KUKAMILIKA kwa miradi ya ujenzi wa barabara za Mabasi ya Mwendo Kasi zenye urefu wa kilomita 138.6 ambazo zimegawanywa katika awamu sita; na barabara za juu (flyingovers) tano kama ilivyoainishwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, sasa ni dhahiri itafumua upya miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam na kuwa katika mwonekano mpya na wa kisasa zaidi.
Hatua hiyo inatokana na jiji hilo kukabiliwa na msongamano wa magari ambayo kila siku husababisha hasara ya Sh bilioni nne.
Kwa sasa awamu ya kwanza ndiyo iliyokamilika ambayo imehusisha barabara yenye urefu wa kilomita 20.9 na ujenzi wake kufadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).
Gharama za awamu ya kwanza ya ujenzi huo zilifikia Sh bilioni 403, kati yake Sh bilioni 317 zilitolewa na WB huku Serikali ikitoa Sh bilioni 63 na Sh bilioni 23.5 zililipwa kama fidia kwa wananchi walioguswa na mradi huo.
Baada ya hatua hii, awamu ya pili inatarajiwa kuwa ya ujenzi wa barabara ya kilomita 19.3 kutoka Gerezani-Kariakoo hadi Mbagala Rangi Tatu.
Awamu ya tatu itakuwa barabara yenye urefu wa kilomita 23 itakayounganisha Barabara ya Uhuru, Bibi Titi Mohamed hadi Gongolamboto.
Awamu ya nne itakuwa barabara yenye urefu wa kilomita 25 itakayoanzia Barabara ya Bibi Titi, Ali Hassan Mwinyi kuelekea Bagamoyo.
Na awamu ya tano itajumuisha barabara yenye urefu wa kilomita 22.8 itakayohusisha Barabara ya Mandela; na awamu ya mwisho itahusisha ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 27.6 kwa Barabara ya Mwai Kibaki.
Mbali na barabara za mwendo kasi, pia kuna ujenzi wa zile za juu ambapo ukiachilia mbali za Ubungo Mataa inayotajwa kufadhiliwa na WB na ile ya Tazara ambayo ujenzi wake umeanza, nyingine ni zitakazojengwa kwenye makutano ya barabara za Nyerere na Kawawa eneo la Chang’ombe Veta, Kilwa na Mandela.
Awamu ya pili itafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Kwamba awamu ya tatu, nne na tano zitafadhiliwa na WB ikiwamo usanifu wake.
Kabla ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka haujaanza jijini Dar es Salaam, wananchi walikuwa wanatumia saa mbili hadi tatu kutoka Kivukoni hadi Kimara, lakini kwa sasa watu wanatumia dakika 30.
Kwamba pia mchakato wa kupata barabara za haraka kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze unaendelea, barabara hii itakuwa na njia sita.
Tunasema hii ni hatua ya kutia moyo na kuleta maendeleo, tena ya kisasa.
Tunadhani miradi kama hii pia ifanywe kwenye miji mikubwa kama Mwanza, Arusha, Mbeya na hata makao makuu ya nchi Dodoma ili kwenda sambamba na maendeleo ya usafiri wa kisasa.
Tunasema tuanze kupanga kufanya hivyo sasa ili iwe rahisi kutekeleza miradi hii bila kujiumiza zaidi kwa kupunguza misongamano ya magari katika miji hii pamoja na kuifanya ya kisasa zaidi.