25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mo Ibrahim na kiu ya kurejesha makali VPL

NA JESSCA NANGAWE

Mohamed Ibrahim maarufu Mo Ibrahim, ni miongoni mwa nyota wa Simba aliyetolewa kwa mkopo msimu huu,akitua katika Klabu ya Namungo yenye maskani yake wilayani Ruangwa Mkoa wa Lindi.

Kutua kwa kiungo huyo ndani ya timu hiyo ngeni ambayo inashiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara, imekua chachu ya kupata matokeo mazuri kwani mpaka sasa haijapoteza mchezo wowote tangu kuanza kwa mikiki mikiki.

Mpaka sasa kiungo huyo ameisaidia timu yake hiyo kupata ushindi kwenye michezo miwli dhidi ya Singida United  ambao alipachika bao la pili na kufanikisha ushindi wa mabao 2-0.

Pia aliisaidia Namungo kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya majirani za Ndanda.

Mo Ibrahim alitua Simba akitokea Mtibwa Sugar lakini na wakati mzuri ndani ya Wekundu hao wa Msimbazi kutokana na kutopata fursa ya kucheza mara kwa mara.

Hali ilizidi kuwa ngumu , baada ya kocha wa sasa wa Simba Mbelgiji Patrick Aussems  kuchukua jukumu la kuifundisha timu hiyo kwani  mshambuliaji huyo alitumia wakati wake mwingi akiwa benchi kiasi cha kuanza kusahaulika miongoni mwa wapenzi wa soka.

Kiungo huyo amekua na mwanzo mzuri ndani ya kikosi kipya cha Namungo kilicho chini ya Mrundi Thiery Hitimana,  baada ya kuanza na ushindi mfululizo ambao umezidi kuwaweka kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

MTANZANIA lilijipa kazi ya kumsaka Mo Ibrahim na kufanikiwa kumpata ambapo lilifanya naye mahojiano.

Anafunguka mengi kuhusu maisha yake ndani ya kikosi cha Namungo.

Anaitazamaje Namungo

Mo Ibrahim anasema kutua kwake ndani ya timu hiyo ngeni kutazidi kumpa morali ya kujituma kwani mipango yake ni kuhakikisjha anaitumia vyema nafasi hiyo kurejesha makali yake dimbani ikiwemo kufunga mabao ya kutosha .

“Naamini kiwango changu ni kile kile na kama unavyojua mpira ni popote, hata ukiwa timu gani kiwango chako ndicho kitaka chokutambulisha sehemu yoyote,”anasema Mo Ibrahim.

Anakitabiria makubwa kikosi chake hicho kwa kusema anaamini ni miongoni mwa timu zitakazoonyesha ushindani wa hali ya juu msimu huu.

Anasema msingi wa yote hayo kikosi chao kuwa na wachezaji wenye ubora mkubwa pamoja na nishamu.

“Namungo imekamilika kwasababu ina watu wa kazi kweli kweli, kila mmoja wetu anatambua wajibu wake, kifupi nidhamu ndani na nje ya uwanja ni ya kiwango kikubwa,”anasema.

Kurejea simba

Mo Ibrahim anasema suala la yeye kurejea kuitumia Simba halipo mikononi mwake lakini anachoamini uwezo wake una mruhusu kuchezea timu yoyote.

“Ukiniuliza kurudi Simba sina jibu,  ila nachojua naweza kuchezea timu yoyote iwe Ligi Kuu ama hata nje ya Tanzania, kutopata nafasi Simba si kwamba uwezo wangu ni mdogo bali ni uamuzi wa mwalimu kupanga wachezaji anaona wanafaa kwa wakati huo,”anasema Mo Ibrahim.

Changamoto Simba

Mo Ibrahim anasema tofauti na timu nyingine, mchezaji anayechezea timu kubwa kama Simba au Yanga anakua na presha kubwa.

“Simba na Yanga zina mashabiki wengi ambao wakati wote wanataka matokeo mazuri tu hawajui kingine, mchezaji anayezichezea anakuwa na presha kubwa na kuzikabili unahitaji moyo mugumu vinginevyo huwezi,”anasema.

Hata hivyo, anasema alijiunga na Simba akitokea Mtibwa kwa moyo wote na alikuwa tayari kukabiliana na changamoto ikiwemo ushindani ingawa kuna kushinda na kushindwa.

“Wakati natua Simba nilijiandaa kukabiliana na lolote, najua presha ya timu hizi lakini haikunipa tabu, ni tofauti na kucheza Mtibwa au Namungo ambako unakua huru zaidi na kile unachokifanya,”anasema.

Timu anayoipa ubingwa

Kiungo huyo anasita kutabiri timu gani itatwaa ubingwa msimu huu kwa madai kwamba ni mapema kufanya hivyo, kwani kwa sasa kila moja inapambana kuwania taji hilo.

Mo anasema timu yoyote itakayojipanga sawa sawa ikiwemo Namungo ina nafasi yake ya kutwaa ubingwa.

“Ni mapema kusema nani atakua bingwa msimu huu, kila timu imejiandaa kufanya vizuri na kuleta ushindani, siwezi kusema ni Simba kwani hata Namungo tunayo wana nafasi ya kutwaa ubingwa, ni suala la muda ,”anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles