26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, September 19, 2024

Contact us: [email protected]

Milioni 105 zaondoa adha ya maji Bisarara

Na Malima Lubasha, Serengeti

Kijiji cha Bisarara kilichopo Kata ya Sedeco, Tarafa ya Rogoro wilayani Serengeti, mkoani Mara, kimeondokana na shida ya maji baada ya kupatiwa kiasi cha fedha Sh 105 milioni zilizosaidia kufikishiwa maji safi kijijini hapo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Bisarara, Thomas Marwa amesema hayo leo Agosti 23,2024 alipozungumza na Mtanzania Digital kuhusu changamoto ya maji inayowakabili wakazi wa kijiji hicho kutokana na kuamka usiku kufuata maji kwenye vidimbwi ambayo si safi na salama.

Marwa ameipongeza Hoteli ya Kitalii ya Bush Top kutoa msaada wa kuchimba kisima kirefu kijijini.

Marwa amesema kuwa msaada huo wa kuchimbiwa kisima kirefu cha maji ni mkombozi kwa akina mama ambao wamekuwa wanaamka usiku wa manane kwenda kusaka maji kwenye visima vya asili wakati mwingine wakichangia na wanyama hali iliyohatarisha maisha yao pamoja na ndoa ambapo kwa awamu hii wameweka vituo viwili vya kuchotea maji eneo la shule ya msingi na kijiji.

Amesema kuwa hoteli hiyo baada kukamilisha kuchimba kisima hicho pia wamejenga tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 7000, kujenga chumba cha kusimika mashine ya kusukuma maji kwenda kwenye tanki mradi ambao umekabidhiwa serikalini.

“ Kijiji chetu kina watu 3,210 kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2022, kina vitongoji vitano vya Chinato chenye kaya 120, Senta kaya 102, Shauri kaya 84, Korabo kaya 87 na Rogoro kaya 74, tunaomba kuongezewa vituo vingine vinne vya kuchotea maji lengo ni kusogeza huduma ya maji karibu na wananchi. Hivyo kupata huduma hiyo tunashukuru wawekezaji kwa msaada huo ambao si haba,”amesema Marwa

Hoteli ya Kitalii ya Bush Top iliyopo ndani ya Hifadhi ya Serengeti ndiyo iliyochagiza kuleta unafuu wa maisha ya upatikanaji wa maji kwenye kijiji hicho kwa kuchimba kisima kirefu na kujenga tanki la kuhifadhia maji kisha kusambaza mtandao wa maji ya bomba hatua ambayo imewezesha wananchi kuanza kupata huduma hiyo pasipo kutembea umbali mrefu kama ilivyokuwa awali.

Amesema kambi hiyo ya Bush Top imekuwa ikitoa misaada mbalimbali sekta ya elimu ambapo hivi karibuni imesaidia kukamilisha ujenzi wa matundu 10 ya vyoo na vyumba viwili vya madarasa kwa shule ya msingi Bisarara.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi baada ya mradi kukamilika baadhi ya wakazi wa kijiji hicho walisema wanauona mradi kama mkombozi aliyekuja kuwatoa kwenye changamoto ya maji iliyowakabili kwa miaka mingi.

Mmoja wa wakazi hao, Hellena Kihingu, amesema walikuwa wakilazimika kuamka saa 10.00 usiku kufuata maji ambayo nayo hayakuwa na uhakika wa kuyakuta na kuna wakati kulikuwa na foleni visima vinakauka wakati wa kiangazi, hatua iliyowapa wakati mgumu wanawake kuweza kuhudumia familia zao.

“ Tulikuwa tunatoka nyumbani saa 10.00 usiku tunawaacha wanaume wamelala,unafika kule unakuta foleni wewe uliye na ndoo mbili au tatu kunapambazuka asubuhi saa 5.00 bado unasubiria maji ndoa zetu zilikuwa mashakani kwani baadhi ya wanaume walianza kufikiri kuwa kuna zaidi ya maji,” amesema Hellena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles