Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
SIKU moja baada ya kusimamishwa kazi kwa watumishi wawili waandamizi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), hofu ya kutumbuliwa kwa maofisa zaidi imetawala hospitalini hapo.
Wakizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana kwa sharti la majina yao kuhifadhiwa, baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo walieleza kuwa hatua zinazochukuliwa sasa na uongozi wa hospitali hiyo zimetia hofu baadhi ya watumishi waliokuwa wakifanya kinyume cha taratibu.
Baadhi ya madaktari na wauguzi waliohojiwa na gazeti hili walieleza kuwa uongozi wa sasa wa hospitali hiyo hauna masihara katika kazi.
Tayari Mkurugenzi Mkuu wa MNH, Profesa Laurence Museru, amekwishawasimamisha kazi Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi, Dk. Praxeda Ongwenyo na mkuu wa kitengo cha kuhifadhi maiti, Dk. Inocent Mosha, ili kupisha uchunguzi dhidi yao.
Wakurugenzi hao wanadaiwa kushindwa kuwasimamia vizuri watumishi walio chini yao katika kitengo cha kuhifadhi maiti na tuhuma ya hivi karibuni waliyoelekezwa ni matukio yaliyotekea Aprili 9 na Juni 20, mwaka huu ya kuchanganywa kwa maiti.
“Uongozi umeamua kutuonyesha wazi kuwa hautaki mchezo katika kazi, lile ni somo kwetu, wahenga walisema ukiona mwenzako ananyolewa tia nywele zako maji,” alisema mmoja wa madaktari wa hospitali hiyo.
Daktari mwingine alisema hatua iliyochukuliwa ya kuwasimamisha kazi wakurugenzi hao wawili imemshtua na kwamba ameanza kujipanga kufanya kazi kwa bidii.
“Unajua miongoni mwetu wapo ambao walikuwa wamejisahau kiutendaji na kuona kwamba cheo ni kama mali yao, kumbe cheo ni dhamana tu, kwa kweli tunapaswa kubadilika na kufanya kazi kwa ufanisi,” alisema.
Suala la kutumbuliwa kwa wakurugenzi hao liliibua mjadala miongoni mwa wafanyakazi baada tu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja, Aminiel Aligaesha, kutoa taarifa ya kusimamishwa huku nafasi zao zikijazwa na Mkuu wa Idara ya Radiolojia Dk. Flora Lwakatare ambaye anakaimu nafasi ya Dk. Ongwenyo na Dk. Herbert Nguvumali aliyeteuliwa kukaimu nafasi ya Dk. Mosha.