GURIAN ADOLF, SUMBAWANGA
MWALIMU wa Shule ya Msingi Kisumba wilayani Kalambo mkoani Rukwa, Lusekelo Mwakyesa (47), amefariki dunia akiwa darasani wakati akisimamia mtihani wa darasa la saba ambao umemalizika jana.
Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 9:30 alasiri katika Shule ya Msingi Mkapa katika Kijiji cha Kateka, Kata ya Matai wilayani Kalambo.
Akitoa taarifa ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando, alisema Septemba 3 majira ya asubuhi, mwalimu huyo alikwenda katika kituo chake cha kazi na kuomba ruhusa kwa mwalimu mkuu, Athuman Rashid kuwa anahisi anaumwa malaria hivyo anataka kwenda kununua dawa.
Kamanda Kyando alisema siku iliyofuata mwalimu mkuu huyo alimuuliza kama ataweza kwenda kusimamia mitihani ya darasa la saba katika kituo alichopangiwa.
Alisema Septemba 4, mwalimu huyo alifika kwenye eneo ambalo wasimamizi wa mitihani walikuwa wameelekezwa kukutana kupewa maelekezo.
“Walipokuwa hapo waliulizwa kama kuna msimamizi ambaye ana matatizo ya kiafya, lakini hakuna aliyejitokeza hivyo walipelekwa katika vituo vyao,” alisema Kyando.
Alisema Septemba 5, mwalimu Mwakyesa akiwa katika kituo chake cha kusimamia mtihani, alifanikiwa kusimamia wa asubuhi na baadaye wanafunzi kutoka kwa mapumziko.
“Wanafunzi waliporudi kwa ajili ya kufanya mtihani wa jioni, mwalimu huyo alitoa maelekezo yote na kugawa karatasi za mitihani pamoja na za kujibia na alipomaliza alikwenda kukaa katika kiti alichoandaliwa.
“Baada ya kukaa aliinama kama amejilaza katika meza iliyokuwa mbele yake kwa muda mrefu bila kuinua kichwa, ndiyo mmoja wa wanafunzi aliyefahamika kwa jina la Joel Mwajungwa, aliona maji yakitiririka kutokea miguuni kwa msimamizi huyo kitendo kilichomshtua na kutoka nje kumwita mgambo aliyekuwa akilinda usalama katika maeneo ya shule.
“Baada ya mgambo huyo kuingia darasani na kumtingisha msimamizi huyo, hakuweza kuamka na alipoangalia yale maji alibaini kuwa ni haja ndogo, akatoa taarifa kwa msimamizi mkuu aliyefika na gari na kumpeleka katika Kituo cha Afya cha Matai kwa ajili ya matibabu,” alisema.
Kyando alisema walipofika kituo cha afya walipokewa na mganga wa zamu, Chapanga Chapanga, ambaye alimfanyia uchunguzi na kubaini kuwa alikwisha fariki dunia.
Alisema kuwa walipokagua katika begi lake walikuta kuna dawa aina tano ambazo ni Aluu, Panadol, Piriton NTZ na Tsonizide na kwamba inasadikika mwalimu huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.