DELHI, INDIA
MAHAKAMA ya Jimbo la Rajasthan nchini India jana imetoa adhabu ya kifungo cha maisha jela dhidi ya mwalimu maarufu wa kiroho Asaram Bapu kwa kumbaka msichana aliyekuwa mfuasi wake mwaka 2013.
Hukumu dhidi ya Bapu (77) ilisomwa ndani ya gereza moja la mji wa Jodhpur, jimbo la Rajasthan kutokana na hofu kuwa wafuasi wake huenda wakafanya vurugu.
Kesi hiyo ni ya karibuni katika mfululizo wa kesi kubwa za ubakaji nchini India ambazo zimesababisha maandamano ya umma na kuzusha maswali kuhusu namna polisi inavyozishughulikia kesi hizo.
Agosti mwaka jana, mwalimu mwingine maarufu wa kiroho, D.k Saint Gurmeet Singh Ram Rahim Insan, alihukumiwa miaka 20 jela kwa mashitaka ya kuwabaka wanawake wawili wafuasi wake.
Bapu amekanusha mashtaka hayo na anaweza kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo katika Mahakama ya Juu.