30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Marekani bado hakujatulia

GOP 2016 DebateWASHINGTON, Marekani

WIKI mbili zikiwa zimepita tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Marekani na mshindi kutangazwa,   matokeo yanaendelea kutoka yakionyesha mgombea aliyeshindwa urais, Hillary Clinton akizidi kupata kura nyingi za jumla (Popular Vote) kuliko Rais Mteule, Donald Trump.

Hilo linakwenda sambamba na kampeni kali nchi nzima kujaribu kuwashawishi wajumbe wa Baraza la Uamuzi (Electoral College) kufanya kitu ambacho hakijawahi kutokea katika historia ya Marekani — kumnyang’anya urais mshindi aliyepatikana Siku ya Uchaguzi Mkuu.

Kwa mujibu wa takwimu mpya ambazo Shirika la Habari la Associated Press (AP) ilizipata juzi, Clinton hivi sasa anamzidi mpinzani wake kutoka Chama cha Republican, bilionea  Trump kwa zaidi ya kura za jumla milioni 1.5.

Kufikia siku hiyo, Clinton alikuwa amepata kura 63,390,669 sawa na asilimia 48 huku Trump akijikusanyia kura 61,820,845 sawa na asilimia 47, ikiwa ni tofauti ya kura1,569,824, kwa mujibu wa AP.

Wakati taarifa hizo za faraja kwa kambi ya Clinton zikitokea, wafuasi wake wanaendesha kampeni za kujaribu kufanya ‘mapinduzi’, wakiwataka wajumbe wa Baraza la Uamuzi (Electoral College) kumpigia kura mgombea wao kutoka Chama cha Democrat badala ya mshindi wa kura hizo za uamuzi, Trump.

Wajumbe 538 wa Baraza la Uamuzi kutoka vyama hivyo vikuu watakutana majimboni mwao Desemba 19 kumthibitisha Rais mteule.

Wanaharakati wanasambaza ujumbe katika mitandao ya jamii wakitumaini  kuwashawishi wajumbe wa Baraza la Uamuzi kutoka Republican kumpigia kura mtu mwingine badala yaTrump na hivyo kumnyima kura 270  zinazohitajika kuwa  rais.

“Ndiyo, ni kweli ni kazi ngumu hii, lakini pia nadhani tunaishi katika nyakati ngeni,” alisema Daniel Brezenoff, ambaye alianzisha mchakato huo kujaribu kurudisha ndoto ya Hillary Clinton ya kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza taifa hilo kubwa katika uchumi na jeshi duniani.

Brezenoff amekuwa akiwataka watu waliosaini kuunga mkono suala hilo, kuwashawishi wajumbe wa Baraza la Uamuzi kwa barua pepe au simu.

Katika uchaguzi mkuu wa Novemba 8, mamia kwa mamilioni walipiga kura kumchagua rais wao pamoja na wajumbe 538 wa Baraza la Uamuzi.

Katika uchaguzi huo, wakati Clinton akiwa ameongoza kwa kura za jumla, Trump alitangazwa mshindi kutokana na chama chake kupata wajumbe 290 wa Baraza la Uamuzi dhidi ya 232 za Clinton, huku jimbo la Michigan likiwa bado halijaamua.

Wapinzani waTrump wamepata nguvu kutokana na matokeo ya kura za jumla na imani yao kwamba Trump, mfanyabiashara  bilionea na mtangazaji wa televisheni hafai kuwa amiri jeshi mkuu.

Hadi sasa mjumbe mmoja wa Baraza la Uamuzi amejitokeza hadharani kueleza kuendelea kumuunga mkonoTrump.

Mwanachama huyo wa Republican kutoka Jimbo la Texas, Art Sisneros, amesema anabakia mwaminifu kwa rais mteule ingawa Trump hakuwa chaguo lake, akisisitiza hatampigia kura Clinton kwa namna yoyote ile.

Layne Bangerterna Melinda Smyser, wajumbe  wawili kati ya wanne wa Chama cha Republican katika Jimbo la Idaho, walisema wana lundo la barua pepe, simu na ujumbe wa Facebook kutoka kwa watu wasiowafahamu wakiwasihi wafikirie upya kuhusu kura yao.

‘Sidhani mpango wao huu utafanya kazi,” Bangerter alisema.”Nina matumaini kwamba utakufa.”

Wajumbe wa Baraza la Uamuzi  wa Republican katika majimbo ya Georgia, Michigan na kwingineko wamekumbana na ushawishi huo wa kuwataka wampigie kura Clinton badala ya Trump.

Michael Banerian (22) mmoja wa wajumbe  16 wa Baraza la Uamuzi wa Michigan kupitia chama hicho, ameeleza kupokea ujumbe wa kifo kutoka kwa watu wanaomtaka asimpigie kura Trump. Lakini amesema hatishiki na vitisho hivyo.

“Ni kwamba, sehemu kubwa ya watu waliokasirishwa na matokeo hayo hawajui kabisa namna mchakato huo unavyofanya kazi,” alisema Banerian.

Mjumbe wa Baraza la Uamuzi  wa Democrat, P. Bret Chiafalo kutoka Jimbo la Washington, anasema yeye na kundi dogo la wajumbe wengine kutoka chama hicho wanahaha kuwasiliana na wenzao wa Republican kuwataka kumpigia kura mgombea yeyote wa chama hicho kama vile Mitt Romney au John Kasich badala ya Trump.

Kwa mujibu wa Katiba ya Marekani, Bunge ambalo kwa sasa linadhibitiwa na Republican huamua atakayekuwa rais iwapo hakuna mgombea aliyefikia kura za Baraza la Uamuzi zinazohitajika kushinda.

Wabunge humchagua rais kutoka miongoni mwa washindani watatu wa juu.

Hiyo si mara ya kwanza kwa kura za uamuzi kukabiliwa na shinikizo za kutaka zibatilishe matokeo ya   uchaguzi.

Iliwahi kutokea mwaka 2000 wakati wa kuhesabu kura katika Jimbo  la Florida wakati mgombea urais wa Democrat aliyekuwa Makamu wa Rais, Al-Gore akiwa anaongoza dhidi ya George W. Bush.

Mgogoro uliisha baada ya Mahakama ya Juu kumpa Bush ushindi katika jimbo hilo na kumfanya aongoze kwa tofauti ndogo ya kura na hivyo kumthibitisha kuwa rais.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles