27.9 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mke wa Rais anusurika kubakwa

Simone GbagboABIDJAN, IVORY COAST

MKE wa zamani wa Rais wa Ivory Coast, Simone Gbagbo juzi alikana mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu wakati wa machafuko ya kisiasa ya mwaka 2010 na alisema kuwa alinusurika majaribio kadhaa ya kubakwa akiwa gerezani.

“Nasimama mbele ya mahakama hii kwa shinikizo la Serikali na kwa madai ya uhalifu ambao sikuufanya,” alisema Simone wakati kesi yake ikiendelea kwa siku ya pili juzi.

“Ninashtakiwa kwa sababu ambazo hazijathibitishwa. Na si hilo tu, ninashtakiwa kwa kuhusika moja kwa moja na uhalifu nisioutenda,” aliongeza.

Mke huyo wa Rais wa zamani, Laurent Gbagbo, aliyejulikana kama ‘Mwanamke wa Chuma’, pia alidai kuathirika na majaribio ya kubakwa wakati yeye na mumewe walipokamatwa Aprili 11, 2011.

Pia alisema askari wa Ufaransa waliopelekwa Ivory Coast walipiga picha moja ya majaribio hayo ya kumbaka.

Simone anatuhumiwa kupanga na kuendesha ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya wafuasi wa hasimu wa mumewe katika harakati za kumbakisha madarakani kwa gharama yoyote.

Gbagbo alikataa kukubali kushindwa na wapinzani wake wakati wa uchaguzi huo wa urais mwaka 2010, hali iliyochochea machafuko baina ya pande mbili.

Kwa sasa anakabiliwa na kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) mjini The Hague, Uholanzi.

Watu zaidi ya 3,000 walikufa wakati wa machafuko ya umwagaji damu ya baada ya uchaguzi ambayo yalisababisha kukamatwa kwa wenzi hao mwaka 2011, wakati askari walipovamia handaki walimokuwa wamechukua hifadhi mjini Abidjan.

Simone amekana tuhuma za uhalifu dhidi ya wafungwa wa kivita, dhidi ya raia na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Makundi kadhaa ya haki za binadamu yanayowakilisha waathirika wa machafuko wamejitoa katika kesi, wakisema imevurugwa na kuendeshwa kiholela.

Kwa mujibu wa mwendesha mashitaka mkuu mjini Abidjan, Aly Yeo, waendesha mashtaka wamejibu tuhuma hizo wakisema kesi itaendeshwa kwa haki na uwazi na kuheshimu upande wa utetezi. Mahakamani Simone alimrushia lawama mpinzani wa mumewe, Rais wa sasa wa Ivory Coast, Allasane Ouattara kuwa chanzo cha umwagaji damu wa 2010.

“Machafuko ya baada ya uchaguzi yaliibuka kutokana na kukataa kwa Alassane Ouattara kwa msaada wa Ufaransa kuheshimu Katiba ya Ivory Coast.

“Binafsi nilipowasili kwenye Hoteli ya Golf (Makao Makuu ya Ouattara wakati huo) makalio yangu yalianikwa, niliwekwa mtupu na niliathirika kwa majaribio kadhaa ya kunibaka mchana kweupe na yote haya yalitokea mbele ya askari wa Ufaransa, ambao walikuwa wakichukua picha,” alidai.

Wakati alipokamatwa, moja ya vitu vya kukumbukwa ni pale mke huyo wa zamani wa rais alipolazimishwa kwa nguvu kuonekana pichani huku nguo zake zikiwa zimechanika mabegani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles