22.3 C
Dar es Salaam
Saturday, July 13, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kushtakiwa,yadaiwa bilioni 17/-

mafuruJPGNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

UMOJA wa Wakulima wa Chai Usambara Tea Growers Association (UTEGA), umetoa notisi ya siku 90 kwa Serikali kulipwa fidia ya Sh bilioni 17 .8  kwa kuwasababishia hasara baada ya kukifunga Kiwanda cha Chai cha Mponde na baadaye kutangaza kukitaifisha hivi karibuni.

Madai hayo yalibainishwa katika barua yao ya malalamiko yenye kumbukumbu namba FK/CF/UTEGA-Mponde Tea iliyowasilishwa kwa Msajiri Hazina na nakala kwenda kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kupitia notisi hiyo iliyoandikwa na Kampuni ya FK Law Chambers ya jijini Dar es Salaam, wakulima hao wanadai  kiwanda hicho kimetaifishwa na Serikali wakati ikitambua  ilikiuza kwa mikataba rasmi kupitia Tume  ya Rais ya Ubinafisishaji  Mashirika ya Umma (PSRC).

Notisi hiyo ambayo MTANZANIA ina nakala yake, Serikali kupitia Msajiri Hazina, imetakiwa kulipa fidia  ndani ya siku 90 tangu tarehe ya notisi hiyo na kwamba gharama zitaendelea kuongezeka wakati kesi ikiendelea mahakamani.

Katika notisi hiyo yenye kumbukumbu FK/UTEGA-Mponde Tea/Claims ya Mei 4, mwaka huu kusudio lao la kwenda mahakamani ni kujadili hoja mbili kubwa za kisheria.

UTEGA kupitia FK Law, wanadai kitendo alichokifanya Msajiri wa Hazina cha kutaifisha kiwanda hicho, huku akitambua wanayo hati halali ya umiliki wa ardhi ni kinyume cha kifungu cha 3(1) (b),(f) na (g) cha sheria ya ardhi sura ya 113 ya sheria za Tanzania iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 inayosomeka pamoja na vifungu 3,4,6,7,8 na 12 vya sheria ya utaifishaji Na.12 ya mwaka 1968 (iliyofanyiwa marekebisho) sura ya 118 ya sheria za Tanzania mwaka R.E. 2002 (the land Acquisition act).

Kwa msingi huo, UTEGA wanataka walipwe hasara zote zilizotokea kutokana na Serikali kutosimamia sheria za nchi hasa baada ya kuvamiwa huku ikitambua kuwa wanacheti cha uwekezaji nchini kutoka Kituo cha Uwekezaji (TIC).

Hasara hizo, ni pamoja na  mali zote zilizonunuliwa na UTEGA kutoka kwa Serikali na zile walizonunua kwa ajiri ya kuendeleza uwekezaji huo ikiwa na gharama za uendeshaji zilizotokana na kiwanda kusimamishwa kikiwa kinafanya uzalishaji.

Hasara nyingine, ni za kupunguza wafanyakazi na kuwalipa mishahara yao, posho na malipo mengine wanayostahili, gharama za kuchukua hatua za kisheria kuhusiana CHC, Serikali, wizara,mkoa na mamlaka nyingine za Serikali.

Kutokana na hasara hizo na nyingine, Mponde Tea na UTEGO na Lushoto Tea wamepata hasara ya Sh 7,824,764,219 kwa kupoteza uwekezaji kutoka benki ya NMB.

Pia wanadai wamepoteza uanachama katika shamba la chai Lushoto na wilayani Korogwe, hali iliyosababisha kupoteza soko la chai ambalo angeweza kupata Sh bilioni 10 hivyo wanaidai Serikali kulipa fidia ya kiasi hicho cha fedha.

Ingawa sababu ya Msajiri wa Hazina anasema alikitaifisha kiwanda hicho kutokana na UTEGA kushindwa kulipa deni la Sh milioni 350 lililokuwa limebaki, FK Law Chambers wanasema wateja wao walishaeleza sababu ya kutolipa deni hilo ni kunyang’anywa kwa shamba la miti la Sakare na kwamba walikuwa wakisubiri kurejeshewa shamba hilo ndipo nao walipe kwani sehemu ya fedha walizolipa kununua kiwanda inahusisha shamba hilo kama mkataba wa mauziano unavyosema.

“Kuthibitisha hilo UTEGA waliandika barua Februari 21,2011 ya kusudio la kuishtaki Serikali (initial notice of intention to sue the government) licha ya kupokelewa serikalini si Consolidated Holdings Limited (zamani PSRC) wala Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyejibu notisi hiyo,” wanasema FK Law Chambers kwa niaba ya wateja wao.

Notisi ya UTEGA kuishitaki Serikali,imenakilishwa ofisi ya Waziri Mkuu, ofisi ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara na Uwekezaji, na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo,  na Ushirika, kusudio hilo linatokana na kifungu cha sita cha mwenendo wa Serikali kama walivyofafanua katika notisi yao.

Katika kusudio hilo,kampuni hiyo inasisitiza hoja ya kwanza inahusu mkataba wa mauziano wa Desemba 7, 2007 kati ya Serikali iliyowakilishwa na Kamati ya Rais ya Kubinafsisha Mashirika ya Umma (Presidential Parastatal  Sector Reform Commission-PSRC)  na Umoja wa Wakulima wa Chai Usambara (UTEGA).

“Hoja ya pili ni barua ya kusitisha na kutaifisha mali zote za Kiwanda cha Mponde (the Letter of Termination and Repossession) iliyoandikwa Januari 22 mwaka huu na Msajiri wa Hazina dhidi ya UTEGA

“Katika hoja hii Msajiri wa Hazina na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndio walengwa wakuu katika madai haya.

“Kwenye mkataba huo wa mauziano, Serikali iliyowakilishwa na PSRC inatajwa kama muuzaji (vendor) na UTEGA wanatajwa katika mkataba huo kama wanunuzi (Purchaser) kama ilivyofafanuliwa katika kifungu cha pili cha mkataba huo.

FK Law wanadai pia kuwa katika hati ya makubaliano (MoU) ya Novemba 22,1999 kati ya PSRC na UTEGA, Serikali ilikubali kuuza mali zote za Mponde Tea Estate yakiwamo mashamba ya chai, kiwanda, majengo, shamba la miti la Sakare na nyumba za wafanyakazi zilizopo katika Kiwanja Na.2 Mpalalu Lushoto na Serikali kukabidhi hati ya Kiwanja hicho Na.5609 ambazo kabla ya kuuzwa zilikuwa chini ya Mamlaka ya Chai Tanzania (TTA).

Katika notisi hiyo, inadai baada ya mauziano hayo, UTEGA walipata mbia wao ambaye ni Lushoto Tea Company Limited, waliyeingia naye mkataba wa uwezeshaji ili kupatikana fedha za kuendesha kiwanda hicho na hati ya makubaliano kati ya UTEGA na Lushoto Tea Company Limited, ambapo UTEGA inamiliki hisa asilimia 50 na zilizobaki ni za mbia. Hati hiyo ilipelekwa kwa PSRC ambao waliridhia makubaliano ya wawili hao.

FK Law wanaeleza pia kuwa wateja wao baada ya kupata nyaraka zote za kuwahalalisha zikiwemo leseni mbalimbali walifanya uwekezaji uliofikia Sh bilioni 2.3 na walikubaliana kuanzisha kampuni ya pamoja itakayosimamia shughuli zote iliyoitwa Mponde Tea ambayo baadaye iliomba mkopo wa Sh bilioni 2 kutoka Benki ya NMB kwa ajili ya ukarabati, uboreshaji na upanuzi wa kiwanda hicho.

January 2008, notisi hiyo inaeleza kundi la watu wasiojulikana walivamia shamba la miti la Sakare lililokuwa likitumika kukata kuni za kuendeshea kiwanda, shamba ambalo liliuzwa na Serikali kwa UTEGA kama sehemu ya mali za kiwanda hicho na Serikali ikaacha kuwachukulia hatua wavamizi hao wala haikutaka kuwaondoa licha ya kujua shamba hilo lilishauzwa kwa UTEGA.

MTANZANIA lilimtafuta Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru ili kujua iwapo amepokea notisi  ya Serikali kushtakiwa mahakamani, alisema  mpaka jana alikuwa hajaipokea.

“Sijaipata hiyo hati (notisi)… waache wadai, hawanidai mimi, wanaidai Serikali si wanaamini kwamba haki itapatikana huko mahakamani…. ‘Let them do it’,” alisisitiza Mafuru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles