26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Shein awapa neno wafanyabiashara Z’bar

MWANDISHI WETU-ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein, amewanasihi wafanyabiashara kuwa waadilifu katika kuwafanyia wanunuzi tahafifu za bei za bidhaa na huduma nyinginezo hasa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Hayo aliyasema jana katika risala maalumu aliyoitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari katika kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani katika mwaka huu wa 1440 Hijria sawa na mwaka 2019 Miladia.

Katika risala yake hiyo, Dk. Shein aliwataka wafanyabiashara kukumbuka kwamba kwa kufanya hivyo, hawatakula hasara bali watazidi kupata fadhila mbalimbali za Mola wao mlezi zinazoambatana na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Aliwataka wafanyabiashara kuzingatia ubora wa bidhaa wanazowauzia wananchi, kwani wanapaswa wahakikishe kwamba wanawauzia bidhaa ambazo hazijapita muda wake wa matumizi.

Kwa msingi huo, Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa wanunuzi nao wanatakiwa wawe makini wanaponunua bidhaa kwani si jambo la busara kununua bidhaa iliyokwishamuda wake wa matumizi kwa kufuata urahisi wa bei kwa sababu urahisi huo ni gharama kubwa kwa afya zao.

Aidha, aliwataka wakulima waendelee na ustaarabu pamoja na utamaduni wao ule ule wa ustahamilivu na uadilifu kwa kujiepusha na tabia ya uvunaji na uuzaji wa mazao machanga.

Aliwataka wauzaji wa bidhaa mbal mbali kama vile matunda, samaki, mboga na nyenginezo waache ile tabia ya kuuza bidhaa zao maeneo ya barabarani au kuziweka chini bila hata ya kutandika kitu kilicho safi.

“Wafanyabiashara ni lazima wafahamu kwamba kufanya biashara bila ya kuzingatia taratibu zilizowekwa, kunaweza kuhatarisha usalama wa wapita njia, kuathiri ubora wa bidhaa hizo pamoja na afya za watumiaji wa bidhaa hizo.

“Lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar si kumkomoa mtu kwa sababu Serikali huwa haiwakomoi wananchi wake bali dhamira yake ni kuwalinda na kuona kwamba hawafikwi na matatizo ambayo yanaweza kuepukika na kujikinga nayo,” alisema Dk. Shein.

Rais huyo wa Zanzibar alizitaka taasisi zinazohusika zisimamie vyema shughuli za biashara masokoni na madukani ili vitendo vya ghilba kwa wananchi ambao ndio wanunuzi na watumiaji wakubwa wa bidhaa visiendelee.

Alisema Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa kuoneana huruma na kufanyiana hisani, kwa hivyo wananchi wazidishe imani na huruma ili waweze kuitekeleza ibada ya saumu bila ya bughudha na usumbufu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles