (DOTF) akimiliki asilimia 52.5 na uongozi wa kiwanda hicho una asilimia 5,” anasema.

Gamba anasema kwa sasa kiwanda kinapokea wastani wa lita 42,000 za maziwa kila siku ingawa uwezo wake ni kusindika lita 50,000 kwa siku. Upungufu wa maziwa kutoka kwa wakulima, anasema ni moja ya sababu inayofanya wasifikie lengo. Pamoja na changamoto hiyo ya kutopata maziwa ya kutosha mahitaji yao, anasema wana mpango wa kupanua kiwanda hicho kiwe na uwezo wa kuzalisha lita 120,000 kwa siku.

Gamba anasema baada ya upanuzi wa kiwanda, ili waweze kupata lita 120,000 za maziwa, watawafikia wafugaji wengi zaidi kutoka kwenye mikoa mbalimbali nchini tofauti na sasa ambapo wanachukua kutoka Tanga, Pwani, Morogoro na Kilimanjaro pekee.

Anasema kiwanda hicho kimetoa ajira za moja kwa moja 142 na nyingine zaidi ya 20 zisizo za moja kwa moja, huku kinafanya kazi na wafugaji 6,000. Gamba anasema upanuzi ukikamilika, ajira mpya kupitia kwa wafugaji zitaongezeka.

“Upanuzi huu utawahakikishia wafugaji kuwa kila tone la maziwa litakalozalishwa litakuwa na soko la uhakika,” anasema. Kiwanda cha Tanga Fresh kilianzishwa mwaka 1997 kikiwa na uwezo wa kuzalisha lita 360,000 kwa mwaka. Kwa sasa uwezo wake umeongezeka na kinazalisha lita zaidi ya milioni 10 kwa mwaka. Mwaka jana kilisindika lita milioni 13 na kulipa kodi isiyopungua Sh milioni 700.

Idadi ya ng’ombe

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Chakula Duniani (Fao) za mwaka 2012, Tanzania ni miongoni mwa nchi 15 zenye ng’ombe wengi duniani.

Inashika nafasi ya tisa kwa wingi wa ng’ombe wa kisasa na kienyeji. Ni ya tatu barani Afrika baada ya Sudan na Kenya kwa idadi kubwa ya ng’ombe wa maziwa. Hadi mwaka 2012, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikadiria Tanzania kuwa na ng’ombe wa maziwa wasiopungua milioni 6.9, kati yao wa kisasa walikuwa 800,000.

Wastani wa uzalishaji wa maziwa kwa ng’ombe wa asili ni lita 180, hivyo ng’ombe milioni 6.1 wanaweza kuzalisha lita bilioni 1.1 kwa mwaka. Takwimu za Shirika la Chakula Duniani (FAO) mwaka 2014, zinaonyesha Kenya inaongoza Afrika kwa uzalishaji wa maziwa ya ng’ombe wakati Tanzania ikishika nafasi ya tisa.

Kenya ina ng’ombe wa maziwa wasiopungua milioni tatu. Unywaji wa maziwa nchini humo unafikia lita 130 kwa kila mtu kwa mwaka, Tanzania ni chini ya lita 50. WHO inapendekeza kila mtu kunywa walau lita 200 za maziwa kwa mwaka. Viwanda vyetu vya kuchakata bidhaa za maziwa vinalazimika kutumia asilimia 27 hadi 30 ya uwezo wake kutokana na uhaba wa maziwa yanayozalishwa kwa mwaka nchini.

Uzalishaji wa maziwa

Uzalishaji wa maziwa kwa sasa ni kati ya lita bilioni 2.1 hadi bilioni 2.7.

Kutokana na idadi ya watu waliopo nchini, wanaokadiriwa kuwa milioni 55, uzalishaji wa maziwa unatakiwa kufika lita bilioni 11 kwa mwaka, hivyo pia ng’ombe wa kisasa wanalazimika kuwa zaidi ya milioni tano.

Asilimia 10 ya maziwa yanayozalishwa kila mwaka huingia katika soko rasmi na kiasi kinachobaki kinatumika vijijini na kuuzwa katika masoko ya miji jirani.

Tanzania ina viwanda 75 vya kusindika maziwa  vyenye uwezo wa kusindika lita 640,000 kwa siku, lakini kwa sasa ni 65 tu vinavyofanya kazi na vinasindika lita 167,070 kwa siku ambayo ni sawa na asilimia 26.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles