25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mwalimu Nyerere mwanalugha, mwanafasihi wa kukumbukwa

Na ABDULAZIZI Y. LODHI, UPPSALA


UNAPOSOMA historia ya Tanganyika, historia ya Muungano wa Tanzania, historia ya Afrika Mashariki, au hata historia ya Bara la Afrika, huwezi kukwepa jina la Mwalimu Julius Nyerere, Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza wa Tanganyika na vile vile Rais wa Kwanza wa Muungano wa Tanzania.

Licha ya maoni na uamuzi wowote ule wa wasomaji kuhusu Mwalimu Nyerere kama kiongozi mkuu wa kisiasa,  Mwalimu daima atakuwa na nafasi yake maalumu katika historia ya lugha na fasihi ya Kiswahili ingawa Kiswahili hakikuwa lugha yake aliyozaliwa nayo na kukulia, bali alianza kujifunza Kiswahili alipokwenda skuli ya misheni kwenye umri wa miaka 12.

Hayati Mwalimu Nyerere alikuwa mshairi na mtungaji wa vitabu wa kiwango cha juu, lakini katika medani ya fasihi anajulikana zaidi kama mtafsiri wa vitabu viwili muhimu vya William Shakespeare: Juliasi Kaizari (1963), Mabepari wa Venisi (1990) na  Utenzi wa Enjili (viatbu 5, 1997).

Baada tu ya tamthilia ya Juliasi Kaizari kutolewa, ilichezwa kwenye redio ya Sauti ya Unguja, Oktoba 1963, kutungwa na Kamati ya Mila ya Umoja wa Wanafunzi wa Zanzibar (All Zanzibar Students’ Union/AZSU). Kazi hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wa AZSU, Sheikh Ali Miskry wa King George VI Grammar School (Lumumba College ya siku hizi) na Maalim Haidar Jabir aliyekuwa na vipindi vyake vya fasihi kwenye redio ambako mara nyingi hutangaza muhtasari wa muda wa nusu saa wa riwaya mbalimbali za Kiingereza kwa lugha rahisi ya Kiswahili.

Nikiwa Katibu wa AZSU wakati huo, nilimwandikia barua Mwalimu Nyerere kuomba idhini yake ya kuicheza tamthilia ya Juliasi Kaizari kwenye Sauti ya Unguja. Wiki hiyo hiyo Mwalimu alinijibu na kutupatia idhini yake bila kudai  malipo ya mrabaha. Hii ilikuwa mara ya kwanza Juliasi Kaizari kurushwa kwenye redio, nayo ilikuwa Zanzibar, wala si mahali pengine popote.

Baadaye Julai, 1966 nilipokutana ana kwa ana na Mwalimu kwa mara ya kwanza alipotutembelea Chuo cha Walimu, Chang’ombe, nikajitambulisha kwake. Akaniambia alifurahi sana kuonana nami na alinishukuru kwa kazi tuliyoifanya. Hapo nikazungumza naye kidogo kuhusu majina ya wahusika katika mchezo wa Juliasi Kaizari yaliyowekwa jinsi yalivyo katika Kiingereza; nikapendekeza ayawasilishe, au tuseme ayabantuishe, kama Marcus liwe Mariko, Brutus liwe Buruto, Cassius liwe Kasio na Casca liwe Kasiko.

Akaniambia atajaribu kufanya hivyo katika toleo jipya la kitabu hicho. Toleo la pili la Juliasi Kaizari la mwaka1969 lina majina hayo yanayosikika na kuelekea kuwa kama ya Kiafrika wala si ya Kiingereza au Kizungu.

Mwalimu siku zote alijaribu kukipanua Kiswahili kwa kubuni maneno mapya, au kuyapa maneno ya Kiswahili maana na vijimaana vipya na pia kutunga kauli mpya za Kiswahili ambazo mawazo yake tulijifunza kutokana na maandishi ya Kiingereza; mfano mzuri mmoja ni “Kaizari alikuwa mpenda cheo” (Caesar was ambitious), “duara la balaa” (vicious circle) na “mtazamo wa akili” (attitude of mind). Mara mbili- tatu aliwahi kuniuliza kama naweza kupendekeza tafsiri bora ya maneno au kauli fulani.

Julai 1994 tuliposafiri pamoja kwenda na kurudi kutoka Swaziland na Msumbiji, aliniuliza nimpatie tafsiri ya “to accommodate South Africa in our Eastern African community”. Nikampendekezea neno “kujumuisha” kwa maana ya “accommodate” katika muktadha huo. Akakubali.

Nakumbuka Swahiba yangu Marehemu Dk. Nisar Sherali wa Zanzibar kwenye semina moja ya elimu ya watu wazima mjini Dar es Salaam, mwaka 1964 au 1965 alimpatia Mwalimu istilahi ya “ngumbaro” kumaanisha “illiterate” kwa vile wasiojua kusoma na kuandika si “wajinga” na “illiteracy” haiwezi kuitwa “ujinga”

Mwalimu alikubali hapo hapo pendekezo hilo. Alisema Kiswahili ni lugha yenye historia ndefu, msamiati mpana na ni lugha yenye uwezo mkubwa wa kunyumbulika, kwa hivyo lazima tuweze kutafsiri kwa Kiswahili maandishi magumu ya lugha nyingine, maandishi ya zamani na vile vile ya kisasa na pia dhana mpya katika nyanda za siasa, sheria, ufundi wa aina  na taaluma tofauti tofauti.

Mwaka 1973 Profesa  Ali A. Mazrui aliandika  kwenye ukurasa wa 88 katika makala yake ‘The Patriot as an Artist’ katika kitabu cha G. D. Killam (Mhariri) African Writers on African Writing. (uk. 73-90) kwamba: Kwa kutafsiri Shakespeare, Nyerere alichukua kipande cha utamaduni wa ulimwengu mzima na kukifanya kiwe cha kilimwengu zaidi katika lugha ya Kiafrika. Ufanisi huo, kwa uchache, ulikuwa uthibitisho wa lugha ya Kiafrika kuwa chombo cha fasihi. (Tafsiri yangu)

Mwalimu Nyerere hivyo alitia kibamba na kutuandalia njia ya kutayarisha tafsiri nyingine na tafsiri zaidi za Shakespeare – Samuel Stephen Mushi, kwa mfano, alitafsiri tamthilia za Macbeth (Makbeth, 1968) na The Tempest (Tufani, 1969) na Mwalimu mwenyewe akachapisha tafsiri yake ya The Merchant of Venice (Mabepari wa Venisi, 1990). Samuel S. Mushi baadaye alitafsiri tamthilia ya Sophocles King Oedipus (Mfalme Edipode, 1971) na vitabu vingine.

Uchaguzi wa Julius Caesar na The Merchant of Venice haukuwa wa kubahatisha tu, bali, jinsi mambo yote Mwalimu alivyokuwa anafanya, uchaguzi huo ulikuwa kwa makusudi na baada ya kupanga vyema. Nia yake ya kisiasa ilionekana wazi katika tafsiri ya The Merchant of Venice kuwa Mabepari wa Venisi badala ya “Wafanyabiashara wa Venisi,” Muundo wa wingi wa nomino mabepari unaonyesha kuwa kuna zaidi ya bepari mmoja, Antonio, katika hadithi hiyo.

Novemba 23, 1990, Mwalimu alikuja mjini Uppsala, Uswidi, kukizindua kitabu chake The Challenge to the South (The Report of the South Commission). Nilikutana na Mwalimu alipofika Chuo Kikuu chetu. Baada ya hotuba yake iliyohudhuriwa na zaidi ya watu 500, pamoja na maaskofu  takribani watano na wachungaji kadhaa wa misheni waliopata kufanya kazi Tanzania, tulikwenda kunywa chai kwa Askofu Mkuu wa Uswidi katika Makao ya Misheni za Kanisa la Uswidi.

Hapo katika mazungumzo yetu kuhusu mada mbalimbali, Mwalimu  alisema, “Kama ningeitafsiri The Merchant of Venice sasa, wakati huu, basi ningeipa jina jingine. Labda Mfanyabiashara wa Venisi, au Matajiri wa Venisi, au labda Tajiri wa Venisi.” Na akaangusha kicheko kama kawaida yake.

Mwalimu  Nyerere ametunga vitabu vingi kwa Kiswahili na Kiingereza. Baadhi ya vitabu aliviandika kwa Kiingereza kwanza na baadaye alivitafsiri yeye mwenyewe kwa Kiswahili; baadhi aliviandika kwa Kiswahili kwanza na kuvitafsiri kwa Kiingereza na maandishi mengine aliyaandika sambamba kwa lugha mbili za Kiswahili na Kiingereza, sentensi fulani kwanza mara kwa Kiswahili na mara kwa Kiingereza.

Urithi mkubwa na muhimu mno Mwalimu ametuachia ni lugha ya Kiswahili kuwa Lugha yetu ya Taifa ya Tanzania na ya Afrika Mashariki nzima, ingawa bado Kiswahili hakijatambuliwa rasmi na nchi fulani fulani kuwa Lugha yao ya Taifa. Kiswahili ni jambo moja la pekee linalounganisha wananchi wote wa Tanzania na karibu watu wote wa Afrika Mashariki. Mchango huo wa Mwalimu Nyerere ni wa kudumu milele!

Tangu tuonane mara ya kwanza Dar es Salaam mwaka 1966, nilipata fursa mara nyingi ya kuonana na Mwalimu na kuzungumza naye mjini Dar es Salaam, ubalozini Stockholm na Chuo Kikuu cha Uppsala. Miaka ya 1975 na 1978, nilipokuwa Mwenyekiti wa TANU – ASP Tawi la Skandinavia, Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania mjini Stockholm, Sweden, nilipata fursa nyingi ya kuonana na Mwalimu na kuzungumza naye mambo anuwai na kupeana mawazo mema ya kisiasa na ya kifasihi.

Alasiri ya Jumatano ya Julai 27, 1994, Mwalimu alinialika chai nyumbani kwake. Asubuhi hiyo alikutana na viongozi wa Chama cha Wananchi CUF. Kama kawaida yetu, baada ya kusalimiana na kuulizana hali, tukaelezana habari za makala na insha tunazoandika, au vitabu na makala tunazosoma, tukaingia katika mazungumzo makali ya siasa, kama kawaida yetu.

Mwalimu mara nyingi alisisitiza kwamba ”Fasihi ni Siasa!” na ”Kila mwanasiasa ingefaa asome fasihi, hasa kama vitabu vya Shakespeare na Bertolt Brecht, Moliere nakadhalika. ili kukomaa kisiasa na kujiongezea utu mwema. Pia wasome tenzi na mashairi ya Kiswahili kujifunza lugha fasaha, msamiati mpana na vijimaana vya maneno mbalimbali.

Halafu akaongeza kwa kumdondoa Plato, “Poetry comes nearer to vital truth than history!” (Ushairi unakaribia zaidi ukweli kuliko historia inavyojidai! Tafsiri yangu.)

Na hapo akainuka akaelekea mezani na kuniletea faili moja kuukuu. Akaniambia: Huu muswada wangu wa JAMHURI, tafsiri ya Kiswahili ya kitabu cha THE REPUBLIC cha Plato.

Tafsiri hiyo bado haijachapishwa na faili yake imehifadhiwa katika makumbusho ya Mwalimu Nyerere huko Butiama pamoja na faili moja niliyotayarisha miye ya mashairi yaliyotungwa na Mwalimu na yaliyoingizwa katika diwani za Sheikh Mathias Mnyampala, Sheikh Abdu Kandoro na wengineo.

Kwa bahati mbaya, Mwalimu hakuwahi kuchapisha mkusanyo wa tungo zake ambazo ni za thamani kubwa kifasihi, tena ni mashairi ya vina, kama Usawa wa Binadamu na Chombo hiki hakina abiria, kila mtu apige kasia!

Mwalimu Nyerere alipata kusoma tenzi na tungo za karibu washairi wote wanaopatikana katika vitabu na majarida. Aliathiriwa pia na Zaburi zilizotungwa na Mmisheni Mchungaji William E. Taylor, Diwani ya Lambert na maandishi ya Maalim Shaaban Robert na Sheikh Mathias E. Mnyampala. Alimwita Samuel Semhoza (Mwandishi wa riwaya ya kwanza kabisa katika Kiswahili Mwaka katika minyororo, 1921) “Baba wa Riwaya ya Kiswahili, sawa na Ngugi wa Thiongo aliye Baba wa Riwaya ya Kiingereza katika Afrika Mashariki na pia sawa na Chinua Achebe aliye Baba wa Riwaya ya Kiingereza barani Afrika.”

Kuhusu kitabu kilichompa moyo wa kuanza kutafsiri fasihi na baadaye hata Injili, Mwalimu alisema ilikuwa kitabu cha Shaaban Robert Omar Khayyam Kwa Kiswahili, cha 1952 (tafsiri ya Rubaiyat of Omar Khayyam, ya Edward Fitzgerald, 1899) na Al-Inkishafi –The Soul’s Awakening ya  Sayyid Abdallah A. Nassir, tafsiri ya William Hichens, 1939. Kwa kusomea Al Inkishafi, Mwalimu Nyerere alijifunza Kiswahili na lahaja zake zote akawa, jinsi alivyojieleza “Mswahili mzawa wa mara nyingi, Mswahili wa jadi kama wewe na jamaa zako”.

Katika tafsiri za vitabu vya Shakespeare na Injili, Mwalimu anatumia lugha tamu ya kishairi na anaandika mistari ya mizani 16 au 18. Ingefaa mkusanyo wa mashairi ya Mwalimu Nyerere ukachapishwa kama Diwani ya Mwalimu Nyerere ili watu wengi wapate kufaidika na mawazo yaliyoelezwa humo na falsafa iliyofafanuliwa kitaaluma.

Mwandishi wa makala haya ni Profesa Mstaafu wa Taaluma za Kiswahili na Lughawiya ya Kibantu. Ameandika vitabu na makala kadhaa juu ya mada mbalimbali, pia juu ya historia ya Pwani ya Afrika Mashariki na mahusiano ya kihistioria na utamaduni kati ya Afrika Mashariki, Mashariki ya Kati na Bara Hindi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles