JOHANES RESPICHIUS-DAR ES SALAAM
WANANCHI wametakiwa kuacha kufumbia macho suala la ukatili wa jinsia na kujenga tabia ya kuripoti katika vyombo vya dola inapotokea.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam na Janeth Biseki ambaye ni mwanachama wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), wakati wa uzinduzi wa vibanda vya filamu za elimu kuhusu ukatili wa jinsia kwenye kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga unyanyasaji na ukatili wa jinsia.
Alisema matukio ya unyanyasaji na ukatili wa jinsia hususan kwa watoto na wanawake yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku kutokana na watu katika jamii kushindwa kuyaripoti katika vyombo husika ikiwa ni pamoja na madawati na asasi mbalimbali zinazohusika na utetezi ili kutafutiwa ufumbuzi.
“Katika maeneo mengi ambayo TGNP imekuwa ikipita tumekuwa tukikumbana na changamoto ya wananchi kuwa waoga wa kuripoti matukio ya ukatili wa jinsia.
“Kutokana na hali hiyo ndiyo maana TGNP tumeamua kuandaa vibanda vya filamu kama sehemu ya kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa jinsia ambako hizi video za makala zitakuwa na dhima ya kupinga ukatili kwa lengo la kuelimisha na kuibua mijadala katika jamii kuhusiana na vitendo vya ukatili,” alisema.
Aliwataka wananchi kushirikiana na mashirika na asasi za kupinga ukatili wa jinsia kwa kila mmoja kumchunga mwenzake kuhakikisha vitendo vya ukatili vinakuwa historia nchini.