Na Derick Milton
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka ameagiza ofisi ya katibu tawala mkoa kutuma wataalamu wa kilimo kuchunguza funza wanaodaiwa kuharibu mahindi na mtama mkoani humo.
Inaelezwa kuwa funza hao wamesambaa mkoa mzima huku wakiharibu mazao hayo kwa wingi katika wilaya za Busega, Itilima, Bariadi na Meatu.
Mtaka alitoa agizo hilo kwenye kikao kamati ya ushauri ya mkoa baada ya wajumbe wa kikao hicho wakiwamo wenyeviti wa halmashauri kulalamikia uharibufu unaofanywa na wadudu hao.
Wajumbe walisema wadudu hao wamesambaa mkoa mzima hasa katika wilaya za Bariadi na Itilima.
Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu, Joyce Masunga alisema alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wilayani Bariadi waliosema ekari zaidi ya 100 za mahindi zimeharibiwa na funza hao.
“Wananchi wengi baada ya mvua kuanza kunyesha wamefanya kazi kubwa ya kulima mahindi na mtama.
“Tatizo kubwa lililopo kwa sasa ni funza, wamepiga dawa mbalimbali lakini imeshindikana,” alisema
Wajumbe wengine walisema wakulima wamejaribu kila dawa lakini imeshindikana kwa vile funza hao wameongezeka na kuendelea kuaribu mazao yao.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ambaye ni mtaalamu wa kilimo, Fabian Manoza alisema dawa yoyote ya kuua wadudu itaweza kuangamiza funza hao lakini wajumbe hawakukubaliana naye.
Kwa sababu hiyo, RC aliagiza wataalamu wa kilimo kutoka ofisi ya mkoa, ofisi za wilaya zote kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti Ukiliguru kwenda katika maeneo husika kuchunguza funza hao na kutafuta dawa sahihi ya kuwaangamiza.