27.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 5, 2023

Contact us: [email protected]

FEDHA HARAMU GFI: NCHI MASIKINI HUFADHILI NCHI TAJIRI

Na Justin Damian


INAKADIRIWA kuwa takribani watu milioni 18 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na matatizo mbalimbali yanayotokana na hali ngumu ya kiuchumi katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania.

Kiasi hicho cha watu wanaopoteza maisha kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, ni wastani wa watu 50,000 kwa siku.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Desemba mwaka 2015 na asasi binafsi inayojihusisha na utafiti wa masuala ya fedha duniani yenye makao yake makuu jijini Washington Marekani inayojulikana kama Global Financial Integrity, wakati idadi hiyo ya watu ikipoteza maisha ya mabilioni ya dola ambayo yangeweza kuokoa maisha yao, yamekuwa yakitoroshwa kijanja kwenda nchi tajiri.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, nchi zinazoendelea zilipoteza Dola za Marekani trilioni 7.8 kati ya kipindi cha mwaka 2004-2013. Mbaya  zaidi ripoti hiyo inasema kuwa, tatizo hilo limekuwa likiongezeka kwa asilimia 6.5 kwa mwaka.

Profesa wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe tawi la Dar es Salaam, Prosper Ngowi, anasema tatizo la uhamishaji fedha kwa njia haramu linaikabili Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingi za Kiafrika.

Anasema tatizo hili ni kubwa kwa sababu fedha hizi zingebaki nchini au katika nchi hizi masikini zingesaidia maendeleo ya uchumi kama kujenga miundombinu kama barabara, reli, viwanja vya ndege nakadhalika. Pia zingesaidia upatikanaji wa huduma za jamii kama maji, afya, elimu nakadhalika. Vipo vifo ambavyo vingeweza kuepukika kama fedha hazingekuwa zikitoroshwa,” anafafanua Prof Ngowi.

Akizungumzia chanzo cha tatizo hilo, anasema: “Tatizo ni namna fedha hizi zinavyokuwa zimepatikana. Kama ni fedha haramu na chafu, kunakuwa na haja ya wahusika kuwa na usiri na fedha hizi. Pia kuna hoja kuwa zinatoroshwa kukwepa kodi katika nchi zinakotoka. Mfano ni fedha katika Panama papers. Ubinafsi na uroho na ulafi uliopitiliza husababisha wahusika kutorosha fedha hizi. Pia hili ni tatizo la kimaadili,”

 “Tunapozungumzia ‘Mabilioni ya Uswisi’ ndiyo mambo haya ya utoroshwaji. Pia katika Panama papers tunaambiwa wapo Watanzania kadhaa. Ni tatizo ambalo madhara yake kwa Tanzania ni makubwa kama ambavyo nimeeleza hapo mwanzoni,” anasema.

Kuhusiana na jitihada mbalimbali zinazofanyika kukabiliana na tatizo hili hapa nchini anasema: “Juhudi mbalimbali zinafanyika. Hata hivyo, ili mafanikio yaweze kupatikana katika suala hili, juhudi za kitaifa pekee hazitoshi. Hili ni tatizo la kimataifa na linahitaji juhudi za pamoja za kimataifa. Nchi ambazo ni ‘tax haven’ kwa maana ya maficho ya fedha zinazotoroshwa lazima zitoe ushirikiano.

Hili limekuwa tatizo kwa sababu nchi hizi zinafaidika kutokana na fedha hizi. Hata hivyo, kuna juhudi za kimataifa za kutaka uwazi zaidi zinaendelea. Nchi kama Uswisi imetoa ahadi ya kutoa ushirikiano zaidi ikiwemo Tanzania.”

Prof Ngowi anasema kuna haja ya kufanya mambo mengi na hasa juhudi za pamoja za kimataifa; kufanya tatizo hili lifahamike na athari zake kwa nchi ni muhimu pia.

“ Pamoja na haya, ni vizuri kujua kuwa hili ni tatizo la kimaadili vile vile. Viongozi wa dini wana nafasi kubwa sana katika kupunguza na hata kumaliza tatizo hili kwa kuwakemea na kuwafundisha waumini wao,” anaeleza.

Raymond Baker ambaye ni rais wa taasisi ya Global Financial Integrity, anasema taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwepo kwa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kimekuwa kikitoka nchi masikini kwenda nchi tajiri.

“Hii inaonesha kuwa badala ya nchi tajiri kuzisaidia nchi masikini, nchi masikini zimekuwa zikizisaidia nchi tajiri,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles