26 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mkapa amzungumzia Moi

Benjamin Mkapa
Benjamin Mkapa

NA BENJAMIN MKAPA

NINAFURAHI na kushukuru kwa kupata fursa hii ya kutoa salamu na pongezi zangu za dhati kwa Rais mstaafu Daniel Toroitich arap Moi wakati akitimiza umri wa miaka 90. Hakika Moi ni nembo, mtu mashuhuri na kizazi adimu cha viongozi wa Afrika.

Kwa karibu miaka minane, tulifanya kazi kwa karibu na kwa amani kama viongozi wa nchi zetu; Kenya na Tanzania, na katika muktadha wa Ukanda wa Maziwa Makuu, kukuza maendeleo na kuimarisha amani na utulivu.

Tangu mwanzo kabisa, Rais Moi alionekana akiibukia kuwa mmoja wa viongozi wakubwa wa Afrika Mashariki na rais aliyeitumikia Kenya kwa muda mrefu zaidi.

Hicho ni kielelezo cha kweli cha mtu kubahatisha kuzaliwa ili kuongoza, na hivyo kujikuta mzigo wa uongozi ukiwa mabegani mwake.

Rais mwasisi wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta, alimbaini mwalimu huyu wa shule akiwa mnyenyekevu na asiyejikuza na kumfanya kuwa makamu wake wa rais kwa miaka mingi.

Moi alionyesha umahiri wake wa uongozi wakati wa harakati za kupigania uhuru wa  Kenya na alianzisha uhusiano na viongozi wa vuguvugu za kudai uhuru Afrika Mashariki.

Wakenya wako kwenye nafasi nzuri ya kushukuru mchango wake kwa maendeleo ya taifa.

Walio nje ya taifa hilo, hata hivyo wanaona jinsi alivyofanya kazi ya kupanua mfumo wa elimu kwa ajili ya fursa sawa kwa watoto wote.

Na kwa siasa za mstari wa mbele, watakuwa wanakumbuka namna alivyokuwa na maono wakati alipoanzisha na kusimamia mfumo wa vyama vingi vya siasa na serikali.

Kwa kufanya hivyo, aliweza kuifanya Kenya ijitegemee kwa miaka 10 bila msaada wa kigeni au wa maendeleo.

Kwa upande wangu, nampigia saluti Rais Moi kwa mambo makubwa mawili ya kukumbukwa; mchango wake kwa amani na utulivu wa eneo la Maziwa Makuu na kufufuliwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Rais Moi kwa muda mrefu amekuwa mtengeneza na mjenga amani asiyechoka.

Kumbukumbu zinaonyesha namna alivyojishughulisha kikamilifu katika utafutaji wa suluhu ya migogoro katika Pembe ya Afrika, nchini Ethiopia, Uganda, Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan ya zamani na Sudan Kusini ya sasa.

Rais Moi atakumbukwa kwa juhudi zake zilizosababisha ufufuaji wa EAC, ambayo ilivunjika mwaka 1977.

EAC ya leo ni matunda ya ushawishi wake na inatoa fursa zisizo na kikomo kwa watu wa Afrika Mashariki kujenga msingi imara wa ushirikiano wa kiuchumi na utangamano.

Kaka yangu mkubwa na kiongozi mwenzangu wa zamani, anaweza kuangalia nyuma akiwa ameridhika kwa utumishi uliotukuka wa aina yake na usio na kifani kwa Kenya na Afrika.

‘Happy Birthday’ Rais Moi.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles