22 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

MCHIMBA SHIMO HUINGIA MWENYEWE 45

hadithi

ILIPOISHIA

Walipoondoka kwa mganga huyo, mke wa Waziri Mkuu na ndugu zake walirudi nyumbani ambapo waliwatuma watu kwenda kuwanunulia wanyama waliohitajika.

Wanyama hao walinunuliwa na kupelekwa kwa mganga. Kuku alipatikana pale pale nyumbani.

SASA ENDELEA

WALIPOKWENDA tena kwa mganga, mke wa Waziri Mkuu alimpelekea Sofia nguo za kubadili, ikiwemo taulo, shuka ya kitandani na ya kujifUnika, sabuni, mswaki na dawa ya meno.

Mmoja wa wasichana ambao walikuwa walinzi wa Sofia alipelekwa kwa mganga ili akakae na Sofia hadi uganga wake utakapokwisha.

Mke wa Waziri Mkuu alimpa mganga huyo nusu ya fedha zilizotakiwa kabla ya kuondoka na wenzake.

Uganga wa Sofia ulianza usiku wa siku ile ambapo mganga aliita mizimu yake na kuifanyia karamu kwa kutumia mbuzi mmoja kati ya wale wawili aliowahitaji.

Aliyatambulisha matatizo ya Sofia na kuitaka mizimu iondoe matatizo aliyokuwa nayo Sofia.

Baada ya shughuli hiyo, Sofia na mlinzi wake walitakiwa waende wakalale. Walilala ukumbini, kila mmoja sehemu yake. Hakukuwa na tatizo la mbu, kwani kila mmoja alifungiwa chandarua.

Baadaye mganga alitandika sehemu yake pale pale ukumbini, akaweka chandarua na kulala.

Kwa vile walikuwa katika mazingira ambayo hawakuyazoea, Sofia na mwenzake walichelewa sana kupata usingizi.

Hatimaye mlinzi wa Sofia alilala. Akiwa katika usingizi aliota ndoto za majini. Aliota majini wa mganga huyo wamemzunguka Sofia wakimuagua. Sofia alichinjiwa mbuzi akaambiwa anywe damu yake.

Mzimu wa Sofia ulikunywa damu ile ukaambiwa uache kunywa damu ya binadamu na uondoke kabisa kwenye mwili wa Sofia.

Wakati anaota, mlinzi huyo wa Sofia alisikia kitu kinakoroma. Kiliendelea kukoroma kwa nguvu hadi kikamuamsha usingizini.

Kulikuwa na kibatari kilichokuwa kinawaka pembeni mwa ukumbi. Msichana huyo aligundua kuwa mkoromo aliokuwa akiusikia ulikuwa halisi. Ulikuwa ukitokea mahali alipokuwa amelala yule mganga.

Mlinzi huyo wa sofia alipoangalia vizuri alimuona Sofia amemuinamia mganga huyo huku mkoromo huo ukiendelea kusikika.

Hakuelewa nini kilikuwa kimetokea, akajiinua na kuketi huku akiendelea kukodoa macho. Sinema kati ya Sofia na mganga ambayo ilikuwa mbele ya macho yake hakuielewa. Akaita.

“Sofia!”

Sofia hakumjibu kitu. Msichana huyo akainuka na kumfuata. Alipofika karibu alimshuhudia wazi Sofia akimfyonza damu yule mganga. Alikuwa ameondoka mahali alipokuwa amelala na kumfuata mwanamke huyo, akakitenga chandarua na kuanza kumfyonza damu.

Alikuwa amemshikilia mikono yote miwili huku midomo yake ikiwa kwenye shingo ya mwanamke huyo ambaye alikuwa akikoroma.

Wakati mlinzi wa Sofia anafika hapo sauti ya mganga huyo ilififia na kisha akaacha kabisa kukoroma. Akamuona Sofia akiinuka akiwa ameukakamua mwili wake, akaelekea mahali alipokuwa amelala.

“Sofia umefanya nini?” Msichana huyo alimuuliza Sofia ambaye hakugutuka wala hakuonekana kusikia wala kujali kama alikuwa anaulizwa kitu.

Alikwenda pale alipokuwa amelala akaingia ndani ya chandarua na kujilaza.

Msichana huyo aliyekuwa akimchunga Sofia alimtazama yule mganga na kugundua kuwa alikuwa ameshamalizika.

Akajiambia pengine alikuwa anakoroma wakati roho yake inatoka.

Moja ya majukumu aliyokuwa amepewa msichana huyo ni kumdhibiti Sofia pale anapoonesha dalili ya kutaka kumfyonza mtu damu. Jukumu hilo alilipewa tangu Sofia alipofikishwa pale kijijini.

Sasa baada ya kitendo hicho kutokea, msichana huyo alijiuliza atamwambia nini mama yake Sofia? Pia alijiuliza, kama Sofia ameshamuua mganga, nani ambaye atamuagua Sofia?

Msichana huyo alipohakikisha kwamba yule mganga alikuwa ameshakufa, alimfuata Sofia na kumkuta amelala usingizi kabisa.

Akaenda kuchukua simu yake aliyokuwa ameiweka mchagoni mwa godoro lake. Aliona akipiga simu hapo atasikiwa, akafungua mlango na kutoka nje. Ingawa kulikuwa giza, msichana huyo alipata ujasiri wa kusogea nyuma ya nyumba na kumpigia simu mama yake Sofia.

Simu iliita hadi ikakata yenyewe. Msichana huyo alijua kuwa mwanamke aliyekuwa akimpigia alikuwa amelala. Ulikuwa ni usiku mwingi. Akampigia tena.

Ile mara  ya pili simu haikuita kwa muda mrefu ikapokelewa. Sauti nzito ya mama yake Sofia ikasikika.

“Hello!”

“Mama kuna matatizo yametokea hapa?”

“Wewe nani?”

“Mimi Moza”

“Enhe niambie ni matatizo gani?”

“Mama Sofia amemfyonza damu yule mganga na kumuua!”

“Unasemaje?”

Moza alirudia kumueleza.

“Yesu wangu…hili ni balaa jingine tena!”

“Sasa tufanyeje mama?”

“Kwani ilikuwaje?”

“Mimi nilikuwa nimelala. Niliposhituka nikamuona Sofia amemng’ang’ania yule mganga. Alikuwa amemfuata mahali alikolala. Mpaka nafika pale, tayari ameshammaliza.”

“Mlilala pamoja?”

“Tulilala pamoja sote watatu”

“Kuna watu wengine walioona hilo tukio?”

“Ni mimi tu na mpaka sasa hakuna anayejua. Sofia mwenyewe ameshalala wala hajielewi.”

“Sasa sikiliza nikufundishe, wewe jifanye hujui kitu. Rudi katika sehemu yako ulale. Huyo Sofia amelala wapi?”

“Amelala kwenye godoro lake”

“Na wewe lala mahali kwako. Huyo mganga muacheni.”

“Asubuhi ataonekana ameuawa!”

“Nani atajua kama ameuawa. Nyinyi mtajifanya hamjui kitu. Watajua amekufa mwenyewe na mashetani yake.”

“Sawa.”

“Muangalie Sofia midomoni, kama ana damu uifute. Asiwe na alama yoyote ya damu.”

“Sawa.”

“Basi fanya hivyo. Sisi tutakuja asubuhi tutajifanya hatujui kitu. Tukiambiwa huyo bibi amekufa tutaondoka pamoja na nyinyi. Hao wanyama pia tutawaachia wao wafanyie matanga.”

“Sawa mama.”

Je, nini kitatokea? Usikose wiki ijayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,504FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles