Arodia Peter, Dodoma
Serikali imesema mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma na Liganga utachelewa kuanza kutokana na mazungumzo na mwekezaji kuchukua muda mrefu tofauti na ilivyotegemewa.
Hayo yamebainika baada ya swali la Mbunge wa Ludewa, Francis Ngalawa (CCM), ambaye alitaka kujua lini Serikali italipa fidia kwa wananchi walioachia maeneo yao kupisha mradi huo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya ameliambia Bunge leo Jumatatu Mei 6, kuwa kazi ya uthaminishaji mali kwa wananchi lilikamilika tangu Agosti mwaka 2015 lakini ulipaji fidia haukuweza kufanywa.
“Serikali ilifanya uthaminishaji mwingine Desemba mwaka jana na kubainisha malipo stahiki yanayopaswa kulipwa pindi taratibu za msingi za maandalizi zikikamilishwa na Serikali,” amesema Manyanya.