23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Msiba wa Sitta wagusa wabunge

sittaBakari Kimwanga Na Gabriel Mushi -DODOMA

MSIBA wa Spika wa Bunge mstaafu Samuel Sitta, jana uliwagusa wabunge wengi hali iliyomfanya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, kulazimika kuliahirisha kutokana na hoja za wabunge.

Hatua hiyo ya Zungu ilitokana na mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Munde Tambwe (CCM).

Munde aliomba mwongozo baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu   akisema kutokana na taarifa za msiba huo Taifa limepoteza kiongozi mahiri hususan wananchi wa Mkoa wa Tabora.

“Mheshimiwa Mwenyekiki marehemu Sitta alikuwa mbunge wa muda mrefu, alikuwa Spika wa Bunge kwa muda mrefu na pia alikuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba la Historia.

“Kwa niaba ya wabunge wenzangu, naomba Bunge liahirishwe ili kupata muda wa kuomboleza na kutafakari mziba huu mzito wa kiongozi wetu,” alisema Munde huku akibubujikwa na machozi.

Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, alisema anakubaliana na hoja ya mbunge huyo kwa sababu  msiba ni mkubwa, umeligusa Taifa na Bunge lilihudumia matibabu ya marehemu.

Alisema pamoja na hayo, Bunge linaendeshwa kwa kanuni.

“Kanuni zinasema anapofariki dunia mbunge, Mheshimiwa Spika alishastaafu kuwa Mbunge naomba tuendelee hadi hapo kutakapokuwa na maelekezo mengine,”alisema Zungu.

Kwa majibu hayo wabunge hao walisimama kuomba mwongozo huku wengine wakipinga maelezo ya Zungu.

Hali hiyo ilimfanya Zungu alazimike   kuwatuliza kila wakati huku akimtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju kuwasilisha  Muswada wa Sheria wa marekebisho mbalimbali ya mwaka 2016.

Hata hivyo kabla muswada huo haujawasilishwa, Mwenyekiti Zungu, alimpa nafasi Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), ambaye alisimama na kuomba utaratibu.

Alisema kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kanuni ya 152   inasema kuwa:

“Endapo Mbunge atafariki dunia wakati Bunge likiwa katika shughuli zake, Spika ataahirisha shughuli za Bunge kwa siku hiyo kwa ajili ya kuomboleza.”

Alisema kanuni hiyo iliwekwa kwenye Kanuni za Bunge baada ya hali iliyokuwa imejitokeza kwa muda mrefu kwa wabunge kufariki dunia na Bunge kutoahirishwa.

Zitto alisema kuona hivyo, baadaye kanuni ya kuahirishwa Bunge, mbunge anapofariki dunia, iliwekwa.

“Toka nchi yetu ipate Uhuru tulikuwa na maspika kadhaa, maspika wote waliopoteza maisha wastaafu Bunge halikuwa kwenye vikao vyake, Adam Sapi, Erasto Mang’enya Bunge halikuwa kwenye session.

“Hivyo kwa vile sasa imetokea tupo kwenye vikao tunaweza kutumia nafasi hii kwa heshima ya Samuel Sitta,” alisema.

Alisema Kanuni ya 153(2) inampa mamlaka Mwenyekiti   kutengua kanuni yoyote.

Zitto alisema  Bunge pia haliendeshwi kwa kanuni peke yake bali linaendeshwa kwa desturi na kwa uamuzi wa maspika, hivyo anaweza kufanya uamuzi utakaosaidia baadaye endapo ikitokea hali kama hiyo.

“Naomba kutoa hoja Bunge liahirishe shughuli zake leo (jana) kwa ajili ya kumuenzi Spika mstaafu Samuel Sitta ambaye ameitumikia nchi kwa muda mrefu sana,”alisema Zitto.

Hata hivyo pamoja na hoja hiyo ya Zitto kuungwa mkono na wabunge wa pande zote, upinzani na chama  tawala CCM, Zungu alisisitiza uamuzi wake unabaki vile vile.

Baada ya kauli hiyo zilisikika kelele za wabunge wakitaka muongozo kwa Spika huku Zungu akimuita Katibu wa kikao aendelee na shughuli inayofuata.

“Mheshimiwa Zitto na Bulaya nasema tunakwenda kufanya shughuli za Bunge pamoja na hii…Zitto nakupa ‘last warning’(onyo la mwisho), nawaomba waheshimiwa kiti kinaongozwa na kanuni, kipindi hiki kigumu.

“… Zitto naomba utumie taratibu za kuzungumza, nikisimama mimi wewe tulia,” alisema Mwenyekiti huyo huku akijitahidi kutuliza kelele za wabunge.

Hata hivyo kelele ziliendelea huku wabunge wakigonga meza na sauti zikisikika zikisema, “hatuwezi kuendelea kuna msiba”.

Hata hivyo,  Zungu aliendelea kusisitiza kuwa anafanya kazi kwa mujibu wa kanuni na si vinginevyo.

Alisema kwa mujibu wa uzito wa suala lenyewe kamati ya uongozi wa bunge itakutana kwa dakika 15 huku  bunge likiendelea na itoe majibu baada ya muda huo.

Mwenyekiti huyo wa kikao licha ya kelele kuendelea alimuita Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju kuwasilisha muswada huo lakini kutokana na kelele Masaju alilazimika kutoendelea kusoma huku Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) akitaka kumpa taarifa mwanasheria hiyo.

Baada ya hali hiyo, Zungu alilazimika kusimamisha Bunge kwa   dakika 15  kusubiri majibu ya kikao cha Kamati ya Uongozi.

Hata hivyo baada ya kikao cha kamati hiyo,  Zungu alisema uamuzi wa kamati hiyo utaelekezwa kwenye kanuni ya tano ya Bunge.

Kanuni hiyo inasema; “Katika kutekeleza majikumu yake yaliyotajwa kwenye ibara ya 84 ya katiba ataongozwa na kanuni hizo na…kwa kuzingatia Katiba, sheria nyingine za nchi uamuzi wa maspika wa mabunge na mila na desturi yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na Bunge la Tanzania.”

Alisema, kwa sababu hiyo,  kamati hiyo imeridhia Bunge liahirishwe hadi kesho (leo) saa tatu asubuhi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles