OTHMAN MIRAJI
RAIS aliyepinduliwa karibuni kutoka madarakani nchini Sudan, Omar Hassan al-Bashir, ametajwa ni mmojawapo wa watu waliochangia katika kuuliwa watu wengi hapa duniani.
Alikuwa katikati ya vita vya ukombozi wa Sudan Kusini vilivyochukua roho za watu milioni mbili na kumalizika mwaka 2005 baada ya kudumu kwa miaka 20 ya maangamizi na njaa. Vita hivyo vilikoma kwa Sudan Kusini kujitenga na kuwa nchi huru.
Baadaye yakafuata mauaji yakiholela katika Jimbo la Darfur ambapo wanamgambo waliokuwa watiifu kwa utawala wa Bashir, Janjaweed, tangu mwaka 2003 waliendesha “safishasafisha“ ya kikabila iliyochukua roho za hadi watu 300000.
Bashir amekuwa akisakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya mjini The Hague ili akajibu tuhuma za uhalifu wa kivita na ukatili dhidi ya ubinadamu huko Darfur. Kukaa kwake madarakani kwa muda wa miaka 30 kumeifanya Sudan kuwa karibu jahanamu ya dunia.
Bashir alizaliwa mwaka 1944 kaskazini ya mji mkuu wa Khartoum. Alianza kulitumikia Jeshi la Misri na mwaka 1973 alikuwa mbele kabisa katika medani ya mapigano katika Vita ya Yom-Kippur baina ya Israel na nchi za kiarabu.
Baadaye alikusanya ujuzi kama askari wa miavuli katika vita huko Sudan Kusini. Juni 30, 1989 alitwaa madaraka ya juu kabisa nchini pale jeshi pamoja na wanasiasa wenye siasa za kiislamu walipoiangusha kutoka madarakani serikali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasiaya Sadiq al-Mahdi.
Watu walioyafanya mapinduzi ya uokozi, kama walivoyaita walisema wanataka kuirejesha Sudan, nchi ya kiarabu na kiislamu katika njia iliyo sawa. Lakini walisahau kwamba Sudan ilikuwa nchi ya mchanganyiko wa makabila dini na tamaduni mahala palipokutana hasa tamaduni za kiarabu na kiafrika.
Vita vya ukombozi wa Sudan Kusini na vile vya Darfur vilivyochukua maelfu kwa maelfu ya roho za Wasudan vilikuwa na kielelezo cha tofauti hizo zilizodharauliwa, lakini pia zikatumiwa na mataifa ya nje yaliyokuwa hayaitakii mema Sudan. Mataifa hayo ya nje yalitaka Sudan, nchi kubwa kabisa katika Afrika kwa eneo, imegukemeguke. Mataifa hayo mwishowe yalifaulu.
Bashir ameshindwa. Ameipoteza Sudan Kusini iliyojipatia uhuru wake mwaka 2011 chini ya uongozi wa Jeshi la Ukombozi wa Sudan, SPLA. Bashir alipoteza kuungwa mkono na watu wenye siasa za kiislamu ndani ya nchi yake wakiongozwa na mwanachuo ni wa kutajirika, marehemu Hassan al-Turabi. Ni al-Turabi na Bashir walioongoza mapinduzi yaliyopelekea Bashir aingie madarakani.
Tangu mwaka 2009 Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya The Hague imetoa waranti wa kukamatwa Bashir, lakini baada ya miezi minne ya maandamano ya mfululizo hivi karibuni huko Sudan dhidi ya dikteta huyo, hamna yeyote kati ya washirika wake duniani aliyenyoosha kidole kutaka kumhifadhi.
Na zaidi ni kwamba hata wanajeshi waliokamata hatamu za utawala huko Khartoum baada ya Bashir wamehakikisha kwamba hawatamkabidhi mtawala huyo aliyepinduliwa kwa Mahakama ya The Hague.
Bashir kwa mshangao wa watu wengi, alikuwa madarakani kwa muda mrefu. Baada ya Sudan Kusini kujitenga sehemu nyingine za Sudan zilibakia kuwa pamoja.
Kwa hiyo, ugaidi na mapigano katika Darfur yaliyafunika mapigano yaliyokuwa yakiendelea katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo.
Nayo Sudan Kusini ikatumbukia katika vita visivyokwisha. Naye Bashir aliitumia ile nafasi ya tofauti zake na marafiki zake wa zamani wenye siasa za kiislamu kujifanya kuwa mpiganaji dhidi ya ugaidi duniani.
Idara zake za usalama na ujasusi zikabadilika kuwa washirika wa kuaminika wa nchi za Magharibi na za kiarabu. Aliidharau ile waranti iliyotolewa na Mahakama ya The Hague na kuiita kuwa ni njama ya kimataifa na hasa nchi za Magharibi kuwazima midomo wazalendo wa Kiafrika.
Bashir alifaulu kwa sehemu kuwashawishi baadhi ya viongozi wa kiafrika kutoyatambua maamuzi ya Mahakama ya The Hague.
Maandamano ya umma yaliyofanywa Sudan miezi iliyopita yamemgharimu Bashir cheo chake, lakini wakati huo huo yamedhihirisha wazi kwamba katika nchi hiyo bado madaraka yanatokea kwenye mtutu wa bunduki na kwamba jeshi ndilo lenye kuamua nani atawale. Urithi wa Bashir bado ungaliko, haujatetereka.
Vipi mwenendo wa demokrasia utakavyokuwa huko Sudan baada ya Bashir bado si jambo lililo wazi, kama ilivyokuwa kabla ya kuangushwa Bashir. Wasudan sasa wako katika njiapanda, lakini ni wazi kwamba watu wote wenye ushawishi wa kisiasa na wa kiuchumi katika nchi hiyo hawataki kuwa upande wa wale watakaopoteza na kula hasara katika sakata hili la sasa.
Wazi pia ni kwamba Sudan katika muda mfupi ujao haitokuwa tulivu. Bashir ni rais watatu wa Sudan ambaye ameingia madarakani kupitia mapinduzi na amepoteza madaraka kupitia mapinduzi.
Jambo moja tusilisahau kulitaja, hata hivyo Nalo ni mchango mkubwa wa wanawake wa Sudan katika kuuondosha udikteta na dhuluma iliyokuwako katika utawala wa Omar Hassan al-Bashir.
Wanawake wamekuwa mbele kabisa katika mapinduzi ya karibuni na pia kwa muda mrefu katika kupigania kuleta mabadiliko. Kweli watu watabaka mbalimbali za jamii walishiriki katika maandamano ya kutaka Bashir aondoke madarakani, lakini wengi wao waliokwenda mabarabarani walikuwa wanawake na wanafunzi.
Mapambano ya wanawake kutaka kuwa na haki sawa kwa kila Msudan yalikuwa ni sehemu ya uasi wa kisiasa wa wananchi dhidi ya serikali. Nusu ya waandamanaji wa karibuni walikuwa wanawake waliodai ziondoshwe pia dhuluma walizokuwa wakifanyiwa.
Mwanafunzi wa kike, Alaa Salah (22),alichomoza kuwa alama ya vuguvugu la mapinduzi dhidi ya utawala wa Bashir. Sauti yake ilisikilizwa na maelfu ya Wasudan pale alipoushambulia utawala wa Bashir kwa kuwabagua wanawake.
Aliwatia moyo wanawake wabebe mustakabali wao katika mikono yao wenyewe na wasiogope kukamatwa. Alaa Salah alitishwa mara kadhaa kuuliwa au kutupwa gerezani kutokana na msimamo wake wa kisiasa.
Wanaharakati mara kadhaa wamelalamika juu ya hali mbaya wanayokutananayo wafungwa wa kike katika magereza ya Sudan ambayo yamesheheni wafungwa. Licha ya hayo yote wanawake wamekuwa mbele kabisa katika kupigania uhuru na mabadiliko ya kisiasa.
Katika maandamano ya karibuni yalishiriki makundi ya kisiasa ambayo kabla ya utawala wa Bashir yalikuwa yanapigania kuboresha hali ya wanawake katika Sudan. Chama cha wanawake wa Sudan kiliundwa tangu mwaka 1952 na kimetoa mchango mkubwa katika kuboresha hali za wanawake katika maisha ya kisiasa nchini humo.
Mwaka 1965 wanawake kwa mara ya kwanza waliweza kugombea ubunge na Fatima Ahmed akawa mbunge wa kwanza wa kike katika nchi hiyo. Baadaye wanawake wakapata haki mbalimbali, ikiwemo ile ya kufanya kazi.
Licha ya vizingiti walivyowekewa wanawake katika kuzidisha sehemu ya wanawake katika siasa, maendeleo yaliyopatikana yalianza kuwekewa vizuizi katika utawala wa Bashir. Mapambano dhidi ya ukeketaji katika Sudan hayajapiga hatua kubwa mbele. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Watoto Duniani (UNICEF) mwaka 2013 katika Sudan na Sudan Kusini asilimia 88 ya wasichana na wanawake walio katika umri baina ya miaka 15-49 walikeketwa.
Wanawake katika maandamano ya karibuni huko Sudan walinyanyua juu sauti zao na wakahakikisha kwamba wanapatiwa nafasi inayostahili katika Sudan ya siku za mbele.
Wanawake wa nchi hiyo sasa wanataka kwamba nusu ya mawaziri katika serikali ijayo ya kiraia lazima wawe wanawake. Kama wito huo utasikilizwa na wanaume na hasa na wanajeshi ni jambo la kungoja na kuona.