24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Messi atangaza kustaafu soka

Lionel Messi
Lionel Messi

NEW YORK, MAREKANI

BINGWA mara tano wa tuzo ya Ballon d’Or, Lionel Messi, ameshtua dunia kwa kutangaza kustaafu soka la timu ya Taifa ya Argentina baada ya timu hiyo kupokea kichapo katika mchezo wa fainali ya Copa America dhidi ya Chile.

Mwaka wa pili mfululizo timu hizi zinakutana katika fainali ya Copa America huku Chile ikionesha ubabe dhidi ya vigogo hao wa soka duniani.

Fainali hiyo ambayo ilipigwa jana alfajiri nchini Marekani, Chile iliibuka na ushindi wa mabao 4-2 kwa mikwaju ya penalti baada ya kumalizika dakika 120 timu hizo zikienda suluhu.

Nahodha wa Argentina, Messi alikosa penalti na Lucas Biglia kwa upande wao, wakati Chile, Arturo Vidal alikosa na kufanya penalti kuwa 4-2.

Kutokana na hali hiyo, Messi ametangaza kustaafu soka la timu ya Taifa kwa kushindwa kuipa taji la kimataifa katika fainali tatu alizoipeleka timu hiyo, huku ikiwa mara mbili kwenye Copa America na mara moja katika fainali ya Kombe la Dunia.

“Huu ni muda wangu wa kusema kwaheri timu ya Taifa, kwa kuwa nimefika mara tatu kwenye fainali nikiwa na Argentina lakini nimeshindwa kutwaa taji lolote, nimeona bora nifanye maamuzi haya, kuipa ubingwa timu ni jambo ambalo nilikuwa nalitaka lakini halijatokea, nimeumia sana kushindwa kuipa ubingwa Argentina,” alisema Messi.

Messi hadi sasa amecheza michezo 113 akiwa na timu ya Taifa tangu mwaka 2005 na kuifungia mabao 55.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Amerika ya Kusini, mbali na Messi kutangaza kujiuzulu timu ya taifa, kuna baadhi ya wachezaji wengine wamedai kuungana na mchezaji huyo kuachana na timu hiyo.

Wachezaji ambao wapo tayari kuachana na timu hiyo ni pamoja na mshambuliaji wa Manchester City, Sergio Aguero, Javier Mascherano, Angel Di Maria, Ezequiel Lavezzi, Gonzalo Higuain na Lucas Biglia.

Katika fainali hiyo, mshambuliaji wa Chile na klabu ya Arsenal, Alexis Sanchez, ameibuka mchezaji bora wa michuano hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles