24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

DIWANI ATHUMANI AWA BOSI WA SABA TAKUKURU



Na NORA DAMIAN,DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola na nafasi yake kuchukuliwa na Kamishna wa Polisi, Diwani Athumani ambaye sasa anakuwa mkurugenzi wa saba wa taasisi hiyo.

Kabla ya uteuzi huo, Kamishna Athumani alikuwa Katibu Tawala Mkoa wa Kagera na sasa Mlowola ameteuliwa kuwa Balozi.

Athumani aliteuliwa kuwa Katibu Tawala Novemba 18, 2016 na kabla ya hapo alikuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Mara kadhaa Rais Magufuli amekaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa Takukuru ndicho chombo pekee cha kuifanya nchi ifike kwenye maendeleo.

Hata hivyo, Aprili 11, 2017 wakati akipokea ripoti ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa mwaka 2015/2016, Rais Magufuli alikaririwa akisema anashangazwa kuona idadi ya watu wanaokamatwa wakiwa na ushahidi wa kula rushwa ni kubwa, lakini ni wachache wanaotiwa hatiani.

“Rushwa ni kansa na nchi nyingi zimeshindwa kundelea kwa sababu ya rushwa, tukiiendeleza tutakwama. Lakini nitoe wito kwenu sijaona sana watu wanaofungwa, inawezekana ni kwa sababu ya sheria, lakini inawezekana pia katika kitengo cha ‘prosecution’ labda tuko ‘weak’.

“Mtu anashikwa na ushahidi akishaenda mahakamani ule ushahidi haupelekwi au unafichwa kwa makusudi, au yule anayeongoza anaamua kutousema halafu baadaye aliyeshikwa na rushwa anakuwa huru,” alisema Rais Magufuli.

Aidha Agosti 28, 2017 alitembelea taasisi hiyo na kufanya mazungumzo na wafanyakazi na kutaka walarushwa wengi wafungwe.

“Wakifungwa hapatakuwa na rushwa kwa sababu ndio wamekuwa walimu wa walarushwa. Kasimamieni hilo na msimwogope mtu yeyote, anayehusika na rushwa ni adui wangu na adui wa Watanzania wote,” alisema.

Aliitaka Takukuru isiwe na kigugumizi kwa kitu chenye ushahidi huku akiwataka wasije kuwa sehemu ya kuficha masuala ambayo yako wazi.

“Sitaki niwe mnafiki, nataka niwaeleze ukweli, changamoto zipo lakini je mnazishughulikia vizuri katika masuala muhimu?

“Chombo hiki ni kikubwa mno na duniani chombo ambacho kinapambana na rushwa kinaogopwa na kila mmoja, kinatakiwa kiwe ‘operated’ na watu muhimu ilimradi msionee watu,” alisema Rais Magufuli.

Mlowola aliteuliwa Desemba 4, 2015 kukaimu nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Dk. Edward Hosea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles