25.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

UWEKEZAJI USAFI MAZINGIRA KUOKOA BIL 301/-

Na JUSTIN DAMIAN


]

Ofisa Mtendaji Mkuu wa UTT Micro finance, James Washima (wa kwanza kushoto), akizungumza muda mfupi baada ya kutiliana saini mradi wa usafi wa mazingira katika kata tano za Manispaa ya Temeke. Anayefuatia ni Mkurugenzi wa Water Aid Tanzania, Dk. Ibrahim Kabole na Mkurugenzi wa Asasi ya People’s Development Forum, George Ndaisaba.

TANZANIA inakadiriwa kupoteza Sh bilioni 301 kwa mwaka kutokana na ukosefu wa maji safi na salama pamoja na usafi wa mazingira. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa athari za kiuchumi zinazotokana na uchafu wa mazingira katika nchi za Afrika iliyofanywa na Benki ya Dunia.

Kiasi hiki kikubwa cha fedha kimekuwa kikipotea kwa kununua dawa na kutibu magonjwa mbalimbali yanayosababishwa na ukosefu wa maji safi na salama pamoja na yale yanayosababishwa na uchafu kama kipindupindu.

Watu wanapokuwa wagonjwa, hawawezi kuzalisha na huitaji dawa pamoja na watu wa kuwahudumia ambao nao pia wanashindwa kufanya shughuli nyingine za uzalishaji mali.

Kwa kipindi kirefu, upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na usafi wa mazingira ni mambo ambayo yamekuwa changamoto kubwa haswa kwenye makazi ya watu wenye vipato vya chini katika nchi nyingi masikini Tanzania ikiwemo.

Ukosefu wa huduma hizi muhimu unatokana na uwekezaji  usiotosheleza katika sekta ya maji na usafi wa mazingira. Jukumu la uwekezaji kwenye maeneo haya mara nyingi limekuwa likionekana kama ni la Serikali peke yake.

Kwa wale ambao wamefika sehemu kama Mbagala na haswa katika Kata ya Kibonde maji, wanaweza kukubaliana na ukweli kuwa mazingira ya eneo hilo si salama hata kidogo kwa kuishi kutokana na uchafu uliokithiri.

Ni mwendo wa takribani saa moja kutoka katikati ya mji, kama hakuna msongamano wa magari unafika katika sehemu hiyo. Kwa yule ambaye ndiye atakuwa anafika kwa mara ya kwanza, anaweza kupigwa na butwaa jinsi watu wanavyoishi lakini hayo ndiyo maisha yao ya kila siku. Kata hii inawakilisha kata nyingine nyingi zenye hali kama hii jijini Dar es Salaam.

Yapo maeneo mengine kama Tandale, Manzese, Kigogo na mengineyo ambayo uchafu umekuwa ni kama sehemu ya maisha ya kila siku ya wakazi wa maeneo hayo.

Mwanzoni mwa wiki iliyopita, mashirika yasiyo ya kiserikali  ya Water Aid People’s Development Forum (PDF) kwa kushirikiana na Manispaa ya Temeke na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (Dawasa),  yalifanya jambo kubwa na la aina yake kwa ajili ya kusaidia kata tano zilizopo katika Wilaya ya Temeke ikiwemo kata ya Kibonde Maji.

Kwa pamoja wadau hawa walitoa Sh milioni 102 kwa ajili ya kuwakopesha  wajasiriamali wanaojihusisha na usafi wa mazingira.

Fedha hizo ambazo zitatumika kununulia vifaa pamoja na kukopesha mtaji wa kufanyia kazi hiyo, zilikabidhiwa kwa mfuko wa uwekezaji wa UTT kupitia kampuni yake tanzu ya masuala ya ukopeshaji ya UTT Micro Finance. UTT itawajibika kuzikopesha na zitakuwa zikizunguka.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kutiliana saini mkataba wa utoaji wa fedha hizo, anasema mradi huo utawanufaisha watu wanaoishi kwenye mazingira ambayo ni vigumu kuzoa taka kwa kutumia magari na kunyonya maji taka katika kata tano za Wilaya ya Temeke.

“Ukifika katika sehemu za mradi unaweza kufikiri haupo  jijini Dar es Salaam. Mazingira ni machafu sana na hakuna hata sehemu ya  kuweza kukusanya taka. Mtu akitoka nyumbani kwake katika maeneo haya kwenda kwenye shughuli zake ni lazima akutane na maji machafu au kinyesi. “Maji wanayoyatumia wakazi wa maeneo haya, mimi na wewe hatuwezi kuyatumia kutokana na kupatikana katika mazingira tatanishi ambayo si salama,” anaeleza.

Mkurugenzi huyo alieleza kuwa mradi huo pia una lengo  la kuonyesha kuwa sekta ya usafi wa mazingira ni fursa ya kibiashara na hivyo taasisi za mikopo zijitokeze kukopesha sekta hii ambayo ni muhimu kwa maendeleo.

Kata ambazo zitanufaika na fedha zilizotengwa kwa ajili ya kukopesha ni Kilungule, Charambe, Kibondemaji, Kiburugwa na Charambe. Wajasiriamali wanaojishughulisha na usafi watawezeshwa kupata vifaa va mitaji kwa ajili ya uzoaji taka na unyonyaji wa maji taka.

“Watu wa maeneo haya wamekuwa wakilipa kiasi kikubwa kwa ajili ya kupata huduma kama ya maji. Wananunua ndoo ya lita 20 kwa Sh 500. Lakini baada ya kuwawekea maji safi ya DAWASCO, sasa wananunua ndoo hiyo hiyo kwa Sh  50 tu,” anafafanua.

Mkurugenzi huyo wa WaterAid, anasema uwekezaji kwenye huduma kama maji na usafi wa mazingira unalipa katika maeneo kama hayo na kuzitaka taasisi za mikopo kwenda kuwekeza.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa UTT Micro Finance, James Washima, anasema taasisi yake imefurahia kuwa sehemu ya mradi huo ambao inawalenga kuboresha hali ya usafi kwa kaya zenye kipato cha chini.

“Moja kati ya malengo yetu ni kusaidia wananchi wa chini kujikwamua kiuchumi. Usafi wa mazingira ni muhimu kwa kuwa unawaepusha wananchi  na magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na kuwafanya wawe na afya njema, hivyo kufanya shughuli za uzalishaji mali,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Ofisa mazingira wa wilaya, Pastory Alexander, alisema kata zinazonufaika na mradi huo ni kati ya kata zinazozalisha kiasi kikubwa  cha taka katika Wilaya ya Temeke.

“Mradi huu tunaamini utaleta mabadiliko makubwa katika kata hizi kwani hali ni mbaya sana. Tunaamini mradi huu utakuwa wenye mafanikio na hivyo kuwa wa mfano kwa sehemu nyingine,” anaeleza.

Pastory ameishukuru WaterAid kwa kufanikisha upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo hayo ambayo huduma hiyo muhimu ilikuwa  ni tatizo kubwa.

“Wakazi wa maeneo haya sasa wanaweza kupata maji safi na salama kwa bei nafuu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles