27 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Muhimbili kuanza kupandikiza uloto mwishoni mwa mwaka

Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

WATAALAMU 11 kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) wamepelekwa katika Hospitali ya Apollo nchini India kwa mafunzo ya vitendo ya mwezi mmoja, ikiwa ni maandalizi ya hospitali hiyo kuanza kutoa huduma ya upandikizaji wa uloto mwishoni mwa mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba MNH, Dk. Hedwiga Swai, alisema wataalamu hao ni pamoja na madaktari bingwa wa magonjwa ya damu watatu, wataalamu wa maabara watatu na wahandisi watatu.

Wengine ni mtaalamu wa fedha atakayefanya uchambuzi wa gharama za huduma hiyo pamoja na mtaalamu wa manunuzi atakayechambua dawa na vitendanishi vinavyotumika na upatikanaji wake.

Alisema kundi jingine la wauguzi watatu, wataalamu wa saratani ya watoto watatu, mfamasia mmoja na wataalamu wengine wawili, walikwishapata mafunzo ya miezi mitatu ya jinsi ya kutoa huduma hiyo.

“Gharama zilizotumika kuwapeleka wataalamu hao katika mafunzo hayo ni Sh milioni 91 zikijumuisha gharama za mafunzo, nauli, fedha za kujikimu na gharama nyingine ambapo fedha hizo zimetolewa na MNH,” alisema Dk. Swai.

Alisema matibabu hayo kwa nje ya nchi inakadiriwa kugharimu Sh milioni 200 kwa mgonjwa mmoja anayepandikizwa uloto kutoka kwa ndugu yake na Sh milioni 150 kwa anayepandikizwa uloto wake mwenyewe.

Akizungumzia maandalizi ya miundombinu, Dk. Swai alisema Serikali imetoa Sh bilioni 6.2 ambapo kati yake Sh bilioni 3.7 zimetumika kwa maandalizi ya ununuzi wa vifaa na kuweka miundombinu ya kutolea huduma hiyo.

Aliongeza kuwa takwimu za MNH zinaonesha kuwa wagonjwa kati ya 130 na 140 huhitaji huduma hiyo kila mwaka ambapo zaidi ya theluthi mbili ya wagonjwa hupoteza maisha kwa kukosa huduma hiyo.

“Uwepo wa huduma hii utasaidia wananchi wengi kutibiwa hapa nchini, kujenga uwezo kwa wataalamu wa ndani, itapunguza mzigo kwa Serikali kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwani gharama za kupata huduma hii zitashuka kwa asilimia 50 kwa mgonjwa mmoja,” alisema.

Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Damu MNH, Dk. Stella Rwezaura, alisema huduma ya upandikizaji wa uloto hutolewa kwa kupandikiza chembechembe mama za kuzalisha damu ambazo hupatikana kwenye uloto  au zile zinazotoka kwenye kitovu cha mtoto au kondo la nyuma la mama.

Aliongeza kuwa upandikizaji huo huanza kwa kumwandaa mgonjwa ambaye chembechembe zake za damu zina tatizo kama saratani ya damu, selimundo na wale ambao mifupa yao inashindwa kuzalisha damu.

“Hii hufanyika kwa kuwapa tiba maalumu ya kuziua chembechembe zote zenye matatizo kisha kupandikiza mpya zilizopo kwenye uloto kutoka kwa ndugu yake mwenye vinasaba vinavyofanana au zilizozalishwa kutoka kwa mgonjwa mwenyewe,” alisema Dk. Stella.

Alisema kuwa tiba hiyo ndiyo pekee inayoweza kumtibu na kumponya mgonjwa mwenye matatizo hayo.

Tanzania itakuwa nchi ya kwanza kupandikiza uloto katika ukanda wa Afrika Mashariki na ya sita katika Bara la Afrika.

Kwa sasa huduma hii Afrika inatolewa Afrika Kusini, Tunisia, Misri, Comoro na Nigeria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles