LIVERPOOL, ENGLAND
KOCHA mpya wa Liverpool, Jurgen Klopp, anaendelea kuboresha kikosi chake kwa ajili ya msimu mpya wa ligi, huku mshambuliaji wa timu ya Southampton, Sadio Mane, jana alikuwa anafanyiwa vipimo kwa ajili ya kujiunga na majogoo hao wa jiji la Liverpool.
Liverpool ilitangaza kuweka mezani kitita cha pauni milioni 30 kwa ajili ya kumnasa mshambuliaji huyo raia wa Senegal.
Klabu hiyo inaweza kumtangaza rasmi mchezaji huyo muda wowote kuanzia leo, ambapo ataungana na wachezaji wapya ambao wamesajiliwa kipindi hiki cha majira ya joto chini ya kocha Klopp, Marko Grujic, Joel Matip na Loris Karius.
Mshambuliaji huyo msimu uliopita alifunga mabao 15 katika michuano yote, huku akifunga jumla ya mabao manne dhidi ya Liverpool katika michezo ambayo walikutana msimu mzima.
Mchezaji huyo ataingia kwenye rekodi ya wachezaji ambao wamesajiliwa kwa fedha nyingi ndani ya klabu hiyo, Andy Carroll, alisajiliwa kwa kitita cha pauni milioni 35 mwaka 2011, huku Christian Benteke akilamba pauni milioni 32.5 mwaka 2015.