31.2 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Mbinu mpya zaipa jeuri Yanga

SIMBA-YANGA-3ADAM MKWEPU NA THERESIA GASPER, DAR

KOCHA Mkuu wa timu ya Yanga, Hans van der Pluijm, amesema alilazimika kubadili mbinu wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar ili kuwapima wachezaji wake kabla ya kurudiana na miamba ya soka barani Afrika, Al Ahly ya Misri.

Kabla ya kuondoka jana saa 7.00 mchana kuelekea Cairo, Misri kwa maandalizi ya mchezo wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, Yanga ilitoa kipigo cha bao 1-0 kwa Mtibwa katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo wa marudiano unatarajiwa kuchezwa keshokutwa katika Uwanja wa Jeshi wa Borg Al Arab uliopo jijini Alexandria, ambapo Yanga wanahitaji ushindi au sare ya zaidi ya bao moja ili iweze kusonga mbele katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Akizungumza na MTANZANIA jana kabla ya kuondoka, Pluijm alisema walitumia mchezo wa juzi kupata mbinu za kuimaliza Al Ahly mapema ambapo lengo kubwa lilikuwa ni kuimarisha safu ya ulinzi na kutaka kufanya mashambulizi ya kushtukiza washambuliaji watakapopata nafasi ya kufunga.

“Kipindi cha kwanza tulianza kwa kuchezesha washambuliaji wawili wakati safu ya ulinzi ikiwa chini ya mabeki watatu ambao ni Vicent Bossou, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani.

“Lakini kipindi cha pili tulibadili mfumo wa uchezaji ambapo tulimtumia mshambuliaji, Donald Ngoma, mbele ili kupima na kuangalia kiwango vya wachezaji kabla ya mchezo wa kimataifa,” alisema.

Hata hivyo, kocha huyo raia wa Uholanzi, alisema anaweza kuwa na aina tofauti ya ushambuliaji na kuzuia huku akieleza kwamba nidhamu pia inaweza kuchangia kupatikana kwa ushindi ugenini utakaowafanya waondoke kifua mbele dhidi ya Al Ahly.

“Tulijua mechi dhidi ya Mtibwa itakuwa ngumu hivyo tulihitaji umakini mkubwa, tuliingia uwanjani kwa lengo la kufanya mashambulizi ya kushtukiza kwani wapinzani wetu walitupania sana,” alisema.

Pluijm alisema lengo lao ni kuhakikisha wanamaliza Ligi Kuu wakiwa vinara ili kutetea taji la ubingwa wanaoushikilia kwa sasa.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu, wamelazimika kufanya maboresho kwenye kikosi hicho kabla ya kurudiana na Al Ahly ambao waliwabana nyumbani na kulazimishwa sare ya bao 1-1.

Wakati huo huo, wawakilishi wengine wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC tayari wamewasili nchini Tunisia kwa maandalizi ya mchezo wa marudiano dhidi ya Esperance.

Katika mchezo wa awali uliochezwa Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam, ‘Wanalambalamba hao’ waliibuka na ushindi wa mabao 2-1, hivyo watahitaji ushindi au sare ya aina yoyote ugenini ili waweze kusonga mbele.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles