26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Moto wa Katiba waibuka upya

hebron-mwakagendaMAULI MUYENJWA-DAR ES SALAAM

JUKWAA la Katiba Tanzania (JUKATA) limemshauri Rais Dk. John Magufuli kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM)kuhusu kukamilisha mchakato wa Katiba mpya.

Vilevile, limeishauri Serikali kutekeleza ahadi yake iliyoitoa kwenye mkutano wa Kimataifa wa Universal Period Review Mechanism (UPR),Mei 2016   Geneva, Uswisi.

Katika mkutano huo  iliahidi kupitisha Katiba Mpya mapema iwezekanavyo.

Ahadi hiyo ya serikali ilitolewa wakati wa kuwasilisha hali ya haki za binadamu Tanzania chini ya mpango huo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa JUKATA, Hebron Mwakagenda, alisema katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Rais Magufuli hakuwa mgombea binafsi bali alipitia kwenye chama cha siasa  cha CCM ambacho kilikuwa na Ilani yake hivyo anapaswa kuitekeleza bila vikwazo.

Alisema kwa kuwa CCM iliwaahidi wananchi ambao ndiyo waliompigia kura Rais Dk. Magufuli, litakuwa ni jambo jema kutimiza ahadi hiyo kwa faida ya Taifa.

Mratibu huyo wa JUKATA alisema katika mkutano wa Kimataifa wa UPR wa Uswisi, Serikali ya Tanzania ilipokea mapendekekezo 227 na iliahidi kutekeleza mapendekezo 130 ikiwa ni pamoja na yale yanayohusu mchakato wa Katiba.  

“Kwa kuanzia,Ibara 145 inayozungumzia   kuendeleza utawala bora, demokrasia na uwajibikaji katika kipindi cha miaka mitano ijayo (2015 – 2020), CCM imeahidi kuwa itahakikisha serikali inatekeleza mambo kadhaa ikiwamo kwenye kifungu cha (g) kukamilisha mchakato wa kutunga Katiba mpya na kuanza kuitekeleza kwa mujibu wa Sheria ya mabadiliko ya Katiba.

“Katika mapendekezo hayo ya kimataifa serikali ya Tanzania ilikubali kufikiria kupitisha Katiba mpya mapema iwezekanavyo, kuitisha kura ya maoni ya Katiba, kuendeleza mchakato wa Katiba mpya ambao ni lazima uwe shirikishi na wenye kupata ushauri kutoka asasi za raia,”alisema Mwakagenda.

Alisema   ni vema Rais Dk. Magufuli atekeleze ahadi hiyo  kuendelea kulinda heshima ya Taifa katika ngazi za kimataifa.

Itakuwa ni fedheha kwa Serikali kushindwa ama kuacha kutekeleza ahadi ilizozitoa yenyewe, alisema.

Katika ushauri huo, Mwakagenda alisema   Katiba mpya pekee ndiyo itamsaidia Rais Magufuli kuinyoosha nchi na kuirudisha kwenye mstari kama ambavyo amekuwa akizungumza mara kwa mara.

Alisema    katiba hiyo pia itamfanya aache kumbukumbu ya kudumu katika mioyo ya watanzania baada ya kumaliza utawala wake.

“Kama   alivyoahidi wakati akipokea taarifa ya Uchaguzi Mkuu 2015, Alhamisi Juni 23 mwaka huu   alipoahidi kukamilisha sehemu ya mchakato wa Katiba iliyobaki,”alisema.

Wakati huo huo, JUKATA   ilizindua kitabu cha mwongozo unaoitwa ‘Mwelekeo wa Katiba mpya Tanzania, tulikotoka, tulipo na tuendako’ kikiwa na lengo la kuelimisha wananchi na watunga sera kuanza rasmi mchakato wa Katiba mpya bila kuchelewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles