33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WAMEJILETA WENYEWE: Ndayiragije atamba Sudan hawana upenyo wa kuepuka kipigo

Na MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

TIMU ya Taifa Tanzania, ‘Taifa Stars’ leo itashuka dimbani kuumana na Sudan , katika mchezo wa kuwania tiketi kufuzu fainali za  Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi ya ndani (Chan), utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo utakuwa wa kuwania kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo,  itakayofanyika mwakani nchini Cameroon.

Stars ilitinga hatua hiyo, baada ya kuitupa nje Kenya ‘Harambee Stars’ kwa ushindi wa penalti 4-1, ikianza kulazimishwa suluhu Uwanja wa Taifa kabla ya kupata matokeo kama hayo katika mchezo wa marudiano uliochezwa Uwanja wa Nyayo, Nairobi.

Kikosi cha Stars kitajitupa dimbani kuwakabili wageni wao kikiwa kinajiamini kiasi cha kutosha, kutokana na rekodi yake ya kutopoteza michezo ya nyumbani kwa miaka ya karibuni.

 Ikumbukwe kuwa, pia Stars imefuzu hatua ya makundi ya michezo ya kuwania tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2022 nchini Qatar.

Stars ilifuzu hatua hiyo baada ya kuifurusha Burundi kwa ushindi wa mikwaju ya penalti 3-0, ikianza kuvuna sare ya bao 1-1 ugenini kabla ya kupata matokeo kama hayo nyumbani.

Stars itakuwa inasaka tiketi ya kushiriki fainali za Chan kwa mara pili , baada ya kufanya hivyo  mwaka 2009 , fainali
zilipofanyika nchini Ivory Coast, ambapo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) ilitwaa ubingwa.

Kikosi kilichoshiriki fainali hizo kilikuwa kinanolewa na kocha raia wa Brazil, Marcio Maximo.

Timu hizo zilikutana mara ya mwisho Juni 2, 2013, katika mchezo wa michuano ya Chalenji.

Katika mchezo huo uliochezwa dimba la Taifa, Stars ilitakata kwa bao 1-0 dhidi ya Sudan.


Hata hivyo, rekodi za jumla zinaonyesha timu hizo zimekutana mara 23, Stars ikishinda michezo minne, sare nane na kupoteza 11.

Akizungumzia mchezo huo, Kaimu Kocha Mkuu wa Stars, Etienne Ndayiragije alisema jana kuwa mkakati wao wa kwanza ni kupata ushindi mnono nyumbani ili kujiweka katika mazingira mazuri kuing’a Sudan.

Alisema amekifanyia maboresho kikosi chake kwenye maeneo mawili, akianza na safu ya ulinzi kwa kuifanya kuwa imara zaidi na ushambuliaji.

Ndayiragije alisema anataka washambuliaji wa timu hiyo watumie kila nafasi wanayopata kufunga bao.

“Kikosi kipo kamili kwa ajili ya mchezo, tumefanya maandalizi yetu kulingana na mchezo uliombele, tumeongeza umakini katika idara ulinzi, lakini pia tumeongeza ubunifu kwenye eneo la ushambuliaji,  kikubwa tunachokitaka ni kupata ushindi wa mabao mengi ili kupunguza presha ya mchezo wa marudiano.

“Tunaanzia nyumbani hivyo lazima tutumie vema faida hiyo, tunatikiwa kwenda ugenini tukiwa na mtaji mkubwa wa mabao, tulishindwa kufanya hivyo katika mchezo dhidi ya Kenya tukajipa mzigo mzito.

“Safari hii tunataka kuanza vizuri kwa kupata ushindi nyumbani,”alisema Ndayiragije.

Mlinda mlango wa timu hiyo, Juma Kaseja ameahidi kuwaongoza wachezaji wenzake kuvusha hatua inayofuata.

“Tunatambua Taifa linatuamini hivyo lazima na sisi turudishe fadhila ya kuaminiwa huko.

“Tunajituma kadri ya uwezo wetu ili kukate kiu ya Watanzania ambao wanatamani kuliona Taifa lao likisonga mbele, mimi kama nahodha naamini hakuna linaloshindikana,”Kaseja ambaye alipangua mikwaju ya penalti moja moja katika michezo dhidi ya Kenya na Burundi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles