24 C
Dar es Salaam
Thursday, July 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mkataba UDA wavunjwa

SIMON* Nauli mabasi mwendokasi zatajwa

Patricia Kimelemeta

HATIMAYE uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, umevunja mkataba wa uwekezaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam(UDA) na Kampuni ya Simon Group Limited inayomilikiwa na mfanyabiashara, Robert Kisena.

Mkataba huo ambao umekuwa ukipigiwa kelele ndani na nje ya Serikali, umetajwa kutokufuata taratibu za kisheria na kukiuka Sheria ya Manunuzi (PPRA).

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, jana, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita alisema uamuzi huo umefikiwa, baada ya kufanyika kikao halali cha Baraza la Madiwani.

Aidha baraza hilo la madiwani pia limeamua kwamba, asilimia 51 ya hisa zilizokuwa zinamilikiwa na kampuni hiyo zirudishwe chini ya uongozi wa jiji hilo.

Mwita alisema madiwani walipitia upya mkataba wa uwekezaji kati ya kampuni hiyo na Halmashauri ya Jiji, ambapo walibaini udhaifu katika maeneo mbalimbali wakati wa makabidhiano.

Meya huyo anayetokana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutoshirikishwa wakati wa makabidhiano.

“Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, imevunja mkataba wa makubaliano ya kuuza Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) kwa mfanyabiashara Robert Kisena, baada ya kubaini kuwapo udhaifu wakati wa kuuza shirika hili,” alisema.

Mwita alisema halmashauri ya jiji kipindi hicho, haikufuata utaratibu wa utangazaji wa zabuni wakati wa kuuza shirika hilo, hali iliyoonyesha wazi  viongozi waliokuwa madarakani wakati huo, walikuwa na maslahi binafsi katika kukabidhi shirika hilo mikononi mwa kampuni hiyo.

Alisema hadi sasa shirika hilo bado limesajiliwa kwa jina la Halmashauri ya Jiji kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), hali inayowapa nguvu ya kuvunja mkataba huo kwa sababu mmiliki wake kisheria bado ni jiji.

“Tuliambiwa Simon Group, alikuwa anakwenda benki kuchukua mikopo kwa hati ya Shirika la UDA, tumefuatilia benki mbalimbali tumebaini hakuna hata hati moja ya shirika iliyowasilishwa kwenye benki  kama dhamana ya mikopo,”alisema.

Alisema shirika hilo hadi sasa lina Sh bilioni 5.9 ambazo zililipwa na Simon Group kama malipo halali ya kuuziana shirika, jambo ambalo haliko sawa.

“Hatuwezi kuona mikataba ya kifisadi inaendelea kuimaliza Serikali, lazima tuchukue hatua ambazo ni pamoja na kuangalia taratibu za kisheria ili kuivunja,’ alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, baraza hilo limeunda timu ya watu watatu wakiongozwa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ili kuangalia athari ambazo zinaweza kujitokeza wakati wa kuvunjwa kwa mkataba huo.

 

SIMON GROUP

Akizungumzia hatua hiyo, Ofisa Habari wa Kampuni ya Simon Group, Deus Bugaywa alisema hadi sasa halmashauri ya jiji haijatoa taarifa yoyote ya kuonesha kama mkataba huo umevunjwa, licha ya magari ya UDA kuanza kazi leo.

“Hatujapewa taarifa yoyote ambayo inasema mkataba kati ya UDA na Halmashauri ya Jiji umevunjwa, tunaamini bado ni wana hisa halali tutafanya kazi kwa ubia kama ulivyo mkataba wetu,”alisema Bugaywa.

Alisema kampuni hiyo, ilifuata taratibu zote za kisheria wakati wa kuingia makubaliano, wala hakukuwa na ukiukwaji wa kisheria.

Alisema kama watakabidhiwa barua ya kuvunjika kwa mkataba huo, wataangalia taratibu za kisheria ili waweze kudai haki yao.

ILIPOTOKA

Awali, UDA ilikuwa inamilikiwa kwa pamoja kati ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Serikali Kuu, kupitia Hazina, wakiwa na  hisa ya Sh milioni 15, kila hisa moja ikiwa na thamani ya Sh 100.

Mchanganuo wa hisa za Uda, unaonyesha halmashauri ya Jiji la Dares Salaam linamiliki asilimia 51 za hisa na Hazina asilimia 49.

Mwaka 2011, Serikali ilibaini kuwepo ukiukwaji wa kisheria katika uuzaji wa shirika hilo na kampuni ya Simon Group Limited ambao umehusisha viongozi mbalimbali waliokuwa madarakani aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya UDA, Idd Simba na Meneja wake, Victor Milanzi.

Bodi ya wakurugenzi wa Uda, chini ya Simba, ilikutana na uongozi wa Simon Group ikiongozwa na Kisena na kusaini mkataba ambao ulithibitisha kwamba UDA ilikuwa imeiuzia Kampuni ya Simon Group hisa za Sh milioni 7.8 ambazo ni sawa na asilimia 52.6 ya hisa zote kwa thamani ya Sh bilioni 1.142.

Katika mkataba huo, Simon Group ingekuwa mwanahisa mkubwa katika umiliki wa UDA kwa vile Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Hazina, wangebaki na hisa milioni 7.7, ambazo ni sawa na asilimia 47.4.
Baada ya mkataba kusainiwa, kipengele cha kwanza kiliitaka Simon Group kulipa asilimia 25 ya fedha za ununuzi wa hisa za UDA ni kati ya Sh bilioni 1.142, ambazo ni sawa na kutanguliza Sh milioni 285.6.

Kwa mujibu wa mkataba huo, fedha hizo zilipaswa kulipwa ndani ya siku 14,  tangu kusainiwa mkataba huo ambapo uongozi wa Kampuni ya Simon Group Limited ulilipa fedha hizo siku  hiyo hiyo na kuufanya  utambulike kisheria.

Wakati huo huo, mradi wa mabasi ya mwendo kasi unatarajiwa kuanza leo, huku Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) ikitangaza viwango vya nauli vitakavyotumika.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA, Gilliard Ngewe alisema  abiria wote watakaotumia mabasi hayo  watasafiri bure  kwa muda wa siku mbili,  ili kupewa elimu ya matumizi ya usafiri huo.

“Tumeamua kwa nia ya dhati abiria wasafiri bure kwa siku mbili, nia yetu wapate maarifa ya namna ya kutumia mabasi haya ambayo ni mara ya kwanza kuanza kutoa huduma,” alisema.

Kuhusu viwango vya nauli za mabasi hayo, Ngewe  alisema vimepangwa kwa kuzingatia umbali wa maeneo.

Kwa njia za pembeni (feeder route), nauli itakuwa Sh 400, njia kuu (trunk route) Sh 650, huku njia kuu na pembezoni ikiwa ni Sh 800.

Alisema wanafunzi wataendelea kulipa nauli ya kawaida ya Sh 200. “Kwa njia za pembeni kuanzia Mbezi Mwisho hadi Kimara, ni Sh 400, Kimara- Kivukoni, Kimara- Kariakoo, Kimara- Morocco, Morocco- Kivukoni, Morocco- Kariakoo  na Kariakoo kwenda  Kivukoni nauli itakuwa Sh 650.

“Katika magari yatakayotumia njia mbili, Mbezi wisho kupitia Kimara hadi Kivukoni, Mbezi-Kimara Kariakoo, Mbezi Mwisho, Kimara-Morocco, nauli itakuwa Sh 800, huku nauli ya mwanafinzi ikibakia palepale,”alisema Ngewe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles