24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI MKUU WA KENYA ‘ATEKA’ MKUTANO WA MAJAJI NCHINI

  • Samia ataka majaji, mahakimu, kurudisha heshima ya mahakama

NA Mwandishi Wetu -DAR ES SALAAM

JAJI Mkuu wa Kenya, David Maraga, amepokewa kwa heshima ya kipekee kwenye mkutano wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Jumuiya ya Madola unaofanyika hapa nchini.

Jaji Maraga amekuwa kivutio katika siku ya kwanza ya mkutano huo, utakaofanyika kwa siku tatu mfululizo.

Hali hiyo ilijitokeza jana baada ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, kutambulisha majaji wakuu 11 kati ya 12 waliohudhuria mkutano huo kisha kusema.  “Napenda kumtambulisha Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga, ambaye alifika tangu Jumatano (Septemba 20) na akafikia katika Hoteli ya Land mark,” alisema.

Baada ya maelezo hayo, Jaji Maraga alisimama huku washiriki wakimshangilia kwa kupiga meza na wengine wakipiga makofi.

Majaji wengine 11, walitambulishwa tu kwa kutajwa majina yao na nchi wanazotoka tofauti na Maraga, ambapo Profesa Juma alisema anamtambulisha kwa upekee.

Pia Jaji Maraga alikuwa na walinzi kadhaa ambao walikuwa hawataki apigwe picha, wakati akiwa nje ya ukumbi wa mkutano kwa ajili ya kupata kifungua kinywa.

Mara baada ya kupata kifungua kinywa, Jaji Maraga, aliongozana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Juma  na yule wa Zanzibar, Omar Makungu, kwenda kwenye chumba maalimu.

Wakati huo, baadhi ya waandishi wa habari walijaa nje ya chumba hicho wakisubiri Jaji Maraga atoke ili waweze kuzungumza naye.

Kabla ya Jaji Maraga na wenzake kutoka kwenye chumba hicho, mtu mmoja aliyedhaniwa kuwa ni kati ya walinzi wake, alitoka ndani ya chumba hicho na kuwaeleza waandishi kuwa,  Jaji Maraga amekataa kuzungumza na waandishi wa habar) kwa kuwa yupo ugenini kwa ajili ya mkutano tu.

Umaarufu wa Maraga

Jaji Maraga amejipatia umaarufu mkubwa duniani baada ya kufuta matokeo ya uraisi nchini Kenya.

Agosti 31, mwaka huu Mahakama ya Juu ya Kenya ilifutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 8, mwaka huu yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyata dhidi ya Raila Odinga.

Baada ya Tume ya Uchaguzi ya Kenya kumtangaza Uhuru kuwa mshindi, Odinga aliyegombe kwa bendera ya muungano wa National Super Alliance (NASA), alikata rufaa kupinga matokeo hayo ya urais.

Baada ya jopo la majaji kusikiliza shauri hilo, Jaji Maraga alitangaza matokeo akisema kati ya majaji sita waliosikiliza kesi hiyo, wanne waliafiki kuwa uchaguzi huo haukufanyika kwa mujibu wa Katiba na sheria za uchaguzi nchini humo, hivyo matokeo yake ni batili.

Baada ya kufuta matokeo hayo, mahakama hiyo ilitaka uchaguzi mpya wa urais ufanyike tena ndani ya siku 60, ambapo sasa Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya, imetangaza uchaguzi huo kufanyika Oktoba 26, mwaka huu.

Makamu wa Rais

Awali akifungua mkutano huo, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliwataka majaji na mahakimu kurudisha imani ya wananchi kwa mahakama kwani mhimili huo umekuwa ukilalamikiwa kwa kuchelewesha kesi.

“Kuna malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu ucheleweshaji wa kesi, fedha na utaratibu wa kupata haki, vitu vinavyosababisha kupoteza uaminifu na kuaminika kwa mahakama.

“Mmejumuisha mada hizo katika mkutano, hivyo majaji na mahakimu mnatakiwa kuhakikisha mahakama inarudi katika hali yake,”alisema.

Samia alisema katika ujenzi wa mahakama madhubuti, huwezi kwenda tofauti na juhudi za wazi za  Serikali katika kupambana na rushwa na umasikini.

Jaji Prof. Ibrahim

Naye Jaji Mkuu Profesa Ibrahimu Juma, alisema hadi kufikia mwaka 2020 mahakama itakuwa imejenga mahakama za wilaya 48, mahakama za mwanzo 100, mahakama za hakimu mkazi 14 na mahakama kuu 13.

Aliwataja majaji wakuu waliohudhuria mkutano huo kuwa ni  Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga, Salamo Injia (Papua New Guinea), William Bailhache (Jersey), Jaji Mkuu  Zanzibar, Omar Makungu, Jaji Mkuu Peter Shivute wa Namibia na majaji wengine saba kutoka nchi mbalimbali wanachama.

Washiriki katika mkutano huo ni 354 ambapo malengo ya mkutano huo ni kuwajengea uelewa wajumbe kuhusu uhuru wa mahakama, mikataba ya kimataifa, maendeleo ya kisheria, upatikanaji wa huduma ya haki na changamoto za mahakama katika usikilizaji wa mashauri.

Mada mbalimbali zitajadiliwa ikiwemo masuala ya ugaidi ambayo changamoto yake ni namna gani ushahidi unavyotumika.

Mkutano huo ulioanza jana, unatarajiwa kufungwa  Septemba 27 na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed  Shein, ambapo maudhui ya mkutano huo ni mahakama madhubuti, inayowajibika na jumuishi.

Changamoto mahakama za Afrika

Kumekuwepo na malalamiko kwa mahakama za kiafrika zikilalamikiwa kuchelewesha kesi na hivyo kufanya baadhi ya watu kukosa haki ama kutopata haki zao kwa wakati.

Mahakama za mataifa hayo pia zinadaiwa kukithiri kwa vitendo vya rushwa, hatua inayofanya wenye fedha kupoka haki za wanyonge.

Pia mhimili huo umekuwa ukidaiwa kuingiliwa na mihimili mingine hivyo kushindwa kutimiza wajibu wake kama inavyopaswa. Malalamiko kama haya pia yapo nchini na hivi karibuni Jaji Mkuu wa Tanzania, aliyakanusha vikali kwa kusema mahakama ina uhuru wake.

Changamoto nyingine inayokabili mahakama ni kutokuwa na fungu lake, hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa kutengemea fungu kutoka serikalini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles