26.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Mjadala ubunge wa Lissu

GRACE SHITUNDU-DAR ES SALAAM  

HOJA mbili alizozitumia Spika wa Bunge, Job Ndugai kutangaza bungeni juzi jioni kumvua ubunge Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), zimezua maswali na kuibua mjadala.

Ndugai alitaja hoja hizo kuwa ni kutoonekana bungeni bila Spika kuwa na taarifa ya maandishi na kutojaza fomu ya tamko la mali na madeni.

Wakati Lissu mwenyewe akieleza kusudio lake la kwenda Mahakama Kuu ili iseme kama kweli hajulikani alipo, baadhi wamehoji kama kweli Spika naye hajui aliko.  

Andiko linalohoji kama Spika hafahamu mahali aliko Lissu liloanza kusambaa mapema jana  kwenye mitandao ya kijamii na kuzua mjadala ni lile la Askofu wa Kanisa Kiinjili la Kilutheri, Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk. Stephen Munga.

Askofu Dk. Munga aliandika; “Ndugu Spika, hivi ni kweli ya moyoni mwako kuwa ulikuwa hujui Mhe. Lissu aliko? Kama moyo hauna huruma na upendo, hata sheria nzuri zitatafsiriwa vibaya. Bwana uturehemu.”

Katika mtazamo huo huo wa Askofu Dk. Munga, mtu mmoja anayejiita Ole Mtetezi kupitia mtandao wa Twitter aliandika; “Tundu Lissu amelipwa mshahara na posho zote za kibunge tangu alipopigwa risasi hadi sasa bila kuhudhuria kikao au mkutano hata mmoja wa Bunge.

“Je, Bunge na Spika Ndugai walikuwa wanamlipa Lissu mshahara na posho za kibunge bila kufahamu alipo na kwa sababu gani hayupo? Kweli?”

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), naye aliandika; “Mh. Spika umemvua Mh Tundu Lissu Ubunge? Moyo wangu unavuja damu… Mungu nisaidie.”

Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule (Chadema), maarufu Prof. J amendika; “Tabasamu tu Kamanda Lissu, Mungu akiwa upande wako wala hakuna kitakachokushinda, hakika watashindana sana na neema za Mungu, lakini kamwe hawatashinda.”

TUME YA MAADILI

MTANZANIA Jumapili liliwasiliana na Kamishna wa Maadili katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji mstaafu Harold Nsekela kupata ufafanuzi kuhusu hoja mojawapo ya Ndugai kumvua Lissu ubunge kutokana na kutojaza fomu ya tamko la mali na madeni.

Katika hilo, Jaji Nsekela alisema suala la Lissu kuvuliwa ubunge kwa hoja hiyo si la tume yake anayoiongoza, bali ni la Spika mwenyewe aliyetangaza uamuzi huo.

Jaji Nsekela ambaye alikuwa akizungumza na gazeti hili kwa simu, hata alipotakiwa kueleza sheria inayowataka viongozi wa umma kujaza fomu za mali na madeni inaeleza vipi kwa mtu kama Lissu ambaye amekuwa nje ya nchi kwa matibabu, alimtaka mwandishi aandike barua ili aweze kumjibu na kusisitia kuwa suala hilo haliko kwake.

Alipoulizwa kwamba akiondoa suala la Lissu je sheria imekaaje kwa kiongozi yeyote ambaye amepatwa na kadhia ya kuugua kwa muda mrefu na hata kushindwa kujaza fomu za mali na maadili, alisema; “‘No comment’.”

Jaji Nsekela alipoulizwa kuwa iwapo mashauriano yamefanyika kati yake na Ndugai na hata kubani Lissu hakujaza fomu ni kwa namna gani hawezi kusema kifungu kinachoweza kutumika kumtia hatiani mtu ambaye hajajaza fomu hizo, Jaji Nsekela alisema; “Jambo hili ni ‘serious’ sana, siwezi kuzungumza juu juu na sasa hivi niko njiani natokea Arusha narudi Dar es Salaam, na hadi nisome ‘ma-book’ ya sheria.”

Alipoulizwa ni lini atakuwa amekamilisha kusoma vitabu hivyo vya sheria ili mwandishi amuone kwa ajili ya ufafanuzi alijibu; “nitarudi Dar es Salam siku yoyote.”

Juzi Ndugai wakati akitangaza kumvua ubunge Lissu, alisema wabunge wanatakiwa kujaza taarifa zenye maelezo ya mali na madeni kama katiba inavyotaka.

“Tunatakiwa tujaze fomu mbili na nakala inabaki kwa Spika, baada ya kuona kwenye kumbukumbu zangu hakuna fomu za Lissu, nilichukua jukumu la kupata uhakika wa jambo hili kwa Kamishna wa Tume ya Maadili na nilijibiwa kwa barua kwamba Lissu hajawasilisha na hawana taarifa zozote,” alisema.

Ndugai alisema kwa maana hiyo Lissu hakuwa amejaza fomu, na kwamba katika mazingira hayo kifungu cha 37 kifungu kidogo cha 3 cha Sheria ya Uchaguzi kinamtaka kumtaarifu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC) cha kufanya.

“Sababu ni mbili, kutotoa taarifa za mahali alipo na kutotoa tamko la mali na madeni kama ibara ya 71 (1g) inavyotaka.

“Napenda kuwafahamisha kuwa nimemwandikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwamba Jimbo la Singida Mashariki lipo wazi, alijaze kwa mujibu wa sheria zetu,” alisema Ndugai. 

MKURUGENZI NEC

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchuguzi (NEC), Athuman Kihamia, alipoulizwa na MTANZANIA Jumapili iwapo kuna muda wa kuitisha uchaguzi mdogo baada ya Spika Ndugai kutangaza kuwaandikia barua kumvua ubunge Lissu, alisema ni mapema kulizungumzia suala hilo ila barua ya kutoka kwa Spika itakapowafikia wataeleza kitakachofanyika.

Alipoulizwa iwapo NEC inaweza kutumia busara kupima sababu zilizotumika kumwondoa mbunge ama kiongozi yeyote wa kuchaguliwa, alisema hiyo si kazi yao.

“Sisi kazi yetu ni kuangalia kama eneo liko wazi na kuitisha uchaguzi, lakini sababu huwa zinaweza zikaletwa na Spika kwa upande wa wabunge na mahakama inaweza kuangalia,” alisema.

UAMUZI WA LISSU

Kutokana na hatua hiyo ya Spika, Lissu mwenyewe amekaririwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akisema kuwa anapanga kwenda Mahakama Kuu nchini kupinga kuvuliwa ubunge wake na iseme kama kweli hajulikani alipo.

Lissu ameiambia BBC kuwa yeye si mtoro bungeni, bali bado yupo barani Ulaya akiendelea na matibabu.

Kuhusu sababu kuu mbili alizozitaja Spika Ndugai kuwa ndizo zilizomsukuma kuiandikia NEC barua hiyo, Lissu alizipinga akisema hashangazwi na tamko lake.

“Mimi si mtoro bungeni na sijawahi kuwa mtoro, kilichonikuta kinajulikana, nilipigwa risasi 16 nikiwa natoka bungeni Septemba 7, nikaletwa nje kwa matibabu. Tangu hapo nipo nje natibiwa,” Lissu alinukuliwa na BBC.

Aliongeza kuwa; “Kwanza walionishambulia hadi  sasa hawajulikani, hakuna aliyekamatwa. Leo inasemwa sijulikani nilipo navuliwa ubunge… kinachoendelea si ajabu, kuna watu hawana maarifa tena, walichobaki nacho ni mabavu tu.

“Ni aibu kwa Spika wa Bunge kusema hajui nilipo, ilhali dunia nzima inajua nipo Ubelgiji na naendelea na matibabu. Kila siku mimi naenda hospitali kufanya tiba ya mazoezi, siwezi kutembea bila kufanya mazoezi hayo.

“Ofisi ya Bunge inajua fika nilipo. Katibu wa Bunge ameshawahi kuwasiliana kwa barua na kaka yangu kuhusu matibabu yangu na nakala ya barua iliyotumwa na katibu ilinifikia nikiwa hospitali Ubelgiji. Wanajua nilipo.”

Alisema anawasiliana na mawakili wake nchini ili wamwandikie kuomba nakala ya barua aliyotumwa NEC na pia kuiomba tume hiyo iwape nakala ya barua kutoka kwa Spika na hatua itakayofuata baada ya hapo ni kulifikisha suala hilo Mahakama Kuu.

Lissu ambaye amekuwa nje ya nchi kwa matibabu tangu Septemba 2017, katika mahojiano hayo alisema anaamini uamuzi huo wa Ndugai imekuja kwa sababu ametangaza kuwa atarejea nchini mwezi wa tisa.

“Hawa watu wana hofu juu yangu, wana hofu juu ya Septemba 7, siku nitakayorudi Tanzania. Siku ambayo itatimu miaka miwili kamili toka niliposhambuliwa, hakuna cha kunizuia kurudi,” alisisitiza.

KAULI YA KIBATALA

MTANZANIA Jumapili liliwasiliana na mmoja wa wanasheria ambao Lissu amekuwa akiwatumia mara nyingi kwenye kesi zake, Peter Kibatala ili kufahamu kama wameanza mchakato wowote wa kupeleka suala hilo mahakamani, ambapo alisema watajua kesho.

Kibatala alisema uamuzi wa Lissu kwenda mahakamani ni msimamo sahihi na ndicho kitakachotokea.

Alipoulizwa ni mawakili gani watakosimamia kesi hiyo, Kibatala alisema ni mapema kusema, kwamba hata Lissu mwenyewe alikuwa hajatulia kwani anaendelea na matibabu.

 “Tukio limetokea jana (juzi), tusubiri, tutajua Jumatatu (kesho), hatujapata muda wa kutosha wa kujadili kwa sababu leo alikuwa anatoka eneo moja kwenda jingine kwa ajili ya matibabu,” alisema.

Kibatala alisema anachokiona yeye kesi itakayofunguliwa na Lissu itakuwa na mawakili wengi na kwamba mwenyewe ndiye anayeweza kusema nani awepo.

Wakati huo huo, Chadema wamesema watatoa taarifa leo baada ya kufanya mashauriano ya kina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles