Na ASHA BANI – Dar es Salaam
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesema kutegemea misaada ya kifedha kama chanzo cha maendeleo katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) hakutasaidia kuziondolea umaskini.
Alisema badala ya kutegemea misaada hiyo, nchi za SADC zinatakiwa kutumia rasilimali za ndani kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuondoa utegemezi huo.
Hayo aliyasema jana Dar es Salaam, wakati wa kufungua mkutano wa nusu mwaka wa Mtandao wa Taasisi za Maendeleo ya Fedha wa Jumuiya ya Maendeleo (SADC-DFI).
“Mtakubaliana na mimi kwamba nchi nyingi za Afrika zina utajiri wa rasilimali, lakini bado masikini na watu wake masikini pia, njia ya kuutupa umasikini ni kujifunza jinsi ya kutumia taasisi za kifedha na matumizi sahihi ya miradi katika kuleta maendeleo chanya,’’ alisema Samia.
Alitoa pongezi kwa DFIs kwa kusapoti miradi ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na ile ya muda mfupi na mrefu lengo likiwa kusaidia ukuaji wa uchumi wa viwanda.
Alisema kaulimbiu ya mwaka huu ya “Kuelekea uchumi wa viwanda kwa maendeleo endelevu na jumuishi, wajibu wa DFIs katika SADC’’, inaendana na dhamira ya Serikali ya Tanzania katika kujikita kwenye uchumi wa viwanda, hivyo ni muda mwafaka wa kutenda.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji alisema nchi za SADC zikijipanga na kutumia mabenki yake vizuri, zinaweza kupata maendeleo ya haraka.