MEXICO CITY, MEXICO
WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Mexico, Luis Videgaray ameionya Marekani kuwa watazitoza ushuru bidhaa za Marekani iwapo Rais Donald Trump atafanya hivyo kwa zile za Mexico.
Trump alitoa tishio hilo ili kuwezesha ujenzi wa ukuta wa mpakani baina ya mataifa hayo, iwapo Mexico itagomea kuulipia.
Waziri huyo amenukuliwa akizungumza na radio moja nchini hapa, akisema taifa lake linakabiliwa na tishio na hivyo Serikali ya Mexico itabidi kuchukua hatua.
Mataifa hayo mawili jirani yapo katika tofauti kubwa ya kidiplomasia, kufuatia msisitizo wa Trump kuwa Mexico inapaswa kulipia ujenzi wa ukuta wa umbali wa kilometa 3,200 katika mipaka yake.
Serikali ya Rais wa Mexico Enrique Pena Nieto imelaani vikali hatua hiyo, ikisema haitaulipia kamwe huo, hatua ambayo ilimkasirisha Trump aliyeapa kuliadhibu taifa hilo jirani kwa kuzitoza ushuru mkubwa bidhaa za Mexico ziingiazo Marekani.