Na Mwandishi Wetu, Geita
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamushikilia mama mmoja anayefahamika kwa jina la Angelina Masumbuko kwa kosa la kuiba mtoto wa wiki mbili kwa mama Juliana Malichades kulenga kumuridhisha mme wake na kuokoa ndoa yake.
Akielezea tukio hili jana, Kamanda Mkuu wa Polisi Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe alisema mama huyo alitenda kosa hilo siku ya tarehe 12 mwezi huu na alipohojiwa ameweka wazi kuwa alifikia maamuzi hayo kwani ndoa yake ilishaanza kuyumba kwa kukosa mtoto.
Kamanda Mwaibambe alisema kabla ya kutenda kosa hilo taarifa zinaonyesha mtuhumiwa baada ya mwenzake kujifungua aliweka mazoea ya ghafla kwenda kumtembelea na kumsaidia shughuli za ndani ingawa hawakuwa wakifahamiana vizuri na mazoea ya aina hiyo hayakuwepo.
“Siku moja mama wa mtoto akiwa nje amemlaza mtoto ndani, alikuja hakumukuta mtoto, majirani kwa kushirikiana na huyu mama walimtilia wasiwasi mama ambaye alikuwa anakuja kusaidia kazi, kwani yeye ndio alikuwa ameleta mazoea kwa mtoto kwa hiyo aprili 22 mwaka huu akakamtwa akiwa na huyo mtoto.
“Huyo mtoto tulimpeleka hospitali, tukampima na akaonekana ana afya njema ikabidi huyu mtoto tumkabidhi kwa mama yake, tukamhoji mtuhumiwa kwa nini umefanya kitendo hiki cha kuiba mtoto, akadai yeye ndoa yeke inayumba, mme anahitaji mtoto kila wakati, hivyo alifanya kumuridhisha mme wake,” alieleza Mwaibambe.
Katika tukio jingine jeshi la polisi linamshikilia Stephano Gerlad (32) kwa kosa la kusababisha kifo cha mtoto wake mwenye umri wa miaka nane tukio ambalo lilitokea usiku wa kuamkia tarehe 28 aprili wakiwa wanapigana na Ziada Haruna ambaye ni mke wake.
“Wakiwa wanapigana na mke wake, waliangushana na kwenda kumlalia huyu mtoto, ambaye alikuwa amelala usingizi na mtoto akakosa hewa akafariki na mama wa mtoto kutokana na ugomvi huo amelazwa kituo cha afya bwanga na hali yake inaendelea vizuri,” alisema Mwaibambe.
Aidha, Jeshi la Polisi linachunguza kifo cha Beatrice Sylivanus ambaye ni mfanyabiashara aliyekutwa ameuwawa barabarani tarehe 28 majira ya saa nne usiku muda mfupi baada ya kushushwa na bodaboda iliyompeleka nyumbani kwake akiwa na mtoto wake mgongoni.
“Uchaguzi wa awali umebaini marehemu alipigwa na kitu kizito kichwani alipokuwa akirejea nyumbani ambapo jeshi la polisi linamshikilia mtu mmoja anayefahamika kwa jina la Fikiri Elieza ambaye ni dereva bajaji mkazi wa Mwabasabi wilayani Geita mkoani hapa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.