26.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 16, 2024

Contact us: [email protected]

MSAJILI WA VYAMA LAWAMANI

Na PATRICIA KIMELEMETA -DAR ES SALAAM

UMOJA wa vyama vya siasa 14 visivyo na uwakilishi bungeni, umemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mstaafu Francis Mutungi, kuwapa rasimu ya mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa ili waweze kuipitia na kutoa maoni yao.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya msajili huyo kuwaandikia barua ya kuwataka kutoa maoni yao kuhusiana na mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa inayotarajiwa kutekelezwa kabla ya mwaka 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa umoja huo, Renatus Muabhi alisema pamoja na msajili wa vyama kuwaandikia barua hiyo, lakini hadi sasa hawajapewa rasimu hiyo, jambo ambalo linawawia vigumu kutoa maoni yao wakati kilichoandikwa ndani hawakijui.

“Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa inapaswa kutuletea rasimu ya mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa ili tuweze kuipitia na kujadili kipengele kwa kipengele kuliko kutuandikia barua bila ya kutupa rasimu, jambo ambalo linatufanya tushindwe kuwasilisha maoni yetu,” alisema Muabhi.

Alisema rasimu ni chanzo cha kutengeneza sheria bora itakayosimamia vyama vya siasa, hivyo basi inahitaji umakini ili kuhakikisha wanapata sheria bora itakayowasimamia.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Abdul Mluya, alisema vyama vyenye uwakilishi bungeni vimepewa rasimu hiyo ili waweze kuipitia, lakini vyama visivyo na uwakilishi hawajapewa, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa wametengwa.

“Msajili ametutenga…. Wenzetu wenye uwakilishi bungeni wamepewa rasimu lakini sisi tumepewa barua halafu tunaambiwa tutoe maoni yetu, tutatoa maoni gani kwenye mazingira kama hayo,msajili anapaswa kuliangalia suala hilo,” alisema.

Hata hivyo, Naibu Msajili wa Vyama Vya Siasa, Sisty Nyahoza alisema ofisi ya msajili haijatoa rasimu mpya ya mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa kwa vyama vya siasa zaidi ya rasimu ile ilitolewa mwaka 2013 wakati mchakato wa mabadiliko ya sheria hiyo ulipoanza.

“Hatujapeleka rasimu kwa chama chochote cha siasa zaidi ya kuwapa barua ya kutaka watoe maoni yao wakirejea rasimu ya mwaka 2013, ili tuweze kufanya maboresho,” alisema Nyahoza.

Alisema katika rasimu hiyo, ofisi hiyo ilichukua mapendekezo  kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwamo vyama vya siasa ili kuhakikisha kuwa, serikali inapata sheria bora itakayosimamia vyama hivyo.

Alisema hivyo basi hakukua na ubaguzi wowote wakati wa usambazaji wa barua hiyo zaidi ya kufuata matakwa ya kisheria ya kuvitambua vyama vyenye uwakilishi bungeni na vile ambavyo havina uwakilishi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles