31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

‘RANGI ZA MAFUTA NI HATARI KWA AFYA YA BINADAMU’

Mkurugenzi wa Mazingira, kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Richard Muyungi

NA LATH MBONEA – DAR ES SALAAM

WAZALISHAJI na wasambazaji wa bidhaa za rangi za mafuta nchini, wametakiwa kuzalisha na kusambaza rangi zenye ukomo unaokubalika wa madini ya risasi ili kulinda mazingira na afya za watumiaji.

Ilielezwa kuwa kuna athari zaidi za kiafya kwa watoto, ambazo ni pamoja na kupungua uwezo wa kuelewa, kuongezeka kwa tabia za hasira, ukorofi na matatizo ya uzazi kwa wanaume.

Watoto wenye umri mdogo wanaathirika zaidi kwa vile wanaweza kushika kuta zenye rangi hizo na baadaye hupeleka mikono kinywani.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam juzi na Mkurugenzi wa Mazingira, kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Richard Muyungi, wakati akizindua ripoti ya taifa ya madini ya risasi katika rangi ya mwaka 2017.

“Ni wajibu wa wazalishaji na wasambazaji kuzalisha na kusambaza bidhaa salama zenye ukomo kukabili kiwango cha madini ya risasi, lakini swali lililopo sasa ni kwa jinsi gani mlaji atatambua kuwa rangi hiyo ni salama,” alisema.

Muyungi ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi huo ulioandaliwa na Taasisi ya AGENDA for Environment and Responsible Development (AGENDA) alisema:

“Inafahamika kuwa madini haya yana athari kwa afya za binadamu na mazingira, hasa kwa kundi la jamii lililo hatarini zaidi, yaani watoto wetu na wanawake walio kwenye umri wa kuzaa.”

Awali, Mwenyekiti wa AGENDA, Profesa Jamidu Katima, alisema utafiti wao ulihusisha aina 46 za rangi za mafuta, ambao ulionyesha asilimia 46 ya rangi hizo zilikuwa na kiwango cha madini ya risasi zaidi ya sehemu 90 ya milioni, ukilinganisha na asilimia 64 kwa utafiti wa mwaka 2015.

Alibainisha zaidi kuwa kiwango cha sehemu 90 ya milioni ndicho kilichopitishwa na wawakilishi wa nchi zaidi ya 20 za Afrika kama cha ukomo kisheria, ambacho pia hutumika katika nchi za India na Marekani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles