24.8 C
Dar es Salaam
Thursday, September 21, 2023

Contact us: [email protected]

MASTAA WASHIKENI MKONO WASANII WACHANGA

NA GRACE SHITUNDU, DAR ES SALAAM

KUNA semi mbalimbali za wahenga zinazosawiri jambo linalokosekana hivi sasa kwenye sanaa yetu hasa muziki na filamu.

Semi kama umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu na kidole kimoja hakivunji chawa, zinatukumbusha suala zima la ushirikiano ambapo umekosekana kabisa kwenye tasnia ya burudani.

Sanaa nchini inaonekana ni kitu rahisi na chepesi kinachofanywa na watu waliopigika kimaisha, hali ambayo ni tofauti na mataifa mengine yanayoheshimu sanaa na kuwapa hadhi ya juu wasanii wake.

Hapa nchini kuna vijana wa kike na wa kiume wenye vipaji vya kufanya sanaa ya muziki, filamu, sanaa za ufundi na zile za maonyesho, lakini hatuna chetu tunachoweza kujivunia.

Pamoja na wingi wa vipaji hivyo kwa miaka yote toka tumepata uhuru, hakuna sanaa tunayoweza kusema imetusogeza hatua kadhaa mbele ukiacha Bongo Fleva ambayo imeanza kupenya kwenye mataifa mengine hivi karibuni. Huko kwenye filamu hali bado si shwari.

Yote haya tumeyataka wenyewe kwa kuwa na mastaa wengi wasiotaka kusaidia vipaji vipya ili viongeze changamoto na hatimaye kuipaisha sanaa yetu kimataifa. Tumebaki tunawatazama wasanii wale wale waliozoeleka.

Jambo linalovunja mioyo ya wasanii wengi wachanga kwa sababu hawapati ushirikiano kutoka kwa wakubwa wao wenye uzoefu na sanaa. Nahisi woga wa kupitwa na chipukizi umetawala kwenye vichwa vya mastaa wetu.

Jambo hilo linakwamisha maendeleo ya sanaa yetu kwa sababu ili tusonge mbele ni lazima kuwe na wasanii wengi wanaochuana vikali kwenye tasnia ya muziki na filamu.

Namkumbuka Steven Kanumba alivyoweza kutumia nafasi aliyonayo kuwaonyesha njia wasanii wachanga ambao wengi wao ni wakubwa hivi sasa. Lakini hata wale walioshikwa mkono na Kanumba wamesahau kulipa fadhila.

Kwenye Bongo Fleva hivi sasa anatazamwa zaidi Diamond Platnumz kama msanii anayeibua vipaji vipya kupitia lebo yake. Si kuibua pekee bali kuwarudisha wakongwe ambao nyota zao zilianza kufifia.

Hiyo ndiyo sanaa, huo ndiyo moyo ambao natamani kila msanii maarufu awe nao ili tuweze kuwa na sanaa yenye mchanganyiko wa vipaji vikongwe na hivi vipya ambavyo vimekuwa vikibezwa pale vinapokwenda kuomba msaada wa kushikwa mkono.

Tunahitaji kina Diamond na Kanumba wengine wengi ili tasnia ya burudani ichangamke zaidi ya ilivyo sasa. Mtaani kuna vipaji lukuki lakini nafasi za kuonyesha uwezo wao hazipatikani kirahisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles