26.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Muziki wa dansi unamuenzi vipi Mwalimu Nyerere?

king_kikii

NA VALERY KIYUNGU

IKIWA Tanzania inaadhimisha miaka 17 toka Rais wa Kwanza, Julius Kambarage Nyerere afariki dunia mwaka 1999, huku kwenye muziki wa dansi, hasa kwenye safu hii ya Old Skul tunapata wasaa wa kumtazama Baba huyo wa Taifa kwenye suala la kuuendeleza muziki huo.

Enzi za uhai wake, hayati Baba wa Taifa alikuwa chachu ya ukuaji wa muziki wa dansi, kwani alihamasisha na kuwezesha wilaya karibu zote Tanzania kuwa na bendi ya muziki, hali kadhalika aliagiza kuanzisha bendi kwenye viwanda na mashirika ya umma.

Kufuatia agizo hilo, ziliibuka bendi nyingi zilizokuwa na wanamuziki mahiri, bendi hizo zilizopata kuvuma zilipewa majina kutokana na mahali ambapo zilitokea, mfano mzuri ni Kilombero Jazz, Kilosa Jazz, Kilwa Jazz pamoja na Butiama, ambayo ilipewa jina hilo kwa heshima ya kijiji alichozaliwa Julius Nyerere, ingawa ilikuwa na makazi yake Ifakara, mkoani Morogoro.

Baada ya kuanzishwa kwa bendi za wilaya ambazo zilifanya kazi nzuri, wanamuziki wakongwe na mahiri wa bendi hizo kila mmoja kwa uwezo wake alifanya kile alichoweza, kama kutunga, kupiga vyombo au kutunga nyimbo.

Maudhui yaliyokuwa yanazibeba nyimbo zilizotungwa na bendi hizo yalilenga zaidi kuwasifu wanasiasa na kuongeza hamasa kwa zile nchi tano zilizokuwa mstari wa mbele katika kuupigania ukombozi wa bara la Afrika.

Nyimbo kama Mwenyekiti, ulioimbwa na Urafiki Jazz, uliotungwa na Juma Mrisho, Nyerere Baba wa Taifa ulioimbwa na waimbaji wa DDC Mlimani Park ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’,  utunzi wake Joseph Mulenga pamoja na ule uitwao Mwalimu Nyerere ulioimbwa na bendi ya National Panasonic Sound uliotungwa na Maurus Mzelu mwaka 1982, nyimbo zote hizo zililenga kusifia mambo mbalimbali aliyoyafanya Nyerere.

Lakini licha ya uhusiano mkubwa wa Mwalimu Nyerere na muziki wa dansi, alipofariki hakuna bendi wala wanamuziki wakongwe waliomkumbuka kwa kutunga nyimbo za kumuenzi ambapo siku kama ya jana zingeweza kuchezwa.

TATIZO NI NINI?

Baadhi ya wanamuziki wakongwe waliozungumza na safu hii walidai kuwa, siku hizi gharama zimekuwa kubwa tofauti na miaka mingi ya nyuma, hivyo wangepata mfadhili wa kuwapa fedha za kurekodi jambo hilo lingewezekana.

KING KIKI AFUNGUKA

Mwanamuziki mkongwe wa bendi ya La Capital, Mzee King Kiki, ameiambia Old Skul kuwa wanamuziki inawawia vigumu kutunga nyimbo za kumbukumbu ya mtu aliyefariki kwa kuwa mtunzi anakuwa hana jambo jipya la kumsifu kwa kuwa matendo ya mlengwa yanakuwa yamekoma.

CHAMUDATA  NAO VIPI

Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (Chamudata), Juma Ubao, anasema kuwa ni gharama kubwa kutunga nyimbo za siasa na matukio ya kumbukumbu kama ya kifo cha Nyerere, hivyo wanahitaji kuwezeshwa ili wafanikiwe kumuenzi Mwalimu.

“Wanamuziki tunahitaji msaada wa kifedha kutoka kwenye Wizara yenye dhamana na muziki, tunapenda kuwatungia nyimbo za kumbukumbu viongozi wetu, kinachotushinda ni gharama, ni kubwa mno,” alisema Juma.

Maoni yako yaweke hapa 0714288656

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles