23.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yatoa milioni 481 uboreshaji shule ya Sekondari Chief Sarota


Na Malima Lubasha, Serengeti

Shule mpya ya Sekondari ya Chief Sarota iliyopo katika Kata ya Nagusi Tarafa ya Grumeti Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara, imepokea Sh.481 milioni kutoka serikalini kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa miundombinu.

Miundombinu inayotarajiwa kuendelezwa ni madarasa, mabweni, nyumba za walimu na vyoo, lengo kuboresha njia za kufundishia na kujifunzia wakati itakapoanza madarasa ya kidato cha tano na sita ( A-level) mwakani.

Akizungumza katika mkutano wa wazazi na walimu wakati wa kutambulisha mradi huo, Diwani wa Kata ya Nagusi, Andew Mapinduzi amewapongeza wananchi kwa kutenga eneo la ukubwa wa hekta 15 kwa ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya shule hiyo.

Mapinduzi amesema sekondari hiyo iliyofunguliwa Januari mwaka huu yenye wanafunzi 95 kidato cha kwanza , imeanza ikiwa na vyumba nane vya madarasa, jengo la utawala, maabara, vyoo matundu 10, chumba cha tehama.

Ameeleza kuwa baada ya kupokea kiasi hicho cha fedha wataanza kujenga madarasa manne, mabweni mawili, matundu 10 ya vyoo yatakayozingatia wenye mahitaji maalum kwa wavulana na wasichana na nyumba mbili za walimu.

“ Kwa niaba ya wananchi na wazazi wa Kata ya Nagusi tunaipongeza serikali kuipandisha hadhi Sekondari hii kuwa ya A-Level kidato cha 5 na 6 kuanzia 2025,mchepuo wa masomo ya sayansi kama itaipendeza serikali tunaomba wanafunzi wa kiume na tunaipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutoa kiasi hicho cha fedha,”amesema Diwani Mapinduzi

Amesema kwa kipindi kirefu kata hiyo haikuwa na shule ya sekondari hivyo wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na kuchaguliwa walilazimika kwenda kata jirani kwa kutembea umbali mrefu, hivyo ujenzi wa shule hiyo umewapunguzia mwendo watoto wa jamii ya wafugaji.

Diwani Mapinduzi amefafanua kuwa hatua zilizochukuliwa awali kusimamia ujenzi wa miundombinu ya mwanzo kwa shilingi milioni 584, itatumika kusimamia fedha hizo nyingine za awamu ya pili kuhakikisha malengo yanatimia.

Aidha aliwatambulisha wajumbe tisa wa Bodi wa Sekondari hiyo ya Chief Sarota na kumtaja Mwenyekiti kuwa ni Masumbuko Mambasa na Makamu Mwenyekiti kuwa ni Joyce Chacha na Katibu wa Bodi hiyo ni Mkuu wa Shule Yusta Leonard ambapo alisisitiza kusimamia maendeleo ya sekondari hiyo pamoja na nidhamu kwa ujumla

Diwani Mapinduzi aliwataka wazazi na wananchi kwa jumla kuendelea kuchangia nguvu kazi pale wanapotakiwa kuboresha miundombinu na kusisitiza kuwafichua watakaobainika kudokoa vifaa vitakavyotumika katika ujenzi na wahakikishe majengo yanajengwa kwa kiwango kinachokubalika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles