24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

VIONGOZI WA KOREA WAKUTANA TENA

SEOUL, KOREA KUSINI


VIONGOZI wa Korea Kaskazini na Kusini juzi wamefanya mazungumzo yasiyotarajiwa baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kufuta mazungumzo kati yake na Kiongozi wa Kaskazini, Kim Jung-Un.

Hata hivyo, baada ya uamuzi huo wa Trump Alhamisi iliyopita, siku moja baadaye, alilegeza msimamo huo akisema mazungumzo hayo yanaweza kuendelea kama ilivyopangwa.

Picha zilizotolewa na Korea Kusini zimemuonyesha Rais Moon Jae-in akishikana mikono na mwenzake Kim katika upande wa Kaskazini wa ukanda usio na shughuli za kijeshi unaozitenganisha nchi hizi mbili.

Ikulu ya Korea Kusini, Blue House ilisema viongozi hao walifanya mazungumzo kwa saa mbili siku ya Jumamosi mchana katika kijiji kilekile cha mapatano cha Panmunjom, ambako walikutana mwezi uliopita, na kutoa tangazo wakiapa kuboresha uhusiano.

“Walibadilishana mawazo na kujadili njia za utekelezaji wa tangazo la Panmunjom na kuhakikisha ufanisi wa mkutano wa kilele kati ya Marekani na Korea Kaskazini,” ilisema Blue House katika taarifa na kuongeza kuwa Moon angetoa taarifa binafsi baadaye jana.

Awali Trump aliitikisa kanda hiyo kwa kufuta mkutano wake na Kim uliopangwa kufanyika nchini Singapore Juni 12 akitoa sababu za ‘uhasama wa wazi kutoka Pyongyang.’

Lakini katika muda wa saa 24 alibadilisha mwelekeo na kusema mkutano huo unaweza kuendelea baada ya mazungumzo yenye tija kufanyika na maafisa wa Korea Kaskazini.

Uamuzi wa awali wa kufuta mkutano huo wa kilele wa kihistoria uliishtua Korea Kusini, ambayo imekua ikiratibu mawasiliano kati ya Washington na Pyongyang, baada ya miezi kadhaa ya kutukanana na vitisho vya vita kati ya Trump na Kim.

Picha zilizotolewa na Blue House pia zilimuonyesha Moon akishikana mikono na dada yake Kim, Kim Yo Jong.

Dada huyo amekuwa na mchango mkubwa katika mazungumzo ya karibuni na Kusini, ikiwemo kuongoza ujumbe ulioshiriki michezo ya olimpiki ya majira ya baridi mwezi Februari.

Wakuu wa mashirika ya upelelezi wa mataifa yote mawili walikuwepo kwenye mkutano huo kwa mujibu wa picha hizo.

Tofauti na mkutano wa mwezi uliopita, uliofanyika mbele ya kamera za televisheni, mkutano wa Jumamosi ulifanyika kwa usiri wa hali ya juu, ambapo waandishi waliambiwa tu baada ya mazungumzo hayo ya ana kwa ana kukamilika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles