28.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 21, 2024

Contact us: [email protected]

MIAMALA YA SIMU YAFIKIA SH TRILIONI 6 KWA MWEZI

 Na Ester Mnyika


] 

Wiki iliyopita Kaimu Meneja wa Habari wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala, alitoa takwimu za kampuni za simu za mkononi kwamba  wamefanikiwa kupitisha Sh trilioni 13.07 kupitia miamala katika kipindi cha miezi miwili.

Anasema fedha hizo zimepatikana kwa njia ya mtandao katika miezi miwili ya Novemba na Desemba mwaka jana.

Anasema katika miezi miwili iliyopita ambapo Novemba walipitisha  Sh trilioni 6.47 na Desemba Sh trilioni 6.60  huku  jumla ya mapato yote yakiwa ni Sh trilioni 13.07  kupitia kampuni za simu zinazohusika na huduma ya miamala.

Alizitaja kampuni zilizohusika na miamala hiyo kuwa ni Zantel (Easy Pesa), Tigo (Tigopesa), Vodacom (M-pesa), Airtel (Airtel Money na Halotel (Halopesa).

“Asilimia kubwa ya mzunguko wa fedha hupitia kwenye simu za mkononi, kwa sasa watu wengi wanafanya huduma kwa njia ya mtandao, kupitia simu za mkononi anaweza kutuma na kupokea pesa na kulipia huduma mbalimbali ikiwamo umeme, maji, ada za shule na zinginezo,” anasema Mwakyanjala.

Anasema kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya simu hapa nchini, ikiwa tofauti na miaka ya nyuma na kumerahisisha huduma.

Aidha, Mwakyanjala aliwatahadharisha wananchi kuwa makini kwa sababu kumekuwa na ongezeko  la utapeli na wanaoghushi utaratibu wa mawasiliano kuwalaghai watu kutuma pesa kwa njia ya simu za mkononi.

Alieleza kuwa kumekuwa kuna ujumbe mfupi wa maandishi ambao unasema  kuwa umetumiwa fedha kimakosa na kufuatiwa na kutumiwa ujumbe mfupi unaofanana na ujumbe wanaoutuma watoa huduma na hivyo kutakiwa kurudisha fedha hizo.

“Usitekeleze maagizo yoyote kutokana na ujumbe wa simu za mkononi na yanayohusu fedha kwa mawasiliano ya simu, hata kama inatoka kwenye namba ya mtu unayemfahamu, mpigie aliyekutumia ujumbe kwa namba nyingine ili kufanya uhakiki,” amesisitiza Mwakyamjala.

Aidha, amewataka wananchi kujihadhari na utapeli unaofanywa kwa kutumia simu za mkononi, huku mamlaka na vyombo vya usalama vinashughulikia suala hilo.

Kutokana  kuwa na miamala  ya Sh trilioni 13.07 kwa miezi miwili iliyopita,  MTANZANIA ilifanikiwa kuzungumza na mawakala tofauti na wateja wa huduma hiyo  kupata maoni yao na kujua kulikoni.

Rose Mwakyusa ambaye ni mkazi wa Mabibo, anasema huduma za kifedha kwa mfumo wa kidigitali nchini Tanzania imepiga hatua kubwa, ni nchi ya kwanza Afrika kwa kutuma fedha na kutoa kwa njia ya simu bila matatizo yoyote na pia kuna mfumo wa kutuma fedha benki kwa kutumia mitandao ya simu.

Anasema yeye ananufaika na huduma hiyo kutokana huduma nyingi analipia kupitia M-Pesa  akiwa mahali popote, imesaidia jamii na kutoa ajira kwa watu wengi.

“Kutokana na kuwapo kwa idadi kubwa ya watumiaji wa huduma hizo wanaotumia mitandao ya simu walau mara moja kwa mwezi, idadi hii ni kubwa na kwamba inaonyesha sekta hii inakua kwa kasi.

“Malipo ya fedha kwa njia ya simu yanasaidia kupunguza gharama hivyo kuwa kichocheo cha maendeleo, sasa hivi wafanyakazi, wakulima, wanaotumia huduma za bima, wanaonunua bidhaa hulipa kwa kutumia simu za mkononi hususan kwamba muda ndio muhimu,” anasema Mwakyusa.

Naye John Chengula ambaye ni mkazi wa Sinza, anasema huduma za kifedha kwa njia ya simu ina faida na hasara zake.

Anasema huduma hizo zimekuwa na faida kwa kuwasaidia watu kuepuka foleni wakati wa kulipia huduma na fedha zao zikiwa na usalama zaidi pale wanapohifadhi kwenye simu zao.

“Tangu kuwapo kwa huduma hizi, zimefanya watu kufanya mambo kwa urahisi zaidi wakati zamani ukitaka kutuma fedha, unatakiwa utume kwenye basi lakini sasa ukituma fedha mtu ndani ya dakika chache anazipata,” anasema Chengula.

Anasema kuwapo kwa huduma hizo kumekuwa na hasara ambayo mtu akikosea kutuma fedha kwa wakala ikaenda kwa wakala mwingine inachukua muda kurudishiwa fedha hizo mara nyingine hupati kabisa.

Kwa upande wake, wakala wa kutoa huduma za fedha kwa njia ya simu ambaye anatoa huduma Mabibo mwisho, Shaa Hassani, anasema huduma hiyo ni nzuri imempatia ajira na anaendesha familia kupitia ajira hiyo.

Anasema biashara hiyo kwa sasa imekuwa na ushindani ikiwa ni tofauti na kipindi   cha  nyuma  kwani kila eneo  kuna  wakala zaidi ya wawili.

“Mimi nina miaka sita tangu nianze biashara ya kutoa huduma za kifedha, ninahudumia familia kupitia ajira hii hivyo nashukuru kampuni za simu kwa kuanzisha huduma hii,” anasema Hassani.

Anasema katika kuhudumia watu katika huduma za kifedha, anakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na wizi wa fedha.

Hassani anasema katika ofisi zao wanahudumia watu tofauti, hivyo kuna wakati wengine ni wezi  na kuwaibia na wateja wengine hudai fedha wametoa kumbe hajatoa anatumia uongo kutaka kukuibia.

Anaiomba Serikali kuwapatia ulinzi kama ilivyo kwenye mabenki na sehemu nyingine zinazotoa huduma za fedha.

Anasema changamoto nyingine ni kampuni za simu kutopokea simu endapo kuna tatizo baina yake na mteja.

“Kwa mfano mteja amekosea kutoa fedha au kwa wakala kutuma fedha, wengi hawana uelewa jinsi ya kufanya ili aweze kupata fedha hizi, unatumia muda mwingi kupiga simu huku una wateja wengine wanahitaji huduma, naomba kampuni hizo zipokee simu kwa wakati,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles