ATLANTA, MAREKANI
MWALIMU mstaafu wa somo la English katika shule ya juu ya sekondari, Yvonne Mason anasema barua aliyopokea kutoka kwa Rais Donald Trump ingepata alama chache na ameirudisha Ikulu ya Marekani, White House.
Mkazi huyo wa Atlanta, ambaye alistaafu baada ya kufundisha kwa miaka 17 katika jimbo la Carolina Kusini alisahihisha makosa ikiwamo ya msamiati barua hiyo yenye sahihi ya Trump ikiwamo mifano 11 ya matumizi mabaya ya harufi ndogo na kubwa kama vile ‘rais’ na ‘taifa.’
‘Iwapo ingeandikwa na mwanafunzi wa shule ya kati, ningeipatia daraja ‘C’ na iwapo ingekuwa shule ya juu, ningeipatia alama ‘D’,” Mason aliliambia gazeti la Greenville News la jimboni humo.
Hakuambatanisha darala aliloipa barua hiyo aliyoisahihisha na kuirudisha White House.
Mason alikiri kuwa barua hiyo kuna uwezekano iliandikwa na mfanyakazi wa Ikulu.
Alipokea barua hiyo baada ya kuandika barua akimuomba Trump akutane binafsi na familia za watu waliopoteza wapendwa wao katika shambulio la silaha moto lililotokea katika shule ya juu huko Parkland, Florida.
“Wakati unapokea barua kutoka ngazi ya juu serikalini, unatarajia kuwa na makosa machache ya kiufundi. Lakini hii wingi wa makosa unatia aibu,” aliliambia gazeti hilo.
Mbali ya hilo, mwalimu huyo alisema kwamba jibu alilopata kutoka White House halikuakisi vyema ombi lake kuhusu familia hizo.