30 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mifumo ya kidijitali Brela yachochea maendeleo ya viwanda, biashara

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mifumo ya kidijitali inayotumiwa na Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) imetajwa kuleta mabadiliko ya ongezeko la matumizi ya Tehama katika huduma mbalimbali zinazotolewa na wakala huo.

Kuna Mfumo wa Usajili kwa Njia ya Mtandao (ORS) ambao ni maalumu kwa ajili ya kuomba taarifa rasmi za kampuni na majina ya biashara, kupata cheti cha usajili wa kiwanda au leseni ya kiwanda, mfumo wa kielektroniki wa utoaji leseni za biashara na ule wa utoaji taarifa za taratibu za biashara za kimataifa.

Wakizungumza Aprili 23,2024 kwenye maonesho ya taasisi za Muungano yanayofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam baadhi ya wananchi waliotembelea banda la Brela wamesema maboresho yaliyofanywa hasa ya huduma za kidijitali yamepunguza urasimu na kurahisisha utoaji huduma.

Mfanyabiashara na mkazi wa Dar es Salaam, Alexandar Mhagama, amesema; “Huduma za Brela zimebadilika sana, wanaendesha huduma zao kwa kidijitali kwahiyo tukisema dijiti inafanya kazi ukienda Brela ndio utaamini. Nimepata huduma nzuri, vijana wako vizuri wanafanya kazi kwa weledi mkubwa.

“Huduma wanazotoa Brela kama inawezekana ingekuwa hivyo na kwenye taasisi nyingine, ikiwa hivi kwenye taasisi zote za Serikali tutapata maendeleo ya haraka kwa sababu vikwazo vinavyosababisha wananchi kutovutiwa kwenda kwenye huduma vitakuwa vimeondoshwa,” amesema Mhagama.

Naye Mjasiriamali Asia Hussein amewashauri wafanyabiashara na wenye makampuni kufuata sheria na taratibu kwa kuhakikisha wanasajili biashara zao.

“Watanzania ambao wana nia ya kusajili kampuni au taasisi wana wajibu wa kuja Brela si tu kupata huduma lakini pia kupata darasa,” amesema Hussein.

Ofisa Leseni Mwandamizi kutoka Brela, Rehema Kionaumela, amesema mifumo hiyo imepunguza changamoto katika utoaji huduma.

“Brela imepiga hatua kubwa na lengo ni kuwarahisishia wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar wafanye biashara zao kwa uhuru bila kupata usumbufu. Ndiyo maana Serikali iliamua kutengeneza mifumo hiyo kuwarahisishia mazingira mazuri ya kufanya biashara.

“Ninawasihi Wazanzibar na Watanzania wengine waliko sehemu mbalimbali kama wanahitaji huduma zozote waingie kwenye mfumo bila kusumbuka kuja Dar es Salaam, na kama leseni itakuwa haina tatizo lolote muhusika ataipata siku hiyo hiyo,” amesema Kionaumela.

Kwa upande wake Ofisa Usajili Brela, Ruth Mmbaga, amesema usajili wa alama za biashara na huduma na usajili wa hataza pia unafanyika kwa njia ya mtandao.

“Unapokuwa na wazo lolote la kufanya biashara na ulishabuni jina lako la biashara unatakiwa kuja kulisajili kwa sababu kuna bidhaa nyingi feki, mtu anaona bidhaa inafanya vizuri sokoni anaiga. Kwahiyo hata kama hujaanza biashara unatakiwa kuja kusajili alama yako ya kwa ajili ya kuilinda,” amesema Mmbaga.

Amesema wanaendelea kutoa elimu kupitia maonesho mbalimbali na kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo waweze kuelewa faida za kutumia miliki bunifu na kuwa na alama za biashara na huduma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles