28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli amsukumia Zitto Ukawa  

ZittoNa Waandishi Wetu

UAMUZI wa Chama cha ACT- Wazalendo kinachoongozwa na Zitto Kabwe kutaka kuungana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kupinga kufukuzwa wabunge saba wa upinzani kutoshiriki vikao vya Bunge una kila dalili kuchochewa na misimamo ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli.

Mapema wiki hii Bunge lilitangaza kuwafungia wabunge saba kutohudhuria vikao vyake kutokana na kupatikana na makosa ya ukiukwaji wa Kanuni na kuonyesha dharau kwa Mamlaka ya Spika wakati wakidai Bunge kurushwa ‘live’.

Wabunge hao ni Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (wote Chadema) na Mbuge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo).

Wakati chama hicho kikiitisha mkutano wake na waandishi wa habari Dar es Salaam jana na kueleza nia yake hiyo kutokana na kukerwa na uamuzi uliochukuliwa na Bunge dhidi ya wabunge wa upinzani waliosimamishwa, miezi michache iliyopita si Zitto wala chama chake kilikuwa tayari kuchukua uamuzi kama huo wa kutaka kuungana na Ukawa.

Kabla ya mkutano huo, Zitto, mwenyewe aliandika ujumbe mkali katika mitandao ya kijamii akimsukumia lawama moja kwa moja Rais Magufuli kwa kuamua kuminya demokrasia.

Katika andiko lake hilo, Zitto alindika; “Rais Magufuli tunakuunga mkono kwa dhati kupambana na ufisadi. Tunakupinga kwa nguvu zote kupambana dhidi ya demokrasia.

“Kuanzia mwanzo tumekuunga mkono dhidi ya ukwepaji kodi, ubadhirifu, uvivu na uzembe. Tangu mwanzo tulionya kuwa ni lazima udhibitiwe na Bunge ili ufanye kazi kwa mujibu wa Katiba, hivi sasa wewe Rais ndio unaendesha Bunge kwa remote control. Tutakupinga kuturudisha nyuma, hutafanikiwa kamwe kubomoa misingi ya taasisi za uwajibikaji tulizoanza kuzijenga.

“Narudia nukuu muhimu sana; “Ukitaka kutawala tawala peke yako. Ukitaka kuongoza ongoza na wenzako. Rais Magufuli Tanzania inataka uongozi madhubuti na sio itawapendeza wa imla. Huko tumeishatoka na Watanzania hawatakubali kurudi huko,” aliandika Zitto.

Wakati Zitto akitoa kauli hiyo sasa na chama chake kikieleza nia ya kuungana na Ukawa, hali ilikuwa ni tofauti kabisa miezi sita iliyopita wakati Rais Magufuli alipozindua na kulihutubia Bunge la 11 ambapo wabunge wa Ukawa kabla hawajatolewa nje ya Bunge walisimama huku wakiimba kama njia ya kumzuia kiongozi huyo kulihutubia Bunge, wakipinga uchaguzi wa Zanzibar kurudiwa.

Zitto alitofautiana na msimamo huo wa Ukawa, hoja ambayo iliungwa mkono na Mshauri wa chama cha ACT- Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo, aliyesema hawawezi kushiriki mpango ambao hawakushirikishwa kuupanga.

Baada ya kuhutubia Bunge, katika hafla ya pamoja kati yake na wabunge, licha ya wabunge wa Ukawa kuisusia, lakini Zitto ambaye amepata kukaririwa akisema katika masuala fulani fulani ni lazima awe na msimamo wake alionekana akibadilishana mawazo na Rais Magufuli aliyekuwa ameongozana na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Ingawa kuna baadhi ya matukio ambayo yamepata kuwaunganisha Zitto na Ukawa katika Bunge hili la 11 lakini si kwa msimamo wa kutaka kuungana kama ambavyo wametangaza sasa hasa baada ya kuonekana kususa na chama hicho kufanya mambo kivyake baada ya Aprili 15, mwaka jana  kiongozi huyo kuonyesha nia ya kuungana na umoja huo kumkatalia.

Februari Mosi, mwaka huu baadhi ya vyombo vya habari viliandika vikihoji siri iliyopo kati ya Zitto kwa upande mmoja na Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe na Ukawa kwa upande mwingine kutokana na kuwa na msimamo unaofanana kupinga uamuzi wa Serikali kuzuia Bunge kurushwa ‘live’na hata kujiuliza kama uhusiano huo wa shaka au wa muda mfupi.

Wakati huo Zitto na Mbowe walionekana wakitabasamu pamoja wakati walipokutana na kutoa tamko juu ya tangazo la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kupitia Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC) kwa madai ya kubana matumizi ya Serikali.

Awali Zitto tangu afukuzwe Chadema na kujiunga na ACT- Wazalendo Machi 21, mwaka jana  alikuwa akitengwa na viongozi wa Ukawa na hata yeye mwenyewe amepata kukaririwa akisema umoja huo ambao uliundwa kwa nia ya kutetea Katiba hawezi kujiunga nao kwa sababu baadhi ya wajumbe wake hawautaki Muungano na wamejificha nyuma ya pazia la kutaka muundo wa Serikali tatu.

Zitto amekuwa na msimamo wa Serikali tatu lakini si wa marais watatu ambao amekuwa akidai kuwa unaweza kuvunja nchi. Msimamo wake ni rais mmoja wa Jamhuri ya Muungano, Mkuu wa Serikali ya Zanzibar na Mkuu wa Serikali ya Bara.

Hoja nyingine ambayo kwa vyovyote inaonekana kumkimbizia Zitto na chama chake Ukawa ni mgogoro ulioibuka katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Mapema wiki hii baada ya Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, kuibua hoja na kutaka suala la wanafunzi zaidi ya 7,000 waliofukuzwa UDOM lijadiliwe bungeni, Zitto naye amekuwa akionekana akitoa kauli zinazofanana na zile za wabunge wa Ukawa.

TAMKO LA ACT

Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya chama hicho Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano, Ado Shaibu, alibainisha kuwa tayari wameviandikia barua vyama vinavyounda Ukawa kuviomba vishiriki katika mapokezi yaliyopewa jina la Operesheni Linda Demokrasia.

“Chama chetu kimeviandikia barua vyama vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi kuviomba kushiriki kwenye mapokezi hayo. Tunasubiri majibu ya vyama tulivyowaalika kwa kuwaandikia barua kwa kuwa hadi sasa hawajatujibu rasmi kama watashiriki ama la zaidi ya kutufahamisha kuwa wamepokea barua zetu,” alisema Shaibu na kuongeza:

“Chama chetu kimeandaa mapokezi haya yaliyopewa jina maalumu la ‘Operesheni Linda Demokrasia’ lengo likiwa ni kuwapa nafasi mashujaa hawa waliofukuzwa bungeni kwa ajili ya kusimamia maslahi ya umma, kuelezea kilichotokea na kinachoendelea bungeni ambacho watawala hawataki kijulikane.”

Alisema kwa kutambua umuhimu wa utetezi wa maslahi ya wananchi na kuisimamia Serikali kupitia Bunge, chama chao baada ya mkutano wa Dar es Salaam utakaofanyika Juni 5, mwaka huu katika Viwanja vya Mbagala Zakhem, pia kitafanya mikutano mingine mikubwa ya hadhara katika mikoa ya Mwanza ( Juni 11, mwaka huu), Kigoma (Juni 12, mwaka huu), Mbeya ( Juni 18, mwaka huu) na Morogoro ( Juni 19, mwaka huu).”

Aliongeza kuwa pamoja na kuomba kuungwa mkono na vyama hivyo, ACT ipo tayari kuungana na Ukawa katika ziara zao kama watapewa mwaliko na operesheni hiyo ni muhimu ikapiganiwa na vyama vyote pasipo kujali itakadi zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles