NA VERONICA ROMWALDÂ – DAR ES SALAAM
SIKU chache baada ya kuzindua rasmi huduma ya upandikizaji figo kwa wagonjwa wenye uhitaji, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) sasa ipo kwenye mikakati ya kuanza kufanya upasuaji wa kupandikiza ini.
Akizungumza hospitalini hapo jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja, Aminiel Aligaesha alisema jopo la wataalamu saba wa hospitali hiyo wanaondoka kwenda   India kupata mafunzo maalum ya kufanya upasuaji huo.
Jopo hilo linajumuisha madaktari bingwa wanne wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini, wauguzi wawili wanaosimamia mifumo ya hadubini na mhandisi wa vifaa tiba anayesimamia mitambo ya darubini, alisema.
“Mafunzo haya yatachukua miezi mitatu tunatarajia wataalamu hawa watarejea nchini wiki ya kwanza ya   Machi, mwakani,” alisema.
Aligaesha alisema inatarajiwa wataalamu hao watakaporejea wataongeza ufanisi katika uchunguzi na tiba ya magonjwa ya ini kwa kutoa mawe, kuzibua mifereji ya nyongo na kongosho iliyozibwa na uvimbe.
“Tutaweza kufanya upasuaji wa ini kuondoa uvimbe mkubwa unaodhoofisha afya na kutishia maisha ya wagonjwa.
“Lengo kubwa ni kujenga uwezo wa ndani kwa muda mfupi utakaowezesha kufanyika kwa upandikizaji wa ini kwa wagonjwa wenye mahitaji hayo,” alisema.
Alisema hatua hiyo imelenga pia kutekeleza azma ya serikali kupunguza rufaa za nje ambazo serikali ilikuwa ikigharamia fedha nyingi kutibu magonjwa hayo.